![]() |
| Peter na Jemimah Mabula Watenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Kipengele: MAOMBI YA KUIFUNGUA MILANGO YAKO YA BARAKA ILIYOKUWA IMEFUNGWA.
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
◼️Kuna milango ya kiroho ambayo ndio hupitisha ushindi kwa watu wa MUNGU.
✓✓Kila baraka kwenye ulimwengu wa roho ina mlango wa kupitia ili ije kwako.
Mathayo 7:7 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;"
andiko hili katika tafasiri ya BHN inasema Biblia inasema
“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa."
✓✓Kumbe kuna kugonga mlango ili ufunguliwe, huwezi kugonga mlango ulio wazi, unagonga mlango uliofungwa, sasa kwenye ulimwengu wa roho kila baraka ina mlango wake usipofunguliwa mlango huo huwezi kuipata baraka hiyo.
✓✓Kuna ushindi wako unahitaji kupita katika mlango kwenye ulimwengu wa roho ili uje kwako.
Kazi ya mawakala wa shetani ni kuifunga milango ya baraka ili baraka fulani zisije kwako.
Kuna watu wanaumwa na milango ya kupona imefungwa na wachawi ndio maana wanaenda hospital na bado hawaponi.
Kuna watu milango ya kupata kazi imefungwa na nguvu za giza, ndio maana wametafuta kazi kwa miaka mingi bila mafanikio.
Kuna watu milango ya mafanikio imefungwa kichawi, ndio maana japo Wana juhudi kubwa sana katika kazi lakini hakuna mafanikio.
Kuna watu milango ya uchumi imefungwa,ndio maana japokuwa sio wazembe lakini mafanikio hakuna.
Hii ni mifano michache tu kati ya mingi.
✓✓Inawezekana na wewe kuna jambo unang'ang'ana nalo bila mafanikio, wakati mwingine fungua kimaombi mlango wa baraka hiyo ndipo utafanikiwa.
Kuna watu milango ya kibali imefungwa, japokuwa hawana kasoro yeyote lakini hakuna wanakokubalika, iwe kazini, kwenye ndoa, kwenye familia, kwenye ukoo,kwenye ofisi, kwenye jamii,kwenye kundi, kwenye Kanisa, kwenye uchumba n.k
Ndugu katika Jina la YESU KRISTO Kuna ushindi mkuu, omba leo Maombi ya kuifungua milango Yako ya baraka na utapata ushindi unaouhitaji.
Kuna watu milango ya ndoa imefungwa na nguvu za giza, ndio maana hawafungi ndoa au wanaachwa kipepo n.k
Kuna watu pia milango ya ndoa kwao haijafungwa ila imefungwa milango ya furaha katika ndoa, amani na upendo wa kweli n.k
Kuna watu milango ya kuzaa imefungwa ndio maana hawajapata mtoto.
Inawezekana hujaelewa vyema ngoja nikupe mfano hai.
Mwanzo 30:22 " MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, AKAMFUNGUA TUMBO. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu."
Biblia inasema kwamba Raheli/Rachel alikuwa amefungwa tumbo, haijulikani ni nani alimfunga tumbo lakini labda ni familia yao mabinti walikuwa wamefungwa matumbo ya uzao maana
Mwanzo 29:31 inasema " BWANA akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai."
Yaani Lea akapata neema ya tumbo lake la uzao kufunguliwa mapema na MUNGU na tena Biblia inasema kwamba Raheli alikuwa hazai, inaonekana hawa wote walikuwa wamefungwa ila Lea akapata neema ya kufunguliwa tumbo mapema.
Sasa kuna tumbo la chakula na tumbo la uzazi, tumbo la uzazi lilikuwa limefungwa yaani mlango wa tumbo la uzazi ulikuwa umefungwa yaani yai la mwanamke haliwezi kukutana na mbegu za mwanaume hata mimba ikatungwa, wapo watu wamefungwa matumbo yao ya uzao ndio maana maombi ya leo tunafungua milango yetu iliyofungwa na nguvu za giza ili tufanikiwe.
◼️Bwana YESU anaweza kumfungua kila mtu, Biblia inasema Leah alifunguliwa akazaa na tena Raheli alifunguliwa akazaa, leo kila mlango wako uliofungwa na nguvu za giza ufungue kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Hadi Mimi Peter Mabula nakuletea Wewe rafiki yangu ujumbe huu nilipewa andiko la ufunuo 3:8 inayosema "Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu."
Maana yake Bwana YESU KRISTO atakufungulia mlango ambao hakuna anayeweza kuufunga.
Kila baraka inahitaji kupita mlangoni, hivyo fungua mlango wako kwenye ulimwengu wa roho na utapokea kirahisi sana baraka ya ki MUNGU uliyoisubiri kwa muda mrefu.
Maana yake nini?
MUNGU kwa maombi yako anaweza hata kukutengenezea mlango mpya na kuufungua ili ufanikiwe, hata kama kuna mahali maadui walifunga
Leo ni siku yako njema ya kuomba na kupokea.
Bwana YESU KRISTO Mwokozi akufungulie Mlango wako uliokuwa umefungwa na sasa MUNGU akubariki.
Jambo moja la mwisho kabla sijamaliza katika ujumbe wa leo ni kwamba liko lango moja tu la mbinguni na liko wazi sasa ili wewe uingie na kupata uzima wa milele, lango hilo ni wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuanza kuishi matakatifu ya Wokovu. Changamka ndugu kuingia kupitia lango hili maana limefunguliwa sasa kwa ajili yako, kumbuka lango hilo likifungwa halitafunguliwa tena, hivyo fanya hima sasa uingie kabla lango hilo halijafungwa.
MUNGU akubariki.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU wa Mbinguni.
+255714252292
Ubarikiwe sana

Comments