MAOMBI MAALUMU (Day 8)

 

Na Mwl Peter Marco Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 



Kipengele; MAOMBI KUFUTA MIPANGO YA WADANGANYIFU DHIDI YAKO.



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.

✓✓Kuna watu wanaitwa wadanganyifu, hawa ni watu hatari sana.


✓✓Kuna watu maisha yao yameharibiwa na wadanganyifu.


Biblia inasema kwamba MUNGU anaweza kutangua yaani kufuta mipango ya wadanganyifu, kazi yako ni kuomba ili mipango ya wadanganyifu kwako ifutike.


Ayubu 5:12 " Yeye(MUNGU) huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao."


Nini maana ya wadanganyifu?


1. Wadanganyifu ni watu wanaofanya mambo ambayo ni ya uongo.


Mipango yako mizuri inaweza kufutika kwa sababu ya mtu mdanganyifu.

Mfano kuna Dada mmoja alikubaliana na kaka mmoja kwamba wataoana.

 Wakiwa wachumba huyu kaka akapata nafasi ya kwenda Ulaya kusoma na kufanya kazi, waliendelea kuwasiliana kwa simu kama wachumba kumbe yule kaka huko Ulaya alifika na baada ya muda mfupi akaoa. 

Dada wa watu huku Tanzania aliwakataa vijana safi kwa sababu anamsubiri Mchumba wake kumbe yule mchumba ni mdanganyifu. Baada ya miaka michache yule kaka alirudi Tanzania akiwa na mke na mtoto, huo ulikuwa udanganyifu wa hali ya juu sana. 

Dada huyu alipotezewa muda kwa sababu ya udanganyifu na ilimchukua miaka mingine zaidi ya 5 kupata Mchumba, udanganyifu ni mbaya sana.


✓✓Wako watu leo wanawasubiria wachumba wadanganyifu, wanapotezewa muda na ndoa hakuna.


✓✓Wako watu waliahidiwa kazi na bosi mdanganyifu, wamekataa kazi zingine na kumbe na kazi nzuri wanayosubiria haipo.


◼️Leo kwa Maombi katika Jina la YESU KRISTO futa mipango ya udanganyifu wote kuhusu wewe, ukiifuta hiyo kimaombi MUNGU atakupa jambo sahihi lisilo na udanganyifu.


Futa mipango yote ya udanganyifu uliyofanyiwa, mngoje MUNGU.

Zaburi 40:1-4 " Nalimngoja BWANA kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake MUNGU wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini BWANA. Heri aliyemfanya BWANA kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo."


2. Wadanganyifu ni watu wanaosema au wanaotenda jambo ambalo sio la kweli kwa ajili ya kuwafanya watu wafikiri ni kweli.



Mfano kuna watu hawasalimiani kwa Sababu ya udanganyifu.


Kuna watu wamefukuzwa kazi kwa sababu ya udanganyifu.


Kuna watu wameachwa kwa sababu ya udanganyifu.


Wewe umefanyiwa udanganyifu na nani? na umefanyiwa udanganyifu gani?

Leo kwa damu ya YESU KRISTO  katika jina la YESU KRISTO ifute mipango ya udanganyifu wowote unaopangwa na wabaya wako ili wewe uharibikiwe.


Omba leo na utapata mpenyo mpya wa ushindi.


Zaburi 6:8-8 "Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa BWANA ameisikia sauti ya kilio changu.

BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu. Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika."



3. Wadanganyifu ni watu wanaotoa  ahadi kwa hila.


Kumbuka kusudi lolote la udanganyifu kwako  ni ili uharibikiwe, baraka zako zichelewe, ukate tamaa, ujione mjinga na hufai, ushushwe chini n.k


Kwa sababu ya udanganyifu kuna baraka mtu alitakiwa aipate baraka hiyo mwaka huu lakini kwa sababu ya udanganyifu baraka hiyo ataipata miaka 8 ijayo, udanganyifu ni mbaya sana.


Wadanganyifu ni watu wanaotoa ahadi kwa hila.


Familia moja wazazi walifariki, katika vikao vya ndugu mjomba alionyesha kuguswa na watoto wa marehemu akasema atawalea kama watoto wake na kuwasomesha, ndugu wakampa Mali za marehemu maana ni yeye atakaa na watoto wa marehemu. Kilichofuata aliwatesa wale watoto na kujitajirisha, watoto wale hakuna hata aliyesoma hata darasa la kwanza, waliishi kwa mjomba wao wakiteswa kama wanyama. 

Mmoja alipokua kidogo akatoroka na kwenda mjini kutafuta maisha, mjomba alifanya udanganyifu mkubwa na uliotesa maisha ya watoto hao kwa muda mrefu, udanganyifu ni mbaya sana.


Leo kwa Maombi futa kila udanganyifu uliofanyiwa au unaopangwa kufanyiwa mwaka huu.


4. Wadanganyifu ni watu wanaotoa ahadi ili kupumbaza watu kwa lengo la kutimiza hila zao.


Kanisa fulani walikuwa waombaji sana wakitaka MUNGU awabariki jengo kubwa la ibada na vyombo, mtu mmoja akatokea na kuahidi kununua vyote na kujenga jengo la Kanisa.

Kanisa walifurahi na kungoja ahadi miaka mingi bila mafanikio, wakimuuliza yule ndugu anawaambia wasubiri maana jambo hilo ni dogo sana kwake. Kanisa waliacha maombi na hata mikesha iliisha maana walijua wameshafanikiwa. 

Ndugu, Mimi Peter Mabula Naamini Wewe rafiki yangu unayesoma somo langu hili Sasa unaanza kujua madhara ya udanganyifu, maana unadanganyifu unaweza kukufanya hata utoke katika kusudi la MUNGU, uache Maombi na ubaki ulipo na kumbe sio kusudi la MUNGU.


Baada ya miaka yule ndugu akazidi sana kuwa tajiri lakini hakutimiza ahadi.

Kuna watu wenye michango midogo ya ujenzi walitaka kuchangia ujenzi wakaambiwa suala la ujenzi limeshamalizika maana tajiri yupo hivyo wakatumia pesa zao.

Kanisa likapumbazika na kutokupanga mipango ya Kanisa wakijua wameshafanikiwa, baadae yule aliyeahidi akasema ameghairi hivyo hatatimiza ahadi yake, hayo ndio madhara ya udanganyifu, yaani mngekusanya michango kidogokidogo baada ya mwaka mngejenga lakini kwa sababu ya udanganyifu wa mtu mmoja jambo ambalo lingetimia baada ya mwaka mnajikuta mnalikamilisha baada ya miaka 7, udanganyifu ni mbaya sana, ndio maana Biblia inasema Yeremia 17:5-6 " BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu."


✓✓Je unasubiri wazungu wakutimizie mahitaji yako, kama hao unaowasubiri ni wadanganyifu ujue utapata hasara.


Je unasubiri nini? Kama hicho kina udanganyifu ujue utapata hasara.

Inawezekana kuna mambo yako mengi yamekwama kwa sababu unamgoja mtu fulani, kumbe mtu hiyo ni mdanganyifu, ni hatari sana.



5. Wadanganyifu ni wote wanaopanga mabaya kuhusu wewe.


Hawa wadanganyifu ni wachawi, waganga wa kienyeji, majini, mizimu, wasoma nyota, wakuu wa giza na kila nguvu za giza, hao wasambaratishe kwa Jina la YESU KRISTO, futa mipango yao yote kuhusu wewe.


Leo hakikisha wanafedheheka na kuabishwa na kutoweshwa.


Zaburi 71:13 "Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya."


Nini uombe leo.


1. Omba MUNGU akupe kuwabaini wadanganyifu ili uwapuuze na ili wasikuzuie kufanikiwa kwa wakati.


2. Haribu mipango yao mibaya kuhusu wewe ili isifanikiwe.


3. Mwambie MUNGU atangue mipango yao kuhusu wewe.


4. Amuru mapigo kwa wadanganyifu wanaotokea kuzimu.


Zaburi 35:6-8 "Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake."


5. Omba ROHO MTAKATIFU akupe akili na maarifa ya kuwabaini.


MUNGU akubariki sana.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.

+255714252292

Ubarikiwe sana

Comments