MAOMBI MAALUMU (Day 27)

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



KipengeleB: KUOMBA KWA MUNGU ILI DAMU YA YESU KRISTO INENE MEMA KWAKO.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Tunaendelea na Maombi yetu ya kufunga , na leo ni siku ya 27 ya Maombi ambapo tunaomba kwa MUNGU ili damu ya YESU KRISTO Mwokozi wetu inene mema kwetu.

Biblia inasema kwamba damu ya YESU KRISTO inanena mema.

Waebrania 12:24 "na YESU mjumbe wa agano jipya, na DAMU ya kunyunyizwa, INENAYO MEMA kuliko ile ya Habili."

✓✓Kunena mema maana yake damu ya YESU KRISTO huongea mema, damu ya YESU KRISTO inatoa sauti ikiongea mema.

Damu ya YESU KRISTO ni kitu cha thamani sana kwa wateule wa MUNGU.

Damu ya YESU KRISTO ni sadaka ya MUNGU ya kipekee sana.

Waebrania 9:28 "kadhalika KRISTO naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu."

 Kwa sababu Biblia inaonyesha juu ya damu ya YESU KRISTO kunena, basi leo unayo nafasi ya kuomba mbele za MUNGU ili damu ya YESU KRISTO ya agano inene mema kwako.

Inawezekana huwa unasikia tu watu wakisema kwamba damu ya YESU inanena mema ila hujui itanenaje mema kwako.

Katika maombi yako leo ita damu ya YESU KRISTO na omba kwa MUNGU inene mema juu yako. Juu ya ndoa yako, juu ya afya yako, juu ya ndoa yako, juu ya kibali chako, juu ya uzao wako na kila baraka zako.

Walawi 17:11" Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi."

Kwanini unahitaji damu ya YESU KRISTO inene mema?

Kwa Sababu damu yeyote ya chochote inaweza kunena mabaya, lakini ni damu ya YESU KRISTO pekee ndio hunena mema, hivyo itumie kufuta kila sauti ya damu inayonena mabaya kwako.

✓✓Inawezekana kuna mtu alikuendea kwa waganga au kwa wachawi na huko alitoa sadaka/kafara ya damu ya mnyama au ndege na hiyo damu ilielekezwa ikunenee mabaya, hivyo kila Siku damu/sadaka hiyo ya kafara ya kipepo huwa inasema kuhusu wewe kwamba "afe" au "afilisike" au "aachike" au " aachwe" au "asizae" au "akimbiwe" au "asalitiwe" au "asipate kazi" au "asifanikiwe" n.k.

Damu hiyo au sadaka/kafara hiyo ya wanyama au ndege inaponena kuhusu wewe ujue majini ambao ndio watendakazi wa kipepo watahakikisha inakuwa kama linavyosema hilo agano la kichawi lilipofanyika.

✓✓Na kumbuka kwamba damu huwa haifi, damu hata kama iko ardhini bado itabaki hai kwenye ulimwengu wa roho.

✓✓Kwa sababu damu hiyo ya kafara iko hai na inaendelea kunena mabaya kuhusu wewe kama ilivyoelekezwa na mganga au mchawi au mizimu ujue mambo mengi mazuri yako yanaweza kuharibika hata hujui vita inatoka wapi, kumbe kuna kafara ya damu au kuna kafara ya pesa inanena mabaya kuhusu wewe hivyo sauti hiyo ya kafara huziamsha roho za kishetani kutekeleza kifungo cha kipepo kwako.

✓✓Ndugu, ndio maana sio wateule wa MUNGU  tumepewa damu ya YESU KRISTO kama sadaka ya milele inayoweza kuitowesha kila mipango ya kuzimu kuhusu wewe.

Bwana YESU mwenyewe aliizungumzia damu yake akisema "Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.-Marko 14:24 "

Katika maombi yako leo hakikisha unaita damu ya YESU KRISTO kufuta kafara za damu na kisha ita damu ya YESU KRISTO ili inene mema kwako, kwa familia yako, kwenye biashara yako, kwenye nyumba yako n.k

Damu ya YESU KRISTO ina kazi nyingi sana, kazi mojawapo ya damu ya YESU KRISTO inaweza kunena mema kama ukiomba kwa MUNGU kwamba inene mema.

Zamani za torati walitumia damu za wanyama katika kusafisha jambo kiroho, kwa sasa tunatumia damu ya YESU KRISTO ya agano.

Waebrania 9:13-14"Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake KRISTO, ambaye kwamba kwa ROHO wa milele alijitoa nafsi yake kwa MUNGU kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu MUNGU aliye hai?"

 Kwa ujumla damu ya YESU KRISTO ina kazi nyingi sana, baadhi ya kazi hizo ni hizi:

1. Damu ya YESU KRISTO hutakasa, yaani kumfanya mtu kuwa safi.

Waebrania 13:12 "Kwa ajili hii YESU naye, ili AWATAKASE WATU KWA DAMU YAKE MWENYEWE, aliteswa nje ya lango."

2. Damu ya YESU KRISTO hutupatanisha na MUNGU.

Warumi 3:25 "ambaye MUNGU amekwisha kumweka AWE UPATANISHO KWA NJIA YA IMANI KATIKA DAMU YAKE,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa."

Tunapompokea YESU KRISTO kama Mwokozi na kutubu, tunakuwa tumeiruhusu damu ya YESU KRISTO kutupatanisha na MUNGU.

Wakolosai 1:20 "na kwa yeye KUVIPATANISHA VITU VYOTE na nafsi yake akiisha kufanya amani KWA DAMU YA MSALABA WAKE; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni."

3. Damu ya YESU KRISTO hutushindia dhidi ya shetani.

Ufunuo 12:11" Nao WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO, NA KWA NENO la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."

 4. Damu ya YESU KRISTO huondoa dhambi.

Mathayo 26:28 "kwa maana HII NDIO DAMU yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi KWA ONDOLEO LA DHAMBI."

5. Damu ya YESU KRISTO hutununua na kutufanya kuwa Mali ya MUNGU.

Ufunuo 5:9 "Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, UKAMNUNULIA MUNGU KWA DAMU YAKO WATU WA KILA KABILA na LUGHA na JAMAA na TAIFA,"

Kama umefanyika kanisa hai la MUNGU la Wokovu wa KRISTO na unaishi maisha matakatifu basi wewe umenunuliwa kwa damu ya YESU KRISTO ya agano jipya.

Kama wewe ni mtumishi basi mtumikie MUNGU katika nguvu ya damu ya YESU KRISTO maana damu ya YESU KRISTO ndio imelinunua Kanisa hai la waenda mbinguni.

Matendo 20:28 "Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha KANISA lake MUNGU, ALILOLINUNUA KWA DAMU YAKE MWENYEWE."

 6. Damu ya YESU KRISTO hutuhesabia haki.

Warumi 5:9 "Basi zaidi sana TUKIISHA KUHESABIWA HAKI KATIKA DAMU YAKE, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye."

7. Damu ya YESU KRISTO hutufanya kuwa karibu na MUNGU.

Waefeso 2:13 "Lakini sasa, katika KRISTO YESU, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza MMEKUWA KARIBU KWA DAMU yake KRISTO."

8. Damu ya YESU KRISTO hutufanya tupaingie patakatifu mbinguni.

Waebrania 10:19 "Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa KUPAINGIA PATAKATIFU KWA DAMU ya YESU,"

Hizo ni baadhi tu ya kazi za damu ya YESU KRISTO.

Damu ya YESU KRISTO ni ya muhimu sana kwa kila mteule wa MUNGU.

Damu pia ya YESU KRISTO hutusafisha tuwe safi ili tumwabudu MUNGU.

Ufunuo 7:14 "Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao WAMEFUA MAVAZI YAO, NA KUYAFANYA MEUPE KATIKA DAMU YA MWANA-KONDOO."

Naamini kila Mteule wa MUNGU anayesoma somo hili ameona umuhimu damu ya YESU KRISTO.

Ndugu kwa maombi yako tumia damu ya YESU KRISTO.

 Nini ufanye katika maombi yako leo?

1. Tubu kwa MUNGU ndipo utaruhusu damu ya YESU KRISTO kufanya kazi kwako.

1 Yohana 1:7-9 " bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote."

Hata kama unataka damu ya YESU inene mema katika ndoa yako, tubu kwa ajili ya chanzo cha matatizo ya ndoa yako.

Kama ni ardhi au eneo lako la biashara, tubu kwa ajili ya ardhi na tubu kwa ajili ya vyanzo vya matatizo.

Toba itaruhusu kibali cha damu ya YESU KRISTO kufanya kazi hapo.

Damu ya YESU KRISTO ipo hai na inakusubiri tu wewe uombe.

Ufunuo 1:5 "tena zitokazo kwa YESU KRISTO, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. YEYE ATUPENDAYE NA KUTUOSHA DHAMBI ZETU KATIKA DAMU YAKE,"

 2. Nyunyiza damu ya YESU KRISTO palipofungwa kipepo au palipoharibiwa na nguvu za giza, au penye tatizo ili tatizo liondoke.

1 Petro 1:2" kama vile MUNGU Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na ROHO, hata mkapata kutii na KUNUNYIZIWA DAMU ya YESU KRISTO. Neema na amani na ziongezwe kwenu."

3. Omba kwa MUNGU kwamba  damu ya YESU KRISTO inene mema katika maeneo yako( yataje maeneo hayo,. Mfano, ndoa,kazini, nyumba,mwili, familia, kiwanja n.k) na yataje maeneo hayo unayotaka damu ya YESU KRISTO inene.

Waebrania 12:24 "na YESU mjumbe wa agano jipya, na DAMU YA KUNYUNYIZWA, INENAYO MEMA kuliko ile ya Habili."

4. Futa kwa damu ya YESU KRISTO kila kafara ya damu au kafara/sadaka iliyofanyika kukufunga popote au kufunga familia, uchumba,ndoa, mwili wako,afya yako,kibali chako,uchumi wako n.k

Ufunuo 12:11" Nao WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na hadi whatsapp).
Ubarikiwe 

Comments