![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu atukuzwe sana Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna watu kadhaa nimewahi kuwasikia wakisema maneno kuhusu baadhi ya watu kwamba watu hao waliachiwa laana na wazazi wao.
Utasikia "Ana laana ya Mama yake ambaye sasa ni marehemu"
"Huyu Baba yake kabla ya kufariki alimwachia laana" na maneno ya namna mengi.
Jambo hili limenipa tafakari kidogo kwamba Baadhi ya wazazi wanapoondoka Duniani huondokaje?
Ni kweli kabisa sio Kila Mzazi hujua muda wake wa kuondoka Duniani hata aache maneno ya Baraka kwa Watoto wake, ila ikitokea neema hiyo ya Mzazi kujua kwamba anaondoka ni vizuri sana kuacha Watoto wako kwa kuwabariki na sio kuwalaani.
Ona mfano huu katika kumbukumbu sura ya 33 nitasoma mstari wa 1 na wa 29
Kumbu 33:1 "Hii ndiyo baraka ya Musa, huyo mtu wa MUNGU, aliyowabarikia wana wa Israeli kabla ya kufa kwake."
Kumbu 33:29 "U heri, Israeli. Ni nani aliye kama wewe, taifa lililookolewa na BWANA! Ndiye ngao ya msaada wako, Na upanga wa utukufu wako; Na adui zako watajitiisha chini yako, Nawe utapakanyaga mahali pao pa juu."
Ni kweli kabisa inawezekana Yuko mtoto hakuwa vizuri na wazazi wake, na wakati wao wa Mwisho wazazi walitamka Mabaya na sio mema na Mabaya hayo yamemtesa aliyetamkiwa.
Leo Kuna wazazi akiona tu mtoto wake amechelewa kwenda kumuona Kijijini kwa sababu amenyimwa ruhusa kazini yeye Mzazi ana mlaani mtoto wake.
Wewe unayesoma ujumbe huu muombe MUNGU wakati wako wa kuondoka ukifika hata kama ni miaka 60 ijayo uache Baraka na sio laana kwa Watoto wako.
Lengo la ujumbe huu ni kwamba Wewe unayesoma somo hili katika wakati wako hata kama ni miaka 100 ijayo, ukagundua kwa neema ya KRISTO kwamba hutakuwa na muda mrefu wa kuishi ni vizuri sana kuwabariki unaowaacha na sio kuwalaani, maana ukiwalaana au ukiwabariki hutafaidika na laana hiyo au baraka hiyo maana wewe hutakuwepo.
Hivyo ni heri kuwabariki na kuwasamehe kama walikukosea, ukiipata neema hiyo lizingatie hili maana pia usipowasamehe kwa sababu walikukosea ujue hutasamehewa na MUNGU wewe pia hivyo hutaingia uzima wa milele kwa sababu ya kutokusanehe.
Mathayo 6:14-15 " Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu."
Utunze ujumbe huu moyoni mwako siku zote za maisha yako ili ukipata neema ya kujua Muda wako wa kuondoka basi uache baraka na sio laana.
Ngoja nikuingize kwenye mifano 4 ya WOSIA WA MWISHO WA MZAZI KWA MTOTO na Mfano hai wa Stefano kwa waliokuwa wanamtesa ili uone faida za kubariki na hasara za kuwalaani uliowaacha.
✓✓Mfano wa Kwanza: Isaka Aliacha Baraka kwa Yakobo na kumsihi asije akaoa Mwanamke mpagani.
Mwanzo 28:1-4 " Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako.
Na MUNGU Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila. Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, MUNGU aliyompa Ibrahimu."
Katika Maandiko haya ndio maneno ya Mwisho ya Isaka kwa Mtoto wake aitwaye Yakobo.
Isaka alimbariki Yakobo na kumsihi asioe waabudu shetani Yaani wakanani.
Kwanini wewe upange kuacha laana kwa Watoto wako na sio kuacha Baraka?
Ukiacha laana ujue watakaoteseka ni Wajukuu zako na inawezekana ukoo wako ukafutika mapema Duniani kwa sababu ya laana uliyoacha.
Ndugu, hakikisha unaacha Baraka.
✓✓Mfano wa pili: Daudi alimwusia Solomon ashike maelekezo ya MUNGU ndipo atafanikiwa Kila aendako na Kila afanyalo.
1 Wafalme 2:1-3 " Basi SIKU YA KUFA KWAKE DAUDI IKAKARIBIA, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;"
Daudi alipojua amekaribia kufa alimwusia mwanawe kwamba ashike maelekezo ya MUNGU na atembee kwenye Neno la MUNGU ndipo atafanikiwa Kila alifanyalo na atafanikiwa Kila aendako.
✓✓Mfano wa tatu: Yakobo alibariki na kulaani baadhi ya Watoto wake.
Habari hii utaisoma katika Mwanzo 49, Mimi nakusomea maandiko machache tu.
Mwanzo 49:1-2 " Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu."
Rubeni kwa makosa yake akatamkiwa Mabaya ya kuondolewa ukuu na ikaja kuwa hivyo hivyo.
Mwanzo 49:4 "Umeruka mpaka kama maji, basi USIWE NA UKUU, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.
Yuda anatabiriwa kwamba kutoka katika kabila lake Bwana YESU KRISTO atatokea na ikawa hivyo.
Mwanzo 49:10 "Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii."
Je Wewe Kwanini usiache baraka kwa Watoto wako?
Unaweza ukaumba madaraka, vyeo, uchumi Mzuri kwa uzao wako na ikaja kuwa hivyo.
Ndugu uweke moyoni ujumbe huu ili siku Ile uache baraka na sio laana.
Ngoja nikupe shuhuda hizi kuhusu Mimi.
Mimi Peter Mabula niliishi na Bibi yangu mzaa Baba katika hatua zake za Mwisho kabla ya kuondoka Duniani. Maneno yake katika siku zake za Mwisho ni kuwabariki tu Watoto wake na sisi Wajukuu zake. Usiku wa Mwisho kabla hajaondoka Duniani alikuwa akiimba Tenzi za rohoni, akifanya Maombi akimweleza Bwana YESU KRISTO apokee roho yake na akiimba nyimbo za kumsifu MUNGU. Nilienda chumbani kwake katikati ya usiku nikiwa na hofu maana hakulala kabisa nikamuuliza "Bibi ni kwema" Bibi akasema "Ni kwema Peter Mjukuu wangu" nikarudi chumbani kwangu.
Asubuhi saa kumi na Moja Asubuhi wakati nikimuaga ili niwahi shuleni maana nilikuwa darasa la sita akaniambia maneno haya " Mjukuu wangu utafaulu, mtakuwa Salama (akinitaja Mimi na majina ya wengine), mtabaki Salama n.k" nikamuuliza "Mbona Bibi unazungumza maneno kana kwamba wewe hutakuwepo?" Akatabasamu na kuniambia niwe na amani. Nikaenda shule, Masaa machache baadae nikaja kujulishwa shuleni kwamba Bibi amefariki.
Napenda kukuambia kwamba darasa Zima mtihani wa darasa la Saba Mwaka uliifuata nilifaulu peke yangu kwenda sekondari.
Ndugu unaacha baraka Gani?
Acha baraka na sio laana.
✓✓Mfano wa nne: Stefano katika dakika yake ya Mwisho Duniani aliwaombea tu msamaha waliomkosea.
Matendo 7:60 "Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, BWANA, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake."
Stefano angeweza angewalaani na laana hiyo ingewapata lakini akachagua fungu lililo jema kwa kuwaombea Toba.
Ndugu kumbuka sana kuacha Baraka na sio laana.
Ushuhuda mwingine ni kwamba Mimi Sina Baba wala Mama, nililelewa na Shangazi yangu. Mwishoni mwa Mwaka Jana Shangazi aliondoka Duniani na Mimi nilikuwa mkoa wa mbali sana na alikokuwa anaishi Shangazi. Lakini siku Shangazi anafariki nilijua bila kuambiwa na Mtu. Muda huo nilikuwa nimekaa kwenye kiti katikati ya watu zaidi ya 80, ghafla nikaanza kusikia baridi na utulivu wa ajabu ukatokea na kwa sekunde kadhaa nikawa siwezi kusikia sauti hata ya walio jirani, nikiwa nimeduwaa nikasikia sauti ya Shangazi yangu akianza kwa kusema "Peter mkae salama" nilijua kabisa MUNGU amemchukua Shangazi na ilikuwa hivyo.
Aliniachia Neno la kubaki Salama.
Ndugu zangu ni vizuri sana kuacha Baraka na sio laana.
MUNGU atupe Mimi na Wewe Msomaji wa masomo yangu Mwisho mwema, katika majira hayo tuache baraka na sio laana.
Kama hujaokoka hakikisha unaokoka.
Mpokee YESU KRISTO Leo awe Bwana na Mwokozi wako.
Acha dhambi zote, acha makosa na maovu yote.
Hakikisha YESU KRISTO anakuwa Mwokozi wako milele.
Kumbuka hakuna uzima wa milele nje na YESU KRISTO, hivyo kama kweli unahitaji uzima wa milele okoka kwa kumpokea YESU KRISTO awe Mwokozi wako
MUNGU akubariki
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292
Ubarikiwe
Comments