![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele  | 
Kipengele: MAOMBI YA KUONDOA MAPEPO YA UDHAIFU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Kuna makundi mengi ya pepo wabaya wanaovamia wanadamu(Waefeso 6:12), kundi mojawapo la baadhi ya nguvu hizo za giza linaitwa mapepo ya kuleta udhaifu.
Kazi ya mapepo wa udhaifu ni kuleta udhaifu, ulemavu wa viungo n.k
Luka 13:11 "Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. YESU alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza MUNGU."
Mama huyu alikuwa mgonjwa anayetembea amepinda, na kumbe chanzo cha ugonjwa wake ni mapepo ya udhaifu, YESU KRISTO katika kumponya hakusema " Pokea uponyaji" bali alijua tatizo ni mapepo ya udhaifu yaliyokuwa ndani ya huyu mama kwa miaka mingi, yalipotoka yale mapepo ya udhaifu mama yule akapona tangu saa ile ile.
✓✓Leo kuna watoto hawawezi kutembea na hospitalini wakipelekwa hauonekani ugonjwa, kumbe ni mapepo wa udhaifu.
✓✓Kuna ndoa zimevamiwa na mapepo ya udhaifu.
✓✓Kuna miili ya watu imevamiwa na mapepo ya udhaifu.
✓✓Kuna biashara nzuri za watu ila zimevamiwa na mapepo ya udhaifu.
Kuna maeneo mengi kwa watu wa MUNGU kunaweza kuvamiwa na mapepo ya udhaifu.
Kwa sababu mapepo ya udhaifu kazi yake ni kuleta udhaifu au ulegevu basi kuna watu akishika tu Biblia ili kusoma analala muda huo huo hata kama ndio asubuhi ameamka, inawezekana zamani hakuwa hivyo ila hiyo hali imempata kuanzia siku za karibuni, mapepo ya udhaifu ndio yanamzuilia kujifunza Neno la MUNGU. Ukitaka kujua kama ni mapepo ya udhaifu ni kwamba muda ule ule anaposoma Biblia anapata usingizi ghafla na kuwa mlegevu, ukimpa kitabu cha riwaya aipendayo usingizi unaisha saa ile ile na akishika kitabu cha riwaya kusoma anaweza kusoma masaa 3 mfululizo bila kuchoka wala kupiga miayo.
Watu wa MUNGU wengi sana wamevamia na mapepo ya udhaifu, mfano
Kuna mteule zamani alikuwa anaweza kuomba masaa 3 bila kuchoka lakini kwa sasa maombi yake mwisho ni dakika 2 anakuwa amechoka sana.
Kuna watu sadaka kwa sasa hutoa Tsh 200 lakini zamani mtu huyo huyo kila siku ya ibada sadaka yake ilikuwa elfu kumi au zaidi, sio kwamba uchumi umeyumba bali ndio uchumi wake sasa umeimalika sana ila amevamiwa na pepo la udhaifu katika utoaji.
Kuna watu kila siku ya ibada anadai amechoka, zamani haikuwa hivyo.
Kuna mtu ibadani akiambiwa "Simama tuombe" hawezi wakati maombi hayo ni dakika 5 tu, lakini mtu huyo huyo akitoka ibadani utamuona nje tu ya Kanisani kasimama na rafiki yake wanapiga story masaa mawili wamesimama bila kuchoka, lakini ndani ya ibada kusimama dakika 5 hawezi.
Kuna watu ibadani kila muda anaangalia saa amechoka wakati ibada yenyewe ni masaa 3 tu yaani saa nne hadi saa saba.
Mapepo ya udhaifu kwa sababu ni nguvu za giza humpa mtu udhaifu kwenye mambo muhimu tu ya ki MUNGU yenye msaada, lakini kwenye mambo ya kishetani hayo mapepo humwongezea nguvu, ndio unaweza kumkuta mtu hawezi kusoma kurasa mbili za Biblia bila kuchoka, lakini mtu huyo huyo anaweza kusoma kitabu kizima cha story za mapenzi au udaku bila kuchoka tena anasoma kitabu kizima kwa siku moja.
Hata kwangu Mimi Peter Mabula kabla sijampokea YESU KRISTO kama Mwokozi mwaka 2008 nilikuwa naweza kusoma kitabu kizima cha story kwa siku moja lakini kusoma kurasa 3 za Biblia siwezi, namshukuru sana Bwana YESU KRISTO Mwokozi maana aliniponya katika hilo.
Mapepo ya udhaifu humruhusu mtu kufanya mambo yasiyo na faida kwake kiroho.
Kuna watu kazini kwake anaweza kusimama masaa 6 mfululizo lakini kuwa kanisani / ibadani dakika 10  anajisikia uchovu.
Ndugu kama unasumbuliwa na mapepo ya udhaifu leo tumia jina la YESU KRISTO kuziamuru hizo nguvu za giza zikuachie.
Mathayo 17:18" YESU akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile."
Kazi za mapepo ya udhaifu ni pamoja na hizi.
1. Kumfanya mtu ayaone mambo mema kuwa mabaya na mambo mabaya kuwa mema.
Marko 5:2-3 "Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;"
Mtu huyu alikuwa anapenda kukaa makaburini wakati haitakiwi mtu kuishi makaburini, anapenda uchafu wakati uchafu hautakiwi. Huo ni mfano hai wa mtu mwenye mapepo kupenda vitu vibaya na huku mema akiyaona ndio mabaya.
2. Kumfanya mtu kudhoofika kiroho na kiufahamu na kumfanya mtu huyo kutenda hata ambayo yeye mwenyewe hayapendi.
Warumi 7:15 "Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda."
3. Kumfanya mtu kuishiwa nguvu katika mema.
Mathayo 8:16" Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,"
Hawa walikuwa hawawezi yaani hawana nguvu.
4. Kumfanya mtu kuwa mlegevu.
Mathayo 4:24" Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya."
5. Kumfanya mtu asiwe imara, akose nguvu.
Matendo 8:7 "Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa."
✓✓Kupooza ni mfano hai wa kukosa nguvu.
Mapepo ya udhaifu ni nguvu za giza mbaya sana, leo ki maombi hakikisha unaziondoa nguvu hizi za giza kwako, kwa watoto wako au kwa mwenzi wako.
Inawezekana unamchapa sana mtoto wako ili asome bado hawezi kwa sababu amevamiwa na pepo la udhaifu wa kusoma shule.
Nguvu hizi za giza zinaweza hata kuvuruga ndoa yako kama mke wako au mume wako atakuwa dhaifu katika tendo la ndoa, kumbe chanzo ni pepo la udhaifu.
Baba mmoja asiye mcha MUNGU siku moja aliniambia mambo ya ajabu sana, alisema kwamba amevamiwa na nguvu za giza zinazomfanya kukosa nguvu za kiume akikutana na mke wake tu lakini kwa hawara nguvu za kiume ni nyingi kuliko kawaida mpaka anapanga kuvunja ndoa yake. Nilimwambia kwamba kwa hawara huyo ni njia pana tena nzuri kwake ila ya kwenda jehanamu, nikamwambia arudi kwa mkewe na aende kanisani ili wakamuombee kuyang'oa hayo mapepo ya udhaifu ambayo hufanya kazi ndani ya ndoa yake tu.
Mapepo ya udhaifu yanaweza hata kuvamia uchumba wako kiasi kwamba mchumba wako ghafla hajisikii kufunga ndoa, hataki kufunga ndoa na wewe na hajui kwanini hataki, hana sababu kwanini hataki kufunga ndoa wakati hata mahari ilishatolewa na kamati ya harusi inaendelea.
◼️Pepo la udhaifu likikuvamia unakuwa dhaifu katika mambo mema na yenye faida kwako.
✓✓Mapepo ya udhaifu yanaweza hata kuleta magonjwa yatakayomfanya mtu husika kuwa dhaifu.
Ndugu, kama ni wewe unamhitaji YESU ili upone maana hizi nguvu za giza zipo na zinatesa wengi.
Luka 4:33" Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu,"
◼️Leo kwa jina la YESU KRISTO lenye mamlaka kuu zifukuze hizo nguvu za giza na ziamuru ziende kuzimu na zisirudi tena.
Nini ufanye kwenye maombi yako Leo?
1. Tubu kwa kilichosababisha nguvu hizo za giza zikakuvamia au zikamvamia mtu unayemuombea.
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
2. Kama una nguvu za kuomba ziamuru hizo nguvu za giza zitoke kwako au kwa mtu unayemuombea.
Mathayo 7:7 "Ombeni, nanyi mtapewa; ..........."
3. Kama wewe ni dhaifu kiasi kwamba hata kujifungua vifungo kimaombi huwezi basi watafute watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO watakuombea na utafunguliwa.
Mathayo 10:1" Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina."
4. Funga kimaombi milango ya kiroho waliyotumia mapepo kuingia kwako.
Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."
5. Achilia damu ya YESU KRISTO ya agano ndani yako maana kwa hiyo unamshinda shetani na mawakala zake wote.
Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ........."
MUNGU akubariki sana ukifanyia kazi.
Omba katika Jina la YESU KRISTO utamuona MUNGU wa Mbinguni 
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292
Ubarikiwe sana.

Comments