SABABU 5 ZINAZOWEZA KUMFANYA MWANAMKE KUOLEWA.

 


Peter Mabula na Mke wake Jemimah Mabula mwaka 2016



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Siku moja wakati ibada ya  jumapili inaisha  nilijulishwa ghafla na Mchungaji Kiongozi kufundisha wanawake ambao hawajaolewa ili waolewe. Ilikuwa ni Kanisani jumapili ambapo ibada ilipoisha Mchungaji alitangaza kwamba dakika kumi zinazofuata kutakuwa na semina kimakundi kwa dakika 40 hivyo Mimi nikatajwa kufundisha wanawake ambao hawajaolewa. 

Dakika kumi hizo watu waliambiwa kupumzika ili zikiisha kipindi cha semina kwa dakika 40 kitaanza.

 Binafsi kama Peter Mabula sikuwa nimejiandaa na hilo hivyo ilikuwa wakati mgumu kwangu maana Mchungaji  alitangaza kwamba mimi nitafundisha wanawake ambao hawajaolewa na nilikuwa na dakika 10 za kujiandaa, niliingia ofisini kwa Mchungaji nikiwa na Biblia yangu na Daftari yangu ya masomo ambayo huwa naandaa, nilimuomba MUNGU kisha nikapata ufunuo huu wa leo.

Nilianza na kutafakari jinsi mimi nilivyomuoa Mke wangu Jemimah, niliwaza ilikuwaje hadi ni Jemimah ndio akawa mke wangu na sio mwanamke mwingine yeyote?
Majibu yangu moyoni hayakujibu vyema juu ya nini niwafundishe wanawake ambao hawajaolewa. Lakini namshukuru MUNGU sana maana nilipata ufunuo huu kwamba nizungumzie baadhi ya sifa zilizopelekea baadhi ya wanawake kuolewa yaani kufunga ndoa takatifu.
Waefeso 5:31 '' Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.''

✓✓Kitu kimojawapo kikubwa sana na kimechelewesha baadhi ya wanawake kuolewa ni kuruhusu dhambi ya uasherati.

1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.''
 
✓✓Ndugu kama ni wewe unahusika na uasherati acha mara moja leo, tubu na anza kumcha MUNGU katika KRISTO YESU.

Lakini pia kabla sijataja sababu hizo 5 zinayoweza kupelekea Mwanamke kuolewa ngoja nikuambie ukweli huu.

✓✓Ni kwamba Sio kila mwanamke ambaye hayuko katika ndoa amefeli katika sababu za kiroho zinazoweza kumfanya Mwanamke kuolewa, ila baadhi na ni  wengi sana wamefeli kwa sababu hizi ninazozifundisha leo.

✓✓Na pia Sio kila aliyeolewa amefaulu katika sababu za kiroho zinazoweza kumfanya Mwanamke kuolewa, wengine wameolewa katika mpango wa shetani wala sio  MUNGU kwa sababu tu watu hao ndoa zao zilitengenezwa na dhambi ya uasherati.

✓✓ Wengine mimba ndizo ziliwafanya waolewe.
Waefeso 5:3 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; ''

Kama unahitaji kupata mwenzi wa ndoa katika mpango wa MUNGU tambua kwamba mpango wa MUNGU unahitaji utakatifu tangu mwanzo hadi mwisho.
Mimi Peter Mabula najua kuna mtu hapa anasoma ujumbe huu na anahitaji sana kumpata mwenzi wa ndoa, ndugu katika mambo 5 hapo chini tafuta mambo ya kuombea na panapohitaji ubadilike tabia badilika haraka ili ikusaidie kufanikiwa kuolewa.

SABABU 5 ZINAZOWEZA KUMFANYA MWANAMKE KUOLEWA.

1. Wakati wake wa kuolewa kwa mujibu wa mbingu umefika.

Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. ''

◼️Biblia iko wazi sana kwamba kwa kila jambo kuna majira yake kiroho, sasa kuna wanawake wakati wao kuolewa kwa mujibu wa mbingu ulipofika na wao wakakubali kuolewa basi waliolewa, tena katika kusudi la MUNGU.

Ukiona wengine waliutumia vyema wakati wao ulipofika basi wapo pia ambao hawakuutumia vyema wakati wao ulipofika.
Majira na nyakati ni mambo ya muhimu sana kiroho japokuwa unatakiwa umsikilize sana ROHO MTAKATIFU.
Mfano wake ni kama wakati wa mvua za masika ukifika mkulima anatakiwa kupanda mbegu shambani. Majira ya kupanda yakipita ujue akitaka kupanda katika majira ya kuvuna hatafanikiwa.

Wengine majira yao yalipofika ROHO wa MUNGU aliwaambia kabla na wengine kupitia Neno au ndoto au maono au watumishi au Ufunuo. Kama ulijulishwa na MUNGU na majira hayo ukayadharau basi inakupasa kutubu na kumuomba MUNGU juu ya majira mapya ya wewe kuolewa.

Ndugu, tumia vyema nafasi ya kiroho ya wewe kuolewa iliyokuja mbele yako kwa kusudi la MUNGU.
1 Petro 4:7 ''............... iweni na akili, mkeshe katika sala. ''

Mfano hai ni huu.
Yakobo muda wake wa kukaribia kuoa aliambiwa hivi na mzazi wake '' Usitwae mke wa binti za Kanaani.-Mwanzo 28:1''

✓✓Yaani kwa leo tunaweza kusema kwamba ''usioe mwanamke ambaye hajaokolewa na YESU ilihali wewe umeokoka''

Sasa mwanawake aliyeokoka angemkataa ingekuwaje?
Maana yake kama ni kusudi la MUNGU huyo Mwanamke angepishana na majira.
Yakobo alizingatia hilo ndio maana majira yale yalitakiwa yaambatane na kupatikana Mwanamke safi wa kuolewa naye.
Hatimaye Yakobo akampenda Raheli Mwanamke sahihi aliyekaa katika kusudi la MUNGU kwa majira hayo.
Mwanzo 29:18 ''Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo.''
 
Changamoto ya Yakobo ilikuwa ni mahari hakuwa nayo maana alikuwa nchi ya mbali na wazazi wake, hivyo ili kumaliza kulipia mahari ya Kupata Mke ilibidi afanye kazi pale bila kulipwa kwa miaka 7, Hiyo miaka saba haikuja kwa sababu ya kuchunguzana bali miaka saba ni kwa sababu tu hakuwa na mahari, angekuwa na mahari inawezekana angeoa mwaka huo huo.
Sasa je, kama kwa kila jambo kuna majira yake na majira hayo kwa Raheli yalikuwa ya kuolewa angekataa ingekuwaje?
Maana yake majira ya wakati huo yangepita hivyo angetakiwa kusubiri majira mengine. Je ndugu majira yako inachukua miaka mingapi ili majira hayo mapya yafike?

◼️Ni vyema sana kuutambua wakati wa MUNGU na kuutumia kwa kusudi la MUNGU.

Kama kuna majira yako ya kufunga ndoa yaliyo kusudi la MUNGU yalipita basi omba maombi ya toba huku ukingoja majira mapya, na hayo majira mapya usikubali shetani akuzidi akili hata na hayo majira yakupite.

Wako watu waliingia katika ndoa kwa sababu tu majira yao yalifika na waliyatumia kwa kusudi la MUNGU.

Majira yako utayatambuaje?
Nimeshawahi kukuletea somo liitwalo MAOMBI YA KUOMBEA SIKU, NYAKATI NA MAJIRA YAKO na huko nilifafanua kwa kirefu hivyo litafute kwa ku-Search google ukiandika somo hilo Kisha majina yangu utaipata na utajifunza mengi kuhusu majira ila kwa ufupi majira yako ya kuingia katika ndoa unaweza ukayajua kwa ROHO MTAKATIFU kukufunulia(1 Kor 2:10), umri sahihi kukujulisha, Watumishi wa MUNGU kukujulisha, Neno la MUNGU kukujulisha n.k

2. Ana adabu inayompa heshima hata aonekane na kuolewa.

Mithali 11:16a '' Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;''
 
✓✓Adabu maana yake ni tabia njema hivyo wako wanawake walifanikiwa kuonekana mbele za wanaume wacha MUNGU waliohitaji wanawake wenye adabu kwa ajili ya kuwaoa.

✓✓Tabia njema ya mwanamke inaweza ikasababisha akapata Mchumba na kufunga ndoa takatifu.

◼️Tabia njema inaweza kuonekana katika mambo mengi sana, baadhi ya mambo muhimu ambako tabia njema inatakiwa kuonekana ni kwenye uvaaji wa adabu, usemi mzuri, hofu ya MUNGU, Utakatifu, nidhamu, maadili mema n.k

◼️Hakuna mwanaume hata mmoja Duniani anayetaka kuoa Mwanamke ambaye anakaa uchi uchi mbele za watu.

Japokuwa pia wapo baadhi ya wanawake huonyesha tabia njema kabla ya kuolewa lakini baada ya kuingia kwenye ndoa tabia njema huondoka, hiyo haifai kuwa hivyo.

✓✓Wapo wanawake wasanii kwa kuigiza tabia njema wakati katika uhalisia hawana, haifai kuwa hivyo.

✓✓Japokuwa wasanii na waigizaji wapo lakini pia wasioigiza wapo na hao tabia zao njema zinaweza kuwafanya waolewe.

Ndugu, kama una la kujifunza katika tabia njema basi jifunze leo.

Kumbuka anayetaka kukuoa anaweza kuwauliza wamama wa kanisani kwenu, watumishi, marafiki au majirani hivyo ukitoka huko ushuhuda mbaya kuhusu wewe unaweza kila siku ukawa unasingizia kwamba una roho ya kukataliwa na kumbe wala huna ila tu huna tabia njema.
Jifunze na zingatia somo hili itakusaidia.

Kumbuka tabia njema huwa ina kawaida ya kuonekana hivyo ikionekana kwako inaweza kukufanya ukafunga ndoa.

Tabia njema ilionekana kwa Rebeka ndio maana akaolewa na Isaka, Soma Mwanzo 24:42-46

3. Amepata kibali na neema ndani ya mwanaume sahihi anayetaka kuoa.

Esta 2:17 ''Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti.''
 
Hili sasa ni suala la kimaombi yaani unaomba mbele za MUNGU kwamba upate Mwanaume wa kukuoa ambaye wewe utapata neema na kibali machoni pake.

Usipopata neema na kibali machoni pa mwanaume huyo ujue hawezi kamwe kukuoa.

◼️Ukiona mwanamke fulani kafunga ndoa na mwanaume fulani ujue amepata neema na kibali mbele za mwanaume huyo.

Kitakachokutangulia wewe mbele ya mwanaume anayehitaji mke wa kufunga naye ndoa takatifu ni neema na kibali, ukikosa neema na kibali mbele ya mwanaume huyo ujue atakupita kama hakuoni maana umekosa neema na kibali machoni pake, akimpata aliyepata neema na kibali kwake atafunga naye ndoa huyo.

Hata wewe lazima mwanaume apate neema na kibali mbele zako ndipo utamkubali ili mfunge ndoa, hata Isaka alipata kibali mbele za Rebeka ndio maana akamkubalia wakaoana(Mwanzo 24:58 )

Jambo la kujua ni kwamba mawakala wa shetani wanaweza kukufanya ukose neema na kibali, hivyo tabia njema na maombi vinaweza kukufanya ukapata neema na kibali vilivyokuwa vimepotea na hivyo utafanikiwa kuolewa.
Omba maombi katika Jina la YESU KRISTO kwamba MUNGU akupe neema na kibali mbele za mwenzi wako aliye kusudi la lake  kwako.

4. Ameomba kwa MUNGU akapewa.

Mathayo 7:7-8 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.''
 
◼️Maombi ni ufunguo wa mambo mengi sana katika ulimwengu wa roho.

Biblia inasema ombeni nanyi mtapewa hicho mlichoomba ambacho mnakihitaji, ila tu muombe sawasawa na mapenzi ya MUNGU.
1 Yohana 5:14 '' Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.''

Tena Biblia inasema ombeni bia kukoma yaani omba hadi utakapopokea ulichoomba.
1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
 
Wengi huomba na kukoma kisha wanaanza lawama nyingi mbele za MUNGU japokuwa wao ndio wakosaji.
Lakini pia wapo wanawake walioitumia nafasi ya kuomba na MUNGU akawapa waume zao.

Ndugu, hata kwako inawezekana hakika kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.
Kama vile ambavyo unaweza ukaomba kitu chochote na MUNGU akakupa basi hata unaweza kuomba upewe mume na ukapewa.

Kama ambavyo unaweza ukafunga na kuomba hata na kutoa nadhiri au sadaka ili tu ufanikiwe jambo fulani unalolihitaji sana basi hata kuomba ili upate Mume unaweza kuomba na ukapata.

Hakuna andiko ambalo linakataza mtu kuomba mbele za MUNGU ili apate mume hivyo omba na utapewa kama Neno la MUNGU linavyosema.
Shida ya watu wengi hata wakipewa wanakataa walichopewa kwa sababu wanaomba huku wakihitaji wanaume tu wenye kazi nzuri na pesa, je katika wanaume wasio na kazi nzuri na sio matajiri hakuna anayeweza kuwa mume mwema wako? jibu ni kwamba yuko hivyo tatizo la wengi ni kumpangia MUNGU kitu ambacho hakiwezekani.

◼️Kitu kimoja MUNGU hawezi kukupa ni wewe kumuomba MUNGU akupe mwenzi wa ndoa harafu MUNGU akupe mpagani, hilo ni jambo ambalo MUNGU hawezi kulifanya.

Mathayo 7:9-11 ''Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana BABA yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? ''

Hakikisha tu na wewe umeokolewa na Bwana YESU na unaishi maisha matakatifu ya wokovu ili ukimuomba MUNGU akupe mwenzi atakupa mteule wa KRISTO safi.

Shida ni mabinti wengi kwenda kimwili na kuweka masharti yasiyo ya ki MUNGU ndio maana sauti ya MUNGU kwao imenyamaza na wanahangaika tu bila kupata jibu la MUNGU.
Wengine wanahitaji tu watu warefu kama kwamba wafupi hawakuumbwa na MUNGU, wanahitaji tu matajiri huku wamesahau kwamba inawezekana kabisa tajiri wa leo akawa ndio masikini wa kesho huku masikini wa leo akawa ndio tajiri wa kesho.
Mimi Peter Mabula huwa naongea na watu wengi sana na kuwaombea wengi sana na huwa najifunza mengi sana kwa wanawake ambao hawajaolewa wanaohitaji kuolewa.
Wapo ambao wamewahi kuniambia kwamba niwaombee kwa MUNGU ili MUNGU awape vijana ambao waliwahi kusali nao zamani au waliwahi kusoma nao au waliwahi kuishi nao. Swali, je kama hao wote sio kusudi la MUNGU si mhusika atakuwa anapishana na kusudi la MUNGU kila mara?

Mtu mmoja yeye alinipigia simu akiniambia kwamba ''Mtumishi mabula niombee niolewe na fulani na nimeshikilia picha yake muda huu'' Nilitamani kucheka ila sikutaka nimkwaze, ila muda ule ule nilifunuliwa kwamba huyo wa kwenye picha sio mpango wa MUNGU kwa binti huyo, nilimuombea huku akisikiliza kwa makini na sikumhusisha wa kwenye picha katika maombi yangu kitu kilichomfanya binti yule kuchukia na tangu siku hiyo wala hakunitafuta tena kwa muda mrefu sana.

◼️Unapomuomba MUNGU basi mhitaji MUNGU aamue juu yako na sio kuomba huku umeshajiamulia wewe.

Wapo waliomuomba MUNGU juu ya kuwabariki waume na hakika walipata waume zao.
Asomaye somo hili na afahamu.

5. Anautambua ulimwengu roho vyema.

1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''
 
Iko wazi sana kwamba anayeweza kutufunulia ya sirini yaliyo katika ulimwengu wa roho ni ROHO MTAKATIFU pekee.
Kumbuka hakuna jambo lolote huanzia tu katika ulimwengu wa mwili bali kila jambo lina chanzo katika ulimwengu wa roho.
Hivyo basi ukitaka kujua chochote kwenye ulimwengu wa roho kuhusu wewe basi mhitaji sana ROHO MTAKATIFU kukujulisha na kukusaidia.
Kumbuka pia kwamba ROHO MTAKATIFU yuko tu katika watu ambao wamempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao, hivyo ukimhitaji ROHO MTAKATIFU ujue kwanza unamhitaji YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako.
Sasa ulimwengu wa roho anayeweza kuujua vyema ni ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATUFU hujulisha yaliyo ya MUNGU kuhusu sisi hivyo anaweza hata akakujulisha mwenzi wako, majira sahihi, nini ufanye na nani umwambie ili akusaidie maombi.
Kwa kutokuujua vyema ulimwengu wa roho wako watu hata hujulishwa vifungo vinavyowazuia kupata baraka zao ila wao hata huwa hawaombi juu ya kuharibu vifungo hivyo vya giza walivyojulishwa.
Ukitaka kuolewa ndoa takatifu basi hakikisha pia umefunguliwa vifungo vinavyozuia watu kufunga ndoa takatifu.
Viko vifungo vingi sana vinaweza kukuzuilia kufunga ndoa, hivyo hakikisha unajua kupambana kimaombi, baadhi ya vifungo hivyo ni maroho ya kipepo ya kurithi ya ukoo,familia au jamii yako.
Ezekiel 16:44-45 '' Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake. Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.''

Biblia inasema ''Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.'' inawezekana Mama yako au bibi yako alizalia nyumbani, inawezekana mama yako alikuwa wa kupata mchumba na kuachwa na wewe umerithi maroho hayo ya giza na sasa unatembea katika hila hizo za giza za kukuzuia, inawezekana mama yako alitafuta mchumba kwa miaka kumi bila mafanikio na akaja akaolewa akiwa na zaidi ya miaka 40 hivyo na wewe unatembea katika njia hiyo hiyo, leo katika jina la YESU KRISTO jitenge na maroho ya kuzimu yaliyoshikilia ndugu zako wa kike kuhusu kuolewa.
Vifungo ni vingi mno vinaweza kumzuia mtu, baadhi ya vifungo kwa ufupi ni hivi, kurushiwa mapepo, ndoa za majini mahaba, kurogwa, agano la kipepo lililokufunga, umefungwa ufahamu, una roho ya kukata tamaa na roho ya mazoelea, uko katika vifungo vya dhambi, unashikiliwa na madhabahu fulani ya giza, umeshikiliwa na sadaka/kafara iliyotolewa katika madhabahu za giza, una alama za kipepo rohoni, umezibwa rohoni, una maroho ya kipepo ya kiume yaani yanakufanya mbele za wanaume uonekane kama mwanaume mwenzao na sio mwanamke hivyo hakuna atakayehitaji kukuchumbia, huna macho ya rohoni n.k
Ndugu, wako walioona vitu kwenye ulimwengu wa roho na wakavishughulikia kimaombi na vikawachia kisha wakafunga ndoa takatifu.
Ajifunzaye ujumbe huu na afahamu.
Katika somo hili sina maana ya kwamba walio katika ndoa ndio watakatifu sana bali nimezungumzia sifa kiroho na kimwili zilizopelekea mwanamke kuolewa, hivyo fanyia kazi na itakusaidia sana.
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292( whatsapp).
Ubarikiwe.

Comments