MAOMBI MAALUMU (Day 6)

 

Na Mwl Peter Marco Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 


Kipengele: MAOMBI YA ULINZI.
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Katika maombi ya leo ngoja tuangalie namna Ayubu alivyolindwa na MUNGU hadi shetani akalalamika maana alishindwa kumtesa Ayubu katika jambo hata moja hadi wakati huo.

Biblia inasema
Ayubu 1:10 "Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi."

Kumbe ili shetani na mawakala zake wakashindwa kumdhuru Ayubu na familia yake ni kwa sababu hizi.

1. MUNGU alimzingira ki ulinzi Ayubu pande zote.

2. MUNGU alizingira ki ulinzi familia yote ya Ayubu.

3. MUNGU alivizingira ki ulinzi vitu Vyote alivyokuwa navyo Ayubu.

4. MUNGU alibariki kazi za mikono ya Ayubu.

✓✓Mambo hayo manne(4) MUNGU akiyafanya kwako utakaa salama siku zote za maisha yako haijalishi una maadui wengi kiasi gani.

Omba MUNGU akulinde wewe na familia yako, akikulinda wewe huku familia yako imevamiwa na nguvu za giza ujue na wewe hauko salama.

Omba MUNGU akulinde wewe na Mali zako, akikulinda wewe huku Mali zako zimevamiwa na nguvu za giza ujue hauko salama.

Omba MUNGU akulinde na kubariki kazi za mikono yako, hiyo ni muhimu sana.

◼️Maana yake Ayubu alilindwa katika afya, uchumi , uzao wake, kutamalaki na alilindwa katika ndoa yake, hizo ndizo baraka tano tu atoazo MUNGU kwa watu wake. Yaani baraka za Uzao, baraka za ndoa, baraka za uchumi, baraka za kiafya na baraka za kumiliki na kutawala.

Katika Ayubu hiyo sura ya kwanza kuna sehemu shetani analalamika mbele za MUNGU kwa sababu MUNGU amemlinda Ayubu kiasi ambacho shetani amemshindwa Ayubu.

Lakini ili Ayubu alindwe kiwango kikubwa namna hiyo Ayubu alikuwa na sifa zifuatazo:

1. Alikuwa mkamilifu(Ayubu 1:1).

2. Alikuwa mwelekevu(Ayubu 1:1).

3. Alikuwa Mcha MUNGU(Ayubu 1:1).

4. Aliishi maisha ya kuepukana na uovu(Ayubu 1:1).


Ayubu 1:1 "Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha MUNGU, na kuepukana na uovu."


5. Alikuwa anazingatia kutoa sadaka(Ayubu 1:5)

6. Alikuwa Muombaji(Ayubu 1:5)

Ayubu 1:5 "Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru MUNGU mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote."


◼️Kwa hiyo ukitaka kulindwa na MUNGU katika KRISTO YESU zingatia sana hayo mambo 6 yaliyokuwapo pia kwa Ayubu, uwe nayo maana ni kanuni za kiroho za kukubaliwa na MUNGU.

 Na ukikubaliwa na MUNGU utalindwa sana kama ilivyokuwa kwa Ayubu.

Japokuwa Ayubu baadae aliingia katika jaribu lililoruhusiwa na MUNGU lakini kwa sababu maalum tu na sio kwamba na wewe utajaribiwa kama Ayubu.

Wewe fuata Kanuni zilozopelekea Ayubu kulindwa na MUNGU hadi shetani analalamika.

Zingatia kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO YESU na leo omba maombi haya.

1. Omba MUNGU akulinde pande zote.


Zaburi 121:7" BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako."


2. Omba MUNGU alinde familia yako yote.


2 Wathesalonike 3:3 "Lakini BWANA ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu."

3. Omba MUNGU alinde vitu vyako vyote na Mali zako zote.

Luka 11:10 "Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."


4. MUNGU abariki kazi za mikono yako.
Kumbu 1:11" BWANA, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi."
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292
Ubarikiwe 

Comments