MAOMBI MAALUMU (Day 24)

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 


Kipengele B: MAOMBI YA KUWACHAFULIA USEMI MAADUI ZAKO.

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu!

Tunaendelea na Maombi yetu ya kufunga, leo ni siku ya 24.

Kila mtu anatambua kabisa kwamba umoja ni nguvu.

Kama umoja ukiondolewa hakika nguvu ya utekelezaji haitaonekana.

Utajisikiaje ikiwa maadui zako katika ulimwengu wa roho hawaelewani na wana uadui wao kwa wao?

Hakika huo ni ushindi kwako.

Unao maadui kwenye ulimwengu wa roho, maadui hao ni falme za giza, mamlaka za kipepo, wakuu wa giza na majeshi yote ya Pepo wabaya, Biblia inathibitisha hilo katika Waefeso 6:12 kwamba '' Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''

Na hawa watendakazi wa shetani hutumia wanadamu.

 Unaweza wakati mwingine ukajikuta una maadui wengi kuliko nywele za kichwa chako.

Inawezekana unapambana na maadui wengi wenye nguvu sana.

Inawezekana kabisa wanaokuchukia ni wengi kuliko nywele zako zote kichwani.

Zaburi 69:4 '' Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.''

Ndugu ngoja nikupe kanuni muhimu sana ya kiroho ambayo mimi Peter  nilifunuliwa, kanuni hiyo ni kwamba njia mojawapo ya kuwashinda maadui zako walio wengi ni pale ambapo wao hawatakuwa na umoja katika mipango yao kukuhusu wewe.

Maadui zako wakikosana hakika huo ni ushindi kwako, maana hawatakuwa pamoja tena katika mipango yao kukuhusu wewe.

 Waisraeli wakati wa Gideoni walikuwa wakati mmoja katika vita mbaya sana dhidi ya maadui zao wenye nguvu.

Biblia inasema maadui hao walikuwa wengi kama nzige.

Wamuzi 7:12 ''Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi.''

Kushinda vita ile ilikuwa ni jambo gumu sana kwao.

Yalikuwa ni mataifa matatu makubwa yenye nguvu wakitaka kupigana na taifa moja dogo ambalo ni Israeli.

Lakini MUNGU ni MUNGU wa ajabu sana kwa wanamtegemea, maana Waisraeli walipoomba kwa MUNGU adui walianza kuuana wao kwa wao na hiyo ndio ikawa mwanzo wa Israeli kushinda vita ile.

Waamuzi 7:22 '' ....... naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.''

 Andiko hilo ukilisoma katika Tafasiri ya BHN Biblia inasema hivi '' ........ Mwenyezi-MUNGU aliwafanya Wamidiani waanze kuuana wao kwa wao kambini. Waliosalia wakatoroka hadi Serera panapoelekea Beth-shita, hadi mpakani mwa Abel-mehola karibu na Tabathi. ''

MUNGU aliwafanya maadui za Israeli kuuana wao kwa wao.

Hata kwako inawezekana kabisa una maadui wengi kazini kwako, kwenye ukoo, kwenye mtaa au sehemu yako ya biashara lakini unaweza kuomba maombi ya kuwachafulia usemi maadui zako na utashangaa maadui hao wanakosana wao kwa wao, utashangaa hata vikao walivyokuwa wanakaa kukujadili vinakufa, utashangaa mmoja katika kundi la watu hao anakupa taarifa wewe juu ya kila mipango mibaya kukuhusu.

Wakikosana maadui zako hakika ni ushindi kwako.

Kuna mbinu nyingi sana za kimaombi za kukusaidia kushinda vita ya kiroho, ufunuo wa leo ni kuomba maombi ya kuwachafulia usemi maadui zako katika ulimwengu wa roho.

 Watu fulani walikuwa na umoja sana wakimpinga Mtumishi wa MUNGU mmoja ambaye ni Mchungaji Mwanamke, vita ile ilikuwa kubwa sana kwa mtumishi yule.

Mama yule aliendelea na maombi tu akimsihi MUNGU amtetee, Ghafla vita ikakoma.

Unajua ilikuwaje?

Mmoja kati ya wale maadui aliota ndoto wenzake wakifanya mipango ya kumdhuru. Akajua kabisa kama alivyoona katika ndoto basi wenzake wanataka kumdhuru. Baada ya ndoto aliwaendea wenzake huku akiwachukia na katika majibizano na wenzake ilipelekea kikundi chao cha uovu kikafa na wakaanzisha vita wao kwa wao. Vita ile ikawa kubwa sana maana kupitia ndoto ile walidhani wanazungukana na kuna mipango ya kuuana wao kwa wao. vita yao kuhusu Mtumishi wa MUNGU ilikoma tangu siku ile, yaani ndio ikawa chanzo cha usemi wao kuchafuka, umoja ukafa na vita ikahamia kwa wao binafsi.

Ndugu unaweza ukawachafulia usemi maadui zako kwa maombi yako katika jina la YESU KRISTO na baada ya maombi ukashangaa huwi tena adui wa maadui zako bali wao kwa wao ndio wamekosana na kuwa maadui, huku wewe ukiwa kama rafiki kwao.

Biblia inasema kwamba ukimtegemea MUNGU kwa maombi na utakatifu na kuliishi Neno lake hakika anaweza akawafanya adui zako kupigwa mbele yako.

Kumb 28:7 '' BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. ''

 MUNGU anaweza kuwafanya adui zako kupigana wao kwa wao na wewe kushinda vita hiyo kirahisi sana.

Mama mmoja ndoa yake iliingia katika mgogoro mkubwa kwa sababu mume wake alitekwa na hawara. Yule hawara anatumia nguvu za giza. Ndoa ile ikawa imekufa maana Baba wa familia alikuwa anakaa kwa hawara hata miezi 8 mfululizo , ameisahau familia yake na hata hajui kama mke na watoto wake wana chakula.

Mama yule kwa maumivu aliendelea kumtegemea MUNGU kwa maombi. aliendelea kumuomba MUNGU ili aiponye ndoa yake, ghafla kukatokea kutokuelewana kati ya yule mwanaume na hawara, ikawa vita kali na hali hiyo ikapelekea Baba yule kurudi kwa mkewe na akatubu dhambi zake maana hawara alitaka kumuua, hapo usemi ulichafuliwa na ndio kupona kwa ndoa kukatokea.

Ndugu, kuna vita ya kiroho unaweza ukashinda kwa maadui zako kukosana wao kwa wao.

Inawezekana kazini kwako unachukiwa sana, lakini unaweza kuomba ya kuwachafulia usemi wanaokuchukia , na ukashangaa wao kwa wao ndio wanakosana na wewe unageuka mtu mzuri mbele ya kila mmoja.

 ✓✓Inawezekana mchumba wako amechukuliwa na watu wanaotumika kipepo, inawezekana mume wako au mke wako kwa sasa ana washauri wabaya kiasi kwamba hamna furaha katika ndoa yenu, leo omba ukiwachafulia usemi ili uhusiano wao unaotaka kuvunja ndoa yako, huo uhusiano uvunjike.

✓✓Inawezekana wewe hukubaliki katika ukoo wa mwenzi wako wa ndoa, inawezekana majirani zako wote wanakaa vikao ili kukupiga vita

✓✓ Inawezekana kikundi cha wachawi au majini wanapanga madhara kwako. Ndugu uko ushindi katika jina la YESU KRISTO kupitia maombi, leo wachafulie usemi ili wasipange jambo lolote baya kukuhusu wewe. Ukiomba hakika MUNGU atakuokoa mbele ya maadui hao.

Zaburi 18:17 ''Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.''

Inawezekana uko katika vita na watu wengi walioungana ili kukuletea madhara, leo wachafulie usemi wao.

MUNGU anaweza kuwafanya maadui zako kupigana wao kwa wao, na hivyo mipango mibaya waliokusudia kuhusu wewe wasiweze kufanya.

Kama huamini soma Biblia yako.

2 Nyakati 20:22-23 '' Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe.''

Maandiko haya hua yananibariki sana maana maadui wanapigana wao kwa wao huku watu wa MUNGU waombaji wakimtukuza MUNGU tu.

Ukisoma sura hii ya 20 ya Nyakati wa pili kuanzia mstari wa kwanza utaona ya kwamba mataifa matatu yaliizingira Israeli ili kuipiga kivita.

Mfalme wa Isareli alipogundua ya kwamba kuwashinda katika vita maadui hao ni ngumu sana aliamua kutangaza maombi ya kufunga.

Biblia inasema '' Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. ..... Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. -2 Nyakati 20:1,3''

Maombi yao ya kufunga yalipata kibali kwa MUNGU , Ndipo MUNGU akawaambia kwamba vita sio yao bali vita ile ni yake(2 Nyakati 20:15) maana kwa maombi yao wamekata rufaa mbinguni hivyo vita sasa sio yao ila ni ya MUNGU asiyeshindwa.

Yaani maombi yale yalimfanya MUNGU ainunue vita ile na kirahisi sana waisraeli walishinda vita ile maana Biblia inasema katika 2 Nyakati 20:23 kwamba mataifa mawili waliokuwa maadui za watu wa MUNGU walianza kupigana na taifa rafiki yao moja ambao wote walikuwa vitani kupigana na watu wa MUNGU.

MUNGU aliwafanya maadui kupigana wao kwa wao.

Ndugu, maombi yako katika utakatifu ndani ya YESU KRISTO yanaweza kumfanya MUNGU akainunua vita yako na wewe kushinda vita.

Hata kama una madui wengi sana, ukiwa na YESU KRISTO hakika utashinda.

 Hata kama unapambana kwa wakati mmoja na majini, wachawi, waganga, falme za giza, mamlaka za kipepo na kila wanadamu wanaotumika kipepo hakika kwa maombi yako katika jina la YESU KRISTO utashinda vita hizo zote.

Madui hao wakichafuliwa usemi hakika watapigana wao kwa wao na hakuna adui ambaye atakuwa na nguvu za kukufuatilia.

Ikumbuke Babeli siku ambayo MUNGU aliwachafulia usemi wanadamu wale.

Mwanzo 11:7 '' Haya, na tushuke huko, TUWACHAFULIE USEMI WAO ILI WASISIKILIZANE MANENO WAO KWA WAO.''

Baada ya MUNGU kuwachafulia usemi waliacha kazi yao maana hawakuwa na usemi mmoja tena.

Inawezekana umoja na ushirikiano wa watu wanaokutakia mabaya ndio unaosababisha wewe uteseke, hebu leo kwa jina la YESU KRISTO wachafunulie usemi wao ili wasielewane. Kama utawachafulia usemi wakati umepata mchumba utashangaa wanakuja kushtuka kukuzuia kuingia kwenye ndoa kipindi ambacho uko tayari katika ndoa, tayari umeshazaa watoto.

 KWANINI UWACHAFULIE USEMI MAADUI ZAKO?

1. Ili wasielewane wao kwa wao, na hivyo mpango mbaya walioupanga kukuhusu wewe hautafanyika.

Amosi 3:3 ''Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? ''

2. Ili kufuta umoja wao wa kipepo na kuwafanya wasiwe na nguvu.

Mwanzo 11:9 "Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA ALIPOICHAFUA LUGHA ya dunia yote; na kutoka huko BWANA AKAWATAWANYA waende usoni pa nchi yote."

3. Ili vifungo vya giza walivyovipanga visikupate wewe bali wapigane wao.

2 Nyakati 20:23 "Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe."

4. Ili wakusahau wewe kama ni adui kwako, wainukiane wao kwa wao.

Waamuzi 7:22 "Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi."

 5. Ili adui wasambaratike na madhabahu zao za  giza wanazoitumikia zisifanye kazi.

Zaburi 124:7-8 " Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi."

6. Ni kanuni mojawapo ya kimaombi ya kuleta ushindi katika vita ya kiroho.

Mwanzo 11:7 "Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao."

7. Ili kumfanya adui yako awe na maadui wengi na hivyo adui huyo kushindwa kutekeleza lolote kwako.

2  Nyakati 20:23 "Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe."

 Nini ufanye leo katika maombi yako?

1. Tubu kwa MUNGU kile kilichosababisha adui zako wakawa na nguvu dhidi yako.

Yeremia 14:20" Ee BWANA, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi."

2. Wachafulie usemi maadui zako huku ukiwataja na huku ukitaja kila eneo wanalotaka kukuharibia.

Mwanzo 11:7 "Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao."

3. Haribu madhabahu ya giza wanayoitumikia.

Kumbu 7:5 "Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga."

4. Watenganishe maadui zako kwenye ulimwengu wa roho ili wasipatane tena.

2 Nyakati 20:23 "Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe."

5. Mshukuru MUNGU Baba wa mbinguni aliyekupa kushinda.

Zaburi 124:6-8 " Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi."
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.
+255714252292
Ubarikiwe sana.

Comments