MAOMBI MAALUMU (Day 7)

 

Peter na Jemimah Mabula 
Watendakazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 


Kipengele: MAOMBI YA KUMWITA ILI ATUSHINDIE.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe Ndugu yangu.
Kuna maandiko mengi yanayozungumzia kumwita MUNGU au kumwita YESU KRISTO ili tusaidike ila leo ngoja tuangalie maandiko machache ili yatupe msingi wa nini tuombe katika kumwita MUNGU wetu Siku hii ya leo ambayo ni Siku ya saba ya maombi yetu ya kufunga.

Lakini kabla ya yote inabidi angalau kwa uchache tuone ni sifa ipi itatufanya wateule wa KRISTO tumwite MUNGU na atusaidie.

Isaya 58:9  ina majibu ya swali hilo Biblia inasema  "Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;"

Ukilisoma andiko hilo katika tafasiri ya BHN unagundua kwamba ili umwite MUNGU na akuitikie fanya haya;
1. Acha dhuluma.
2. Acha dharau.
3. Acha uovu.

✓✓Kwa namna hiyo sifa unazotakiwa kuwa nazo hata umwite MUNGU na akuitikie ni hizo 3 kulingana na andiko moja tu la Isaya 58:9, lakini usisahau ni lazima uwe umeokoka yaaani umefanyika mtoto wa MUNGU yaani umempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Yohana 1:12-13 inasema " Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;  waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

Zingatia hilo na usije ukasahau hata siku Moja.

Aina ya maombi ya leo ni kumwita MUNGU ni haya.

1. Mwite MUNGU ili akuokoe na akutoe katika mateso.

Zaburi 50:15 "Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza."

Ni MUNGU mwenyewe amekuruhusu wewe Mteule wa KRISTO ili umwite Siku ya mateso, siku unateseka na ni yeye MUNGU atakuokoa na kukuondolea mateso hayo.

Je wewe uko katika mateso gani?

Je ndoa yako iko katika mateso gani?

Je biashara yako au kazi yako unapata mateso gani?

Je familia yako inapata mateso gani?

Je unaumwa? Je unaonewa na watu wenye nguvu?. Je unanyanyaswa na nguvu za giza?

◼️MUNGU anasema mwite atakuitikia na kukuokoa kutoka katika mateso hayo.

Ona mfano huu wa Samsoni aliyekuwa anateswa na wafilisi na walikuwa wamemtoboa macho, Samsoni akamwita MUNGU, Waamuzi 16:28 "Samsoni akamwita BWANA, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee MUNGU, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili."

Baada ya Samsoni Kumwita MUNGU kilichofanyika ni wafilisti wengi mno wakiwemo waliomtesa wote wakajikuta wamekusanyika ndani ya jengo moja huku na Samsoni akiwa hapo na wakafa wote.
Waamuzi 16:30 "Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake."

Kosa la Samsoni ni kwamba alimwita MUNGU akimuomba kwamba hata yeye afe pia na akafa nao, wewe usimwite MUNGU akuue ila mwite MUNGU awaue maroho wote wa kuzimu wanaokutesa.

Lakini Biblia inasema wale maadui wa Samson waliokufa siku hiyo moja ni wengi kuliko wote waliowahi kufa katika maisha ya Samson ya kabla.

Kumwita MUNGU kulisababisha wafilisti wengi kukusanyika ili wafe.

Mwite MUNGU ili akutoe katika mateso uliyopo.
Mwite MUNGU hata awatoweshe wakuu wa giza waliokutesa.

2. Mwite MUNGU ili akufunulie yaliyojificha ambayo inakupasa uyajue.

✓✓Kwanza ni muhimu kujua kwamba sio kila kitu lazima ukijue ila omba MUNGU akupe kujua yanayokustahili wewe kujua.

Yeremia 33:3" Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua."

andiko hilo ukilisoma katika tafasiri ya BHN Biblia inasema
“Niite, nami nitakujibu na kukuambia mambo makubwa yaliyofichika ambayo hujapata kuyajua."

Kuna mambo mengi yamejificha na ni haki yako kuyajua, Mwite MUNGU ili akuitikie na kukujibu na kukujulisha hayo hayo yaliyojificha.

✓✓Wakati mwingine unatakuwa kuwajua adui zako ili upate kuwashinda, usipofunuliwa huwezi kuwajua.

Mfano kuna Mama fulani alikuwa anarogwa na rafiki yake. Rafiki huyo ni mpole, mkarimu, anayejali na ni mtu wa tabasamu muda wote, ilikuwa ngumu sana kumjua kama japokuwa alimtesa sana mama huyu kwa kumroga na hata kuua watoto wake.

◼️Kuna mambo mengi unahitaji kuyajua wewe kama Mteule wa KRISTO na hayo ni MUNGU tu katika ROHO MTAKATIFU anaweza kukujulisha ukimwita.

✓✓Unahitaji kufunuliwa juu ya mwenzi wako kama hujaingia kwenye ndoa.

✓✓Unahitaji kufunuliwa juu ya yaliyojificha katika kazi yako.

✓✓Unahitaji kufunuliwa juu ya adui zako.

✓✓Unahitaji kufunuliwa juu ya wanaokuwinda.

✓✓Unahitaji kufunuliwa juu ya jinsi ya kupata baraka yako.

✓✓Unahitaji kufunuliwa ni Mtumishi nani anaweza kukusaidia ili ushinde.

◼️Mambo ya ulimwengu wa roho ni siri hivyo omba MUNGU akufunulie ndipo utakuwa na uhakika au ndipo  utashinda.

Mimi binafsi kama Peter Mabula najua utumishi wangu kwa KRISTO unanihitaji nifanye nini mwaka huu, je nilijuaje?
Nilifunuliwa na MUNGU.
MUNGU anaweza akakufunulia kwa maono, ndoto, macho ya rohoni, masikio ya rohoni, kwa Neno la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU, kwa kutumia watumishi wengine, kwa kusoma Biblia, kwa mazingira, kwa njia ya Malaika na kwa sauti ya moja kwa moja.

Ngoja nikupe mfano mmoja hai.
Biblia inasema kwamba Hajiri na Ishmaeli walikuwa jangwani wakitembea kwenda Misri, maji yaliisha na jangwani hakuna maji, ikafika kipindi wakajua wanakufa, ila Biblia inaonyesha kwamba Ishmaeli alimwita MUNGU maana MUNGU aliisikia sauti ya Ishmaeli na kumtuma Malaika.
Mwanzo 21:17 "MUNGU akasikia sauti ya kijana. Malaika wa MUNGU akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana MUNGU amesikia sauti ya kijana huko aliko."

Baada ya MUNGU kuitwa akaitika na kumfumbua macho Hajiri akakiona kisima jangwani na kupata maji ya kunywa hata hawakufa yeye na mtoto wake.
Mwanzo 21:19 "MUNGU akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana."

Huyu alifumbuliwa macho akakiona kisima, wewe unaweza kufumbuliwa macho ya rohoni ukaziona baraka zako ziliko, ushindi wako uliko, Mume/Mke wako aliko n.k.

Katika Maombi Leo.

1. Kwa leo mwite MUNGU akutoe katika mateso na omba MUNGU akufunulie ya sirini unayopaswa kuyajua.

2. Mwite Bwana YESU KRISTO Mwokozi akuokoe.

3. Mwite ROHO MATAKATIFU akufunulie ya sirini yote yanayokustahili wewe kujua.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU wa Mbinguni.
+255714252292
Ubarikiwe.

Comments