![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Kipengele: MAOMBI YA KUZIITA AHADI ZA MUNGU ALIZOKUAHIDI.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Leo tunaomba kuhusu ahadi njema alizotuahidi MUNGU Baba yetu wa mbinguni.
Ahadi za MUNGU ni nini?
■Ahadi za MUNGU ni yale mambo mema ambayo MUNGU katika KRISTO YESU alisema atakutendea.
Mfano hai ni MUNGU alitimiza hata na kuzidi juu ya ambayo Solomoni aliyaomba kwa MUNGU.
1 Wafalme 3:13 "Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote."
■Ahadi za MUNGU kwako ni agano au patano au kauli ya MUNGU kupitia ROHO MTAKATIFU aliyoisema kuwa atatimiza.
Mfano MUNGU aliahidi kuwabariki Ibrahimu na Sarah mtoto wa kiume na ikawa hivyo, haijalishi umri wa Sarah kuzaa kibinadamu umri ulivuka, Sarah alikuwa kikongwe lakini alizaa mtoto wa kiume kama ahadi ya MUNGU kwao ilivyokuwa.
Mwanzo 18:10" Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake."
Kuhusu ahadi za MUNGU kumbuka hii.
●Siku zote ahadi za MUNGU ni ndio na kweli.
2 Wakorintho 1:20 "Maana ahadi zote za MUNGU zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; MUNGU apate kutukuzwa kwa sisi."
●Siku zote MUNGU hawezi kuahidi uongo.
1 Wafalme 8:24 "Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo."
Je wewe unayejifunza somo hili, MUNGU alikuahidi nini?
Inawezekana MUNGU alisema na wewe kwa ndoto au maono au kupitia watumishi wake waaminifu, inawezekana MUNGU alikupa ahadi kupitia andiko n.k
■Ndugu, MUNGU akikuahidi kitu hutimiza.
■Bwana YESU KRISTO akikuahidi kitu hakika atatenda.
■ROHO MTAKATIFU akikuahidi kitu ujue hakika atatimiza.
●Japokuwa MUNGU akiahidi kitu atatimiza lakini ni vyema kutambua jambo hili muhimu sana kwamba anayeweza kuchelewesha kutimia ahadi ya MUNGU kwako ni wewe mwenyewe.
●Lakini pia ni wewe mwenyewe unaweza pia hata kuifuta ahadi ya MUNGU kwako na isitokee kamwe hata kama MUNGU aliahidi.
Kwa njia gani ahadi ya MUNGU aliyokuahidi inaweza isitimie kwako au ichelewe?
1. Dhambi zako zinaweza kuichelewesha ahadi njema ya MUNGU kwako au dhambi zako zinaweza kuifuta kabisa ahadi ya MUNGU kwako usipotubu na kuacha dhambi.
Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
2. Kumwacha YESU KRISTO/Kuacha Wokovu kunaweza kufuta ahadi za MUNGU kwako na hata na mema uliyotenda yasikumbukwe mbele za MUNGU.
Ezekieli 18:24 "Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa."
3. Ahadi za MUNGU kwako zinaweza kuchelewa kutimia au zinaweza kutokutimia kwa sababu umelikimbia kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU na wakati huo hilo kusudi la MUNGU limebeba majira ya kupokea kwako ahadi ya MUNGU aliyokuhidi.
Mhubiri 3:1 "Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."
Ndugu, je MUNGU katika ROHO MTAKATIFU alikuahidi nini?
Kuna waliokuwa wagonjwa sana lakini MUNGU akawaahidi uponyaji na wakapona.
Zaburi 119:170 "Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako."
Kuna Bwana YESU KRISTO aliahidi kuwatetea dhidi ya mawakala wa shetani na akawatetea na kuwashindia.
Zaburi 119:154 "Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako."
Je wewe uliahidiwa nini na MUNGU katika KRISTO YESU?
Je wakati wa maombi yako ya mkesha au wakati wa. Maombi yako ya kufunga au wakati ulipotoa sadaka au wakati ulipokuwa katika uwepo wa nguvu za ROHO MTAKATIFU uliahidiwa nini na MUNGU?
Wako walioahidiwa kufunga ndoa, hata kama watu wote wanakuona wewe ni mbaya na hakuna wa kufunga ndoa na wewe, kama YESU
amesema utafunga ndoa hakika itakuwa.
Wako walio tasa au wagumba na vipimo vyote vya hospitali vinaonyesha hawawezi kuzaa au umri wa kuzaa umewapita, kama YESU KRISTO amekuahidi kwamba utazaa hakika utazaa.
Kuna ahadi nyingi za MUNGU na inawezekana uliahidiwa ahadi mojawapo au ahadi mbili au zaidi, ndugu ukikaa katika utakatifu na maombi hakika MUNGU Baba atatimiza ahadi zake.
ROHO MTAKATIFU alikuahidi kitu ujue kitatimia.
Bwana YESU KRISTO alikuahidi baraka fulani hakika itakuwa.
MUNGU akikuahidi hakika hutumiza maana MUNGU sio mwanadamu hata aseme uongo.
Hesabu 23:19 "MUNGU si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?"
■Ahadi za MUNGU ziko nyingi sana na ahadi kuu ni hii kwamba ukimpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na ukaishi maisha matakatifu katika yeye hakika ahadi ya MUNGU kwako ni uzima wa milele.
1 Yohana 2:25 "Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele."
Nini ufanye ili ahadi ya MUNGU kwako itimie?
1. Tubu dhambi zilizozuia ahadi hiyo isitimie, na ziache dhambi zote.
Zaburi 119:58 "Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako."
2. Hakikisha uko ndani ya YESU KRISTO kwa usahihi.
Yohana 15:4 "Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu."
3. Mtii na kumsikiliza sana ROHO MTAKATIFU.
1 Wakorintho 2:10" Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."
4. Omba MUNGU atimize ahadi yake kwako aliyokuahidi.
Zaburi 119:41" Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako."
5. Kama ahadi hiyo ya MUNGU kwako sio ya wakati huu mngoje MUNGU, vumilia huku ukiomba na kuishi maisha matakatifu.
Waebrania 6:15" Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi."
6. Ki maombi iite hiyo ahadi ya MUNGU kwako ili itimie.
Zaburi 119:76 "Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako."
7. Kaa katika kusudi la MUNGU.
Mwanzo 18:19 "Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake."
8. Ukiendelea kutii Neno la MUNGU na kuliishi hakika ahadi za MUNGU zote alizokuahidi zitatimia kwako.
1 Wafalme 3:14 "Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi."
Katika points hizo hapo juu sehemu inayokuhitaji kuomba basi fanya maombi na sehemu inayokuhitaji kufanyia kazi basi fanyia kazi.
MUNGU akubariki sana sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.
+255714252292
Omba katika jina la YESU KRISTO na utamuona MUNGU wa miujiza.
Ubarikiwe.

Comments