MAOMBI MAALUMU (Day 13)

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 



Kipengele: MAOMBI YA KUOMBEA SADAKA ULIZOWAHI KUTOA.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe!
Najua unafahamu kuhusu sadaka.
Hebu soma somo hili kwa utulivu Kisha Maombi, somo hili ambalo Mimi Peter Mabula nakuletea Wewe rafiki yangu ni Ufunuo wa wazi ambao nilipewa kwa habari ya kutoa Sadaka na kuiombea hiyo Sadaka.

✓✓Kuna sadaka ya fungu la kumi, kuna sadaka ya kawaida(Sadaka ya dhabihu) na sadaka zingine kulingana na maelekezo ya ulimwengu wa roho wa Nuru.

Kabla ya yote ngoja nikuonyeshe faida ya sadaka mojawapo.

Ezekieli 44:30 "Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu
cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga
mbichi, ili kukalisha baraka juu ya nyumba yako."

✓✓Biblia inasema hivi "ILI BARAKA IWE JUU YA NYUMBA/FAMILIA YAKO TOA SADAKA YA MALIMBUKO"
Maana yake sadaka hii utasababisha MUNGU aikalishe baraka juu ya nyumba Yako yaani familia Yako.

Sasa inawezekana umekutana na Neno la MUNGU likikutaka usiache kutoa sadaka yako au zaka yako mwaka baada ya mwaka
Kumbu 14:22 " Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka."
Ila hujui kazi yake kiroho.

Wakati mwingine umekutana na Neno la MUNGU likisema kwamba sadaka ni takatifu kwa MUNGU lakini wewe hujui faida za kutoa hiyo sadaka au zaka na unajiuliza je MUNGU kweli anahitaji sadaka na zaka za nini.

Walawi 27:30 "Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; ni takatifu kwa BWANA."

Wakati mwingine unajiuliza kwanini MUNGU ameagiza kwamba zaka au fungu la kumi wapewe watumishi na ni haki yao siku zote.

Hesabu 18:21" Na wana wa Lawi(Makuhani), nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania."

◼️Najua unafahamu kwamba sio kila mahali unaweza kutoa matoleo yako bali kule ambalo ROHO wa MUNGU atakupa msukumo rohoni ili utoe.
Kumbu 12:13-14 "Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; bali katika mahali atakapopachagua BWANA katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo."
Japokuwa umesikia msukumo rohoni kutoa lakini unashindana na maagizo hayo ndani ya roho yako, unajiuliza kwanini umapewa maagizo ya kiroho kutoa matoleo yako?

◼️Ni kwa sababu sadaka ni jambo la kiroho na lenye faida nyingi za kiroho.

Mawakala wa shetani nao kwa kujua baadhi ya kazi za sadaka kiroho ni rahisi kumfunga mtu kupitia sadaka.
◼️Moja ya mambo ya kujua kuhusu sadaka ni kwamba moyo huambatana na sadaka iliko.
Mathayo 6:21" kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako."

Aliyeyasema haya ni Bwana YESU KRISTO Mwokozi mwenyewe akitutaka tutoe sadaka zetu kwenye ufalme wa MUNGU maana kwa njia hiyo sehemu ambako sadaka zetu zitakuwa na roho zetu zitakuwa huko, ni jambo jema sana kutoa matoleo yetu kwa MUNGU katika KRISTO YESU.

Lakini kwa sababu moyo(nafsi) huifuata sadaka basi ukitoa sadaka kwa mashetani ujue moyo wako unaifuata sadaka hiyo huko.

✓Ukitoa kwa mganga ujue moyo wako unaifuata sadaka yako huko.

✓Kwa sababu sadaka huhusika kutengeneza agano basi ujue sadaka yako inaweza kutengeneza agano kati yako na nguvu za giza.

✓Kuna watu hawakuwahi kuhusika na nguvu za giza ila matambiko ya ukoo yalizifanya nguvu za giza kuwafuatilia. Na matambiko huhusisha sadaka na damu ya sadaka hizo za kipepo.

✓Kuna watu hawakuwahi kuhusika na nguvu za giza ila walidanganywa na kutoa vitu(Sadaka) vyao kwa mashetani.

Kuna watu walikwenda kwa waganga wa kienyejj ili kuzifuata nguvu za giza  kwa wao kutoa sadaka/kafara au chochote kwa mganga basi hadi muda huu nafundisha somo hili wao wanamilikiwa na nguvu za giza.

Kupitia matambiko na mazindiko na mambo yote ya uganga wa kienyeji watu wengi hujikuta wameambatanisha na uzao wao kwa mashetani.
Zaburi 106:37 "Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani."

Mwanamke mmoja kwenye ulimwengu wa roho Mara nyingi alijiona kuzimu huku mapepo wakimtesa, wakisema kwamba wana uhalali maana walikabidhiwa ukoo na babu yake huyo mwanamke kupitia tambiko lenye sadaka nzuri.

Katika ulimwengu wa mwili ni mateso mengi sana amekutana nayo.

Sadaka kumpa mtu ambaye hujamthibitisha kama ni Mtumishi wa MUNGU wa kweli katika KRISTO YESU ni jambo la hatari sana.

Mimi binafsi kuna vipindi tofauti kuna watu ambao ni marafiki zangu Facebook, mtu wa kwanza siku moja aliandika meseji inbox zaidi ya 5 akiomba nimtumie Tsh 5,000 au 2,000 na anashida nayo sana, hajala tangu asubuhi, roho yangu ikawa nzito sana hivyo nikakaa karibu masaa 4 bila kumjibu huyo ndugu, baadae nikafungua profile yangu na kukuta amepost muda mfupi uliopita akiwa na gari yake nzuri na akiwa na familia yake wakila chakula, maelezo tu aliyoandika yanaonyesha wala hakuhitaji 2000 kwa sababu hana, baadae nilijua ni hila za shetani, maana nafsi yako inaweza hata kuambatana na sadaka yako kwenda kwa mchawi.
Mtu mwingine siku moja alinitafuta sana akiomba pesa ya kununua dawa anaumwa, ni tsh 5000 nikamwambia anipigie nimuombee na atapona, akakataa kuombewa, baadae nilijua pesa yangu inatafutwa kama sadaka ili kuifunga huduma yangu kiroho.

Kwa sasa watu wa namna hiyo ni wengi sana na huwa hata siwajibu maana najua wanachotafuta.

Kumbuka pia kutokutoa sadaka mbalimbali kwa MUNGU ni hatari sana kwako kuliko ukitoa, hivyo usiache kamwe kutoa Sadaka kwa MUNGU katika KRISTO YESU, Muhimu hapo ni huyo Mtumishi unayempa mthibitishe kuwa ni Mtumishi wa kweli wa Bwana YESU KRISTO.

Ndugu kutoa kwa MUNGU katika KRISTO YESU ni muhimu sana na ina faida sana kwako kiroho lakini zingatia sana kwamba sio kila mtu wa kumpa sadaka yako, ukimpa Mtumishi wa shetani ujue na moyo wako unaweza kuambatana na sadaka yako katika madhabahu ya shetani, ni hatari sana usipojua kuomba katika jina la YESU KRISTO na ukitumia damu ya YESU KRISTO ya agano ili kujinasua.

Sadaka katika KRISTO zina kazi yake kiroho ndio maana watu wa MUNGU tangu zamani walitoa sadaka.

✓✓Sadaka ni hitajio la kiroho japokuwa wengi hawajui.

Jambo la kwanza kujua ni kwamba hakuna agano bila sadaka, yaani agano lolote haliwezi kusimama kama hakuna sadaka zetu.

Kwanini leo tuombe juu ya sadaka tulizowahi kutoa?

1. Sadaka hunena.

Waebrania 11:4 "Kwa imani Habili alimtolea MUNGU dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; MUNGU akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena."

Ingawa Habili alikufa lakini sadaka alizokuwa ametoa kabla kwa MUNGU ilisababisha awe ananena, kwa sababu ya Sadaka 

Ni kama sadaka ya Ibrahimu iliyotengeneza agano na MUNGU na agano hilo likakumbukwa Miaka mingi baadae kwa ajili ya Uzao wake.

Kutoka 2:24-25 " MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. MUNGU akawaona wana wa Israeli, na MUNGU akawaangalia."

MUNGU alikumbuja agano likilotengenezwa na Sadaka, hiyo ndio maana ya kusema sadaka inazungumza.

Sadaka ya Habili ilikuwa inanena, hata sadaka yako inaweza kunena.
Kama ulitoa sadaka kwa MUNGU ielekeze sadaka yako inene mema juu ya nini.
Kama ulitoa sadaka kwa mashetani na hiyo sadaka ya kipepo inaendelea kunena basi ifute hiyo sadaka kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.


2. Kuna sadaka ulitoa kwa MUNGU kama mbegu ili ziote na ujue uvune.

2 Wakorintho 9:6 "Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu."

Kama ulitoa sadaka ya namna hii kwa MUNGU basi omba kupewa nguvu na uwezo wa kuvuna kama ulivyopanda.

3. Kwa sababu ni heri(baraka) kutoa kuliko kupokea, omba MUNGU akupe uheri unaotokana na kutoa kwako.

Matendo 20:35" Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana YESU, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea."

4. Kwa sababu sadaka kuitoa kwa MUNGU hutengeneza agano na MUNGU basi imalisha agano hilo kwa Maombi na utakatifu.

Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."

Kinyume chake ni kwamba kama ulitoa sadaka kwa mawakala wa shetani na sadaka hiyo ikatengeneza agano na mashetani basi futa agano hilo la kipepo kupitia sadaka yako, lifute agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.

5. Utoaji humfanya MUNGU awakemee maadui zako.

Malaki 3:11 "Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi."

Hivyo mwambie MUNGU awakemee maadui zako(wataje), na akiwakemea MUNGU maana yake hawatakugusa tena.
Maadui kama magonjwa na maroho wote wa kuzimu na hata wanadamu wanaotumika kipepo.
Nina mengi sana ila kwa leo ngoja niishie hapo.
Usiache kutoa zaka na sadaka ila to a kwa Mtumishi wa MUNGU aliye hai.
Omba katika maeneo hayo 5 na MUNGU wa Mbinguni atakutendea Muujiza wako uliotokana na Sadaka zako.
MUNGU akubariki sana sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU wa Mbinguni.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili, Ushauri, Maombi, Whatsapp n.k)
Ubarikiwe sana.

Comments