| Na Mwl Peter Marco Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Maombi ya toba.
KIPENGELE: UMUHIMU WA KUTUBU.
Leo tunachambua Mithali 28:13 ambapo Biblia inasema "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. "
Katika andiko hili tunaona umuhimu mkubwa wa kila mtu kuwa na maombi ya toba na kila mtu kugeuka kutoka mabaya yote na sasa atende mema.
Katika andiko hilo tunajifunza mambo yafuatayo;
1. ANAYEFICHA DHAMBI ZAKE HAWEZI KUFANIKIWA POPOTE.
✓✓Dhambi ni uovu mtu ametenda, ni machukizo yaliyofanyika ambayo mtu asipoyatubia hawezi kufanikiwa katika eneo hilo.
✓✓Dhambi ni uasi kwa MUNGU.
Mtu anayeficha dhambi zake yaani hana muda wa kuzitubia huyo hawezi kufanikiwa maana dhambi huuficha uso wa MUNGU.
Isaya 59:1 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
Mfano ndoa yako ina migogoro kwa ya misingi mibaya ya ndoa yenu, yaani mliingia katika ndoa mkitokea katika uasherati kwa siri, yaani mlikuwa wazinifu, sasa ili MUNGU akusaidie wakati huu unahitaji toba, ukificha dhambi hiyo usiwe na muda wa kutubu hautafanikiwa kupata msaada wa MUNGU hata migogoro iishe.
Kama hujaingia katika ndoa na unasoma somo hili usikubali kufanya dhambi ya uasherati na mchumba wako maana unaweza kupanda magugu ambayo yatakushinda kuyang'oa hata kabla ya ndoa au baada ya ndoa.
Mfano wa pili, wewe umewahi kutoa mimba, miaka imeenda na kwa sasa kila unachofanya kimekataa, huoni mpenyo na kosa lako ni ujinga wako wa kufanya dhambi ya uasherati na kosa lingine kutoa mimba, ndugu kuficha dhambi yako hiyo hauwezi kufanikiwa, waone wachungaji wakupatanishe na MUNGU maana wao wamepewa huduma ya upatanisho ndani yao.
2 Wakorintho 5:18" Lakini vyote pia vyatokana na MUNGU, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa KRISTO, naye alitupa huduma ya upatanisho;"
Mfano mwingine uliharibu Kanisa fulani ukamua kuhama hapo huku ukiwasema vibaya watumishi wa MUNGU, ndugu unaweza kuzunguka hata makanisa 10 na tatizo lako au laana yako imekushikilia, rudi katengeneze kwanza pa mwanzo, kaseme dhambi zako na kutubu ndio uachiliwe na kuhama salama.
Mfano mwingine uliua zamani na kwa sasa unateswa na laana ambayo hata ukiomba hufanikiwi, ndugu kumbuka afichaye dhambi zake hatafanikiwa, waone watumishi wa MUNGU wakusaidie.
2. KUFANIKIWA CHANZO CHAKE NI TOBA NA KUACHA DHAMBI ILI UTENDE MEMA.
Mfano hai ni Ninawi ambao waliendelea kuishi baada ya kutubu na kuacha dhambi.
Yona 3:10 "MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende."
Watu hawa walipangiwa kufa baada ya siku 40 lakini kutubu kwao na kuziacha Dhambi zao ndiko kulifuta dhambi yao hata ilikuwa wafe ila sasa wakaishi, kwa hiyo kutubu dhambi na kuziacha ni chanzo kikuu cha kufanikiwa, hawa walifanikiwa kuishi baada ya kutubu.
Bwana YESU KRISTO baadhi ya watu aliokuwa anawaponya alikuwa anawaambia kwamba "Umesamehewa dhambi zako"
Mfano Mathayo 9:2 "Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye YESU, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako."
Mfano mwingine Luka 7:48-50 "Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani."
Hawa chanzo cha matatizo yao kilikuwa ni dhambi ndio maana Bwana YESU aliwasamehe dhambi ndipo akawaponya.
Toba ndio mlango wa kufanikiwa kutoka katika tatizo, usifiche dhambi bali tubu.
Mfano mwingine wa namna toba inavyoweza kuwa ufunguo wa kufanikiwa kwako ni huu.
Bartimayo kipofu ili aponywe na Bwana YESU KRISTO alisema manenp haya "YESU unirehemu'' hiyo iko katika Marko 10:47 "Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, YESU, unirehemu."
Neno kurehemiwa lina maana yake ni kusamehewa dhambi na kuachiliwa na kuhurumiwa, kipofu hivyo alipona baada ya kutanguliza toba.
Hata wewe mwambie MUNGU akurehemu na atakusamehe kabisa na kukufutia adhabu zilizokuwa zije kwako kwa sababu ya dhambi.
3. MTU ANAYEZIUNGAMA DHAMBI ZAKE NA KUZIACHA HUPATA REHEMA YA MUNGU.
◼️Kuungama ni nini?
✓✓Kuungama ni kukubali kwamba ulitenda dhambi hivyo unahitaji kutubu na kuziacha Dhambi hizo.
✓✓Kuungama ni kukiri mbele za MUNGU katika KRISTO YESU kwamba ulikosea na unahitaji sasa msamaha.
Ili usamehewe na MUNGU inakupasa kuungama, kutubu na kuziacha dhambi zako.
Isaya 55:7 "Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa."
✓✓Lakini usiishie tu leo kutubu kwa ajili ya wizi wako kisha kesho unaendelea na wizi, hiyo sio toba ya kweli.
✓✓Usiishie tu leo kutubia uzinzi wako au uasherati wako kisha kesho unaendelea na uzinifu huo, hiyo sio toba ya kweli.
✓✓Usiishie tu leo kutubu kwa ajili ya utapeli wako kisha kesho unaendelea na utapeli, hiyo sio toba ya kweli.
✓✓Usiishie tu leo kutubu kwa ajili ya ukahaba wako au umalaya wako kisha kesho unaendelea na dhambi hiyo, hiyo sio toba ya kweli.
✓✓Usiishie tu leo kutubu kwa ajili ya uongo wako na usengenyaji wako kisha kesho unaendelea na dhambi hizo , hiyo sio toba ya kweli.
✓✓Usiishie tu leo kutubu kwa ajili ya ulevi wako kisha kesho unaendelea na kunywa pombe, hiyo sio toba ya kweli.
✓✓Usiishie tu leo kutubu kwa ajili ya kuwasema vibaya watumishi wa MUNGU kisha kesho unaendelea na dhambi hiyo , hiyo sio toba ya kweli.
Ndugu katika Maombi Yako leo.
1. Tubu na kuziacha Dhambi.
2. Tubu huku ukiungama dhambi zako mbele za MUNGU katika KRISTO YESU.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi Katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Comments