ISHINDE SILAHA YA MWISHO YA SHETANI BAADA YA WEWE KUMSHINDA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu kujifunza Neno la MUNGU.

✓✓Silaha kubwa ambayo shetani huitumia unapomshinda ni "mashtaka "

Mashtaka ni nini?

✓✓Mashtaka ni malalamiko anayoyatoa mtu mbele za watu au mamlaka kwa ajili ya mtu mwingine.

✓✓Mashtaka ni tuhuma dhidi ya mtu fulani, tuhuma za shetani siku zote ni za uongo.

✓✓Mashtaka ni kumnyooshea kidole mtu ili kumfanya asiendelee katika kazi njema ya MUNGU.

Mashtaka ya shetani ni mishale ya shetani yenye sumu ambayo ikiingia ndani ya mtu hushambulia moyo.

Baadhi ya wataalamu wa saikolojia wanasema kwamba vitu vitatu vinavyoumiza zaidi duniani cha kwanza ni kifo cha mwenzi wa maisha, kitu cha pili kinachoumiza sana ni deni/kudaiwa na kitu cha tatu kinachoumiza sana ni mashtaka ya uongo.

✓✓Sasa shetani kwa sababu hutumia watu basi utashangaa baada ya wewe kumshinda shetani kwenye vita ya kiroho utaona watu walio upande wa shetani wanalalamika kuhusu wewe, ukiona ni hivyo basi tambua kwamba hapo shetani anaitumia silaha yake ya mwisho kubwa iitwayo mashtaka, silaha hii iitwayo mashtaka huwa shetani anaitumia baada ya wewe mteule wa KRISTO kumshinda yeye na mawakaka zake.

◼️Biblia inamwita shetani "Mshitaki " yaani mpeleka mashitaka, na huwa anatumia silaha hii ya mashitaka pale unapomshinda katika vita ya kiroho.

1 Petro 5:8 "Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze."

Kuna watu humezwa na mashtaka ya shetani na kujikuta wanasalimu amri kwa shetani na kushindwa vita ya kiroho.

Nini nataka kusema?

◼️Wakati mwingine ukimshinda shetani huwa anabakiza silaha yake ya mwisho ambayo ni mashtaka, hata silaha hiyo inakupasa kuishinda kwa maombi katika jina la YESU KRISTO Mwokozi na kwa kuwa na akili za kiroho zinazofunuliwa na Neno la MUNGU kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.

✓✓Ukiona mtumishi wa MUNGU unashtakiwa kwa kusingiziwa ujue hapo shetani anaitumia silaha yake ya mwisho iitwayo mashtaka.

✓✓Ukiona Watu wa MUNGU Kanisani wanashitakiana kwa kusingiziana ujue shetani anajaribu kuwaingia baadhi ya watu ili aitumie silaha yake ya Mwisho iitwayo mashtaka.

✓✓Ukiona mtu mbaya amekujaribu kwa nguvu za giza amekushindwa, silaha ya mwisho baada ya kumshinda shetani ni mashtaka hivyo usishangae ukianza kuzushiwa mambo mengi ya uongo.

Mashtaka ya uongo humfanya anayeshitakiwa kunyong'onyea, kudhoofika na kutengwa ili hatimaye asalimu amri kwa shetani.

Mawakala wa shetani huajiri watu karibu ili wawe sehemu ya mashtaka ili kukuletea athari kubwa zaidi.

Inaumiza sana pale ambapo mtu wa karibu yako anapotumika na shetani ili kukuweka wewe hatiani kwa uongo.

Zaburi 41:9 "Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake."

Kuna huduma zilikufa kwa sababu tu watu wa karibu na Mchungaji wanaotumika kipepo walimsingizia Mchungaji kwa uongo na kusababisha huduma hiyo njema kufa.

Ziko ndoa zilikufa baada ya mashtaka ya uongo kutokea, waletaji wa mashtaka hayo ni mawakala wa shetani wanaotafuta masilahi yao katika ndoa hiyo.

Shetani hasa huwalenga sana watumishi wa MUNGU kwa habari ya mashtaka ya uongo ili kuwafanya watumishi hao wasiwe na nguvu za kiroho baada ya kujeruhika na hila hizo za shetani.

✓✓Watu wa MUNGU wengi hupenda kufanyia kazi mambo ya uongo yanayotokana na silaha ya mwisho ya shetani baada ya kushindwa na watumishi waaminifu wa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

Shetani anapoitumia silaha hii ya mashtaka ni ili kuchafua mahusiano mema baina ya watu wa MUNGU.

Mithali 10:18 "Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu."

Malengo ya mawakala wa shetani "washitaki" wanapotumia silaha hii ya mashtaka ni ili

1. Kukushushia hadhi na kukuabisha.

2. Kukuangusha dhambini.

3. Kukudhibiti na kudhoofisha huduma yako.

4. Kuzalisha chuki na uchungu na kuleta matengano.

5. Kukukatisha tamaa na kukuchanganya.

6. Kuwageuza marafiki ili wawe maadui.

7. Unageuzwa wewe mwenyewe uwe mshitaki kwa kukufanya uwe mtu wa kulalamika tu na kuitafuta haki hata kwa kuwashitaki wengine.

8. Kukuzuia ili usiendelee katika mipango.

9. Kukutia hofu na kukufanya upunguze hali yako ya kujiamini.

Kumbuka hofu ni pepo mchafu mtangulizi wa mapepo mengine.

10. Ili kukuangamiza au kuangamiza huduma yako au kuangamiza uchumi wako.

Mfano ni Nabothi ambaye aliuawa kwa kusingiziwa kwamba amemtukana MUNGU na mfalme, wakiandaliwa watu waovu ili waseme mbele ya watu kwamba ni kweli alifanya kosa hilo, kumbe wala hakufanya hivyo.

1 Wafalme 21:9-13 " Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa."

Nini ufanye katika mazingira ya kushtakiwa uongo?

1. Omba ROHO MTAKATIFU akupe maneno sahihi ya kuongea ili usiingie katika mitego ya mawakala wa shetani.

Marko 13:9-11 "Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao. Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote.
Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni ROHO MTAKATIFU."

2. Mtegemee MUNGU kwa maombi na atakushindia.

Ayubu 19:25" Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi."

✓✓Usijitetee, mwache MUNGU akutetee, usijipiganie mwache YESU KRISTO akushindie.

✓✓Usipunguze chochote katika kazi ya MUNGU inayoifanya.

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments