![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
✓✓Neno hili nawiwa rohoni mwangu nilitoe kwa njia ya ushauri kwa vijana na mabinti wenye wachumba au wanaotarajia kupata wachumba kisha ifuate kufunga Ndoa Takatifu
Mambo ya kuzingatia katika kumpata mchumba na wakati wa uchumba.
1. Usimkubali mtu kwa sababu ya vitisho vyake.
Nimewahi kukutana na kesi za namna hii. Mtu anamtisha binti au kijana kwamba yeye ndiye atakuwa mkewe au mumewe hivyo hata aende wapi atarudi tu.
✓✓Ndugu mkubali mtu kwa sababu umempenda rohoni mwako na sio kwa sababu ya vitisho.
Binti mmoja alimkataa kijana fulani, kijana huyo akamwambia huyo binti kwamba hatapata kamwe mwanaume wa kumuoa.
Binti alipokataliwa na wanaume wawili akadhani ni kweli yale maneno ya mtu wa zamani.
Ndugu kama huyo kijana anataka kulazimisha uchumba na wewe kwa nguvu kwa vitisho Usimkubali kamwe.
◼️Funga ndoa na mtu unayempenda wewe mwenyewe bila shinikizo wa kitisho, hilo ndilo agizo la MUNGU.
Hesabu 36:6 "BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, NA WAOLEWE NA WAUME WAWAPENDAO; LAKINI NA WAOLEWE KATIKA JAMAA YA KABILA YA BABA ZAO."
◼️Jambo Moja tu kuzingatia ni kwamba Funga Ndoa na Mtu kutoka JAMAA yenu yaani JAMAA ya Wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Wagalatia 6:10 ''Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.''
✓✓MUNGU anataka ufunge ndoa na mtu uliyempenda na sio aliyekutisha.
Vitisho hivyo vina sababu, inawezekana anataka tu ufunge naye ndoa ili akukomoe na kuanza kukutesa.
✓✓Ndugu, Wakristo hawafungi ndoa ili kukomoana bali wanafunga ndoa kwa sababu wamependana kwa upendo sahihi wa ki MUNGU na katika kusudi la MUNGU.
MUNGU anataka ufunge ndoa na mtu ambaye ametokana na yeye na mtu aliyetokana na MUNGU huyo lazima utampenda tu.
2. Mkubali mtu kwa sababu umempenda na una amani naye.
Mfano ni huu ambapo Isaka alimpenda Rebeka ndio maana akamuoa.
Mwanzo 24:67 ".......... akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; ........"
◼️Mkubali mtu kwa wewe binafsi kumpenda mtu huyo na moyoni una amani naye.
Sio watu wengine wampende kisha wakulazimishe na wewe kumpenda ili ufunge naye ndoa.
Ndugu mpende wewe mwenyewe na sio wengine wampende kwa ajili yako.
3. Usimkubali mtu kwa kulazimishwa au kushawishiwa.
Hii ndio hatari mbaya sana.
Kama unatafuta mtu wa kufunga naye ndoa basi maamuzi juu ya huyo yatoke ndani yako kulingana na mtazamo wako na Neno la MUNGU, usikubali kulazimishwa kumpenda mtu ili ufunge naye ndoa.
Hata wazazi au Watumishi wa MUNGU wasikushawishi au kukulazimisha kufunga Ndoa na Mtu kama Wewe binafsi hujampenda.
Usikubali kushawishiwa kufunga ndoa na kijana fulani au binti fulani, bali wewe mwenyewe binafsi mpende mtu huyo.
Yakobo alimpenda Raheli hivyo alikubali kumgharamikia miaka sasa ili ampate kwa sababu tu alikuwa anampenda mwenyewe bila kulazimishwa wala kushawishiwa.
Mwanzo 29:18-22 " Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu."
Yakobo alimpenda Raheli bila kulazimishwa wala kushawishiwa ndio alivumilia katika utakatifu hadi ampate.
Kama angekuwa amelazimishwa au kushawishiwa asingeweza kuvumilia kwa utakatifu muda mrefu, angechagua mwingine au angewaza vingine lakini kwa sababu alimpenda alivumilia hadi siku ya ndoa.
Natamani wewe kijana au binti unayesoma somo hili, natamani uwe mvumilivu, usianguke dhambini na hakikisha unaingia katika uchumba na mtu uliyempenda mwenyewe, sio kishawishiwa au kulazimishwa.
4. Hakikisha mchumba wako ana YESU na anaishi maisha matakatifu ya wokovu.
Hili ni jambo la muhimu sana na la kuzingatia sana sana.
Maana katika KRISTO Biblia inasema " na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana(YESU) mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.- Waefeso 4:3-6"
Kama Wakristo kuna kitu tunahifadhi, tunahifadhi "Umoja wa ROHO MTAKATIFU "
Umoja huo hutufanya tuwe mwili wa KRISTO, vipi kama watu wawili wameoana lakini mmoja yuko katika mwili wa KRISTO na mwingine yuko katika mwili wa shetani?
Ndoa hiyo inaweza kumfanya aliye mwili wa KRISTO amwache KRISTO, ni hatari sana.
Hivyo kwa ambao wako kwenye ndoa tayari ila wako na watu ambao hawana YESU waishi na watu hao kwa akili bila kuwaruhusu kukutoa kwa YESU KRISTO Mwokozi.
◼️Ila kwa ambao hawajaingia katika ndoa usijaribu kamwe kuingia katika ndoa na mtu asiye na YESU KRISTO.
◼️Wewe mwili wa KRISTO usikubali kamwe kuingia katika ndoa na mtu aliye mwili wa shetani.
Umoja wa ROHO MTAKATIFU unatufanya tuwe katika YESU KRISTO ambaye ni mmoja, umoja wa ROHO MTAKATIFU unatufanya tuwe katika MUNGU mmoja tu tena tuwe katika imani moja yaani wokovu wa KRISTO, hivyo haiwezekani aliye mwili wa KRISTO aungane na mtu wa shetani, ndugu yatafakari maandiko hayo ya Waefeso 4:3-6 ili usikengeuka na kuifuata miungu ukamwacha MUNGU aliye hai.
Ndugu, hakikisha mchumba wako ana YESU KRISTO na anaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU ulio wa thamani sana.
5. Shirikiana na Mchungaji wako na Kanisa katika hatua zote za uchumba hadi ndoa.
Watu wengi wanapopata wachumba hujiweka mbali na wachungaji wao na hujiweka mbali na Kanisa, hiyo ni mbaya sana.
Kuna watu uchumba wao ulikufa kwa sababu hii tu ya kukaa mbali na mchungaji na kukaa mbali na Kanisa.
Mfano binti umepata mchumba hukumwambia Mchungaji wako, mahari imetolewa Viongozi wa Kanisa na Mchungaji hawajui, tarehe ya ndoa mmeshapanga tayari ndipo unamshirikisha Mchungaji kwa sababu tu ndio yeye atafungisha ndoa hiyo, ndugu Mchungaji anaweza akakataa hatua zote ili mwanze upya na ajiridhishe kwamba mnatembea kwenye utakatifu, ikiwa tu ni hivyo unaweza kuchelewa sana kufunga ndoa hata kama unampenda mchumba wako na umemthibitisha kwamba anakufaa.
Ndugu, shirikisha mchungaji wako na hata Kanisa katika hatua zote za uchumba hadi ndoa.
Biblia inasema "Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote. Msidanganyike, MUNGU hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.-Wagalatia 6:6-7
✓✓Hivyo wewe kama Mwanafunzi(Mwamini au mshirika) mshirikishe Mkufunzi wako yaani Mchungaji wako mema yote.
Tena Biblia inasema kwamba mambo yote yatendeke kwa utaratibu na uzuri
1 Wakorintho 14:40 "Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu."
Sasa wewe ukijichanganya na kukengeuka usifuate utaratibu huu unaweza kunasa au kukwama na ukaanza kudai shetani kaingilia kati kumbe tatizo ni kukurupuka kwako usifuate utaratibu na uzuri utupasao Wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Tena Biblia inasema kila mtu na aiheshimu mamlaka iliyo kuu.
Warumi 13:1-2 " Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa MUNGU; na ile iliyopo umeamriwa na MUNGU. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la MUNGU; nao washindanao watajipatia hukumu."
◼️Kanisa ni mamlaka kuu mno na katika hili la ndoa unaihitaji sana mamlaka hii, usipoiheshimu hii mamlaka unaweza kukwama hata kama unadai umeonyesha kwa mchumba wako huyo unayetaka kufunga naye ndoa.
◼️Kumbuka mchungaji ana sehemu yake na Kanisa lina sehemu yake hivyo ukihitaji ndoa yenye afya shirikisha Kanisa na Mchungaji.
Katika hili sina maana umwambie kila mwana Kanisa lakini ukiwaambia viongozi wa juu Kanisani hapo umeliambia Kanisa, hiyo ni muhimu sana na hapo utapata sapoti nyingi ya maombi, wahudhuriaji siku ya ndoa, washauri wazuri, wasaidizi siku ya kufunga ndoa na hata michango n.k
Hivyo shirikiana na Mchungaji wako na Kanisa katika hatua zote za uchumba hadi ndoa.
6. Usikubali kamwe kufanya uasherati na mchumba wako.
Hiki ndicho kikwazo kikuu kinachozuia wachumba wasioane, hata wakioana wasiwe na ndoa njema na yenye furaha.
Wengi wameachwa na wachumba wao kwa maumivu kwa sababu tu ya dhambi ya uasherati walioifanya na wachumba zao.
1 Wakorintho 6:18 "Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."
✓✓Uasherati huleta maagano ya kipepo.
✓✓Uasherati humfanya shetani aingie ndani yenu na kuwatesa, na kwa sababu shetani kazi yake ni kuua na kuharibu basi atahakikisha anaua uchumba na ndoa.
✓✓Uasherati kwa wachumba huondoa ulinzi wa MUNGU kwenye uchumba huo, ulinzi wa MUNGU ukiondoka ujue mapepo yanachukua nafasi.
Ndugu kama kweli unahitaji kuingia katika ndoa takatifu basi jambo la kwanza jitenge mbali na dhambi ya uasherati.
Waefeso 5:3 "Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;"
Mchumba wako kama anataka mfanye uasherati mwache haraka sana maana huyo hakufai, huyo katumwa na shetani ili aharibu maisha yako, usikubali kamwe.
✓✓Uasherati ni mojawapo ya ibada ya sanamu yaani kumwabudu shetani.
Wakolosai 3:5-6 "Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU."
✓✓Uasherati huuchafua mwili wote kiroho ndio baada ya muda utasikia "nina roho ya kukataliwa n.k" kumbe tatizo ni mwili kunajisiwa kiroho kupitia uasherati.
7. Kwa kila jambo na kila hatua ya kuelekea ndoa tanguliza maombi.
Mathayo 7:7 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;"
◼️Maombi ndio ufunguo mkubwa zaidi unaotumika kufungua kila kitu katika ulimwengu wa roho.
Usipokuwa muombaji ujue wachawi au wakuu wa giza wanaweza kukuzuia kuingia kwenye ndoa hivyo kila ukipata mchumba anakuacha, kila ukipata mchumba wanamfanya akuchezee kisha anakuacha.
Usipokuwa muombaji ujue majini wanaweza kukaa ndani yako kila ukipata mchumba ili uchumba wenu ufe na huo uchumba unakufa kweli, au kila ukipata mchumba mapepo yanamvamia mchumba wako anakuacha.
Bila maombi wewe kuingia kwenye ndoa unaweza kuwa unakusikia tu mitandao ya kijamii na kwenye Tv, kama unahitaji kuingia katika ndoa unahitaji sana Kuwa muombaji katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.
1 Wathesalonike 5:17 "ombeni bila kukoma;"
Maombi ni maisha ya kila mteule wa MUNGU katika KRISTO YESU, husisha sana maombi katika kila hatua, omba kabla kisha umshukuru MUNGU baada ya kukufanikisha.
Kumbuka pia maombi ya mtu asiye haki ni machukizo kwa MUNGU
Hivyo hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO ndipo utakuwa muombaji sahihi.
8. Ridhika na mtu huyo Kabla hujaanza uchumba naye.
Kuridhika ni nini?
✓✓Kuridhika ni kutosheka hivyo tosheka na mtu huyo kabla hujaanza naye uchumba.
1 Timotheo 6:6 "Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa."
Utakatifu na kuridhika ni faida kubwa.
Kuna watu anampata mtu anamwambia na uchumba unaanza lakini moyoni mwake hajaridhika naye hivyo akitokea mwingine ambaye ataridhika naye zaidi anamwacha mchumba wa kwanza na kumfuata huyu mpya, akitokea mwingine akamridhisha zaidi anamwache na huyu ili amfuate yule mpya.
Ndugu ukiwa mtu wa namna hiyo kwanza utakuwa hujitambui maana utajikuta unawaacha hata 20 na bado hutampata atakayekuridhisha kama unavyotaka.
Wanadamu wote duniani ni wazuri sana inategemea tu na mtazamo wako hivyo ridhika na mtu mapema kabla hata hujaanzisha uhusiano naye ili usiwe mtu wa kutangatanga, ili usimwache kipindi yeye anakupenda hivyo kumuumiza sana moyo wake, haifai kuwa hivyo.
Hivyo wewe kama ni mwanaume hakikisha kwa mtazamo wako, hakikisha rohoni mwako amekuridhisha ndipo mweleze ili muwe wachumba kisha mfunge ndoa.
Kama wewe ni mwanamke ridhika mtu kabla hujamkubalia.
Usiwe wa kukubali leo kisha kesho unamkataa kwa sababu ametokea aliye bora zaidi kwako.
Mtu asiyeridhika hata akiingia kwenye ndoa atakuwa na tabia hiyo chafu ya kutokuridhika lakini Neno la MUNGU linaonya likisema.
Waebrania 13:4 "Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu."
Kuna wanandoa leo wanatamani kuvunja ndoa kwa sababu ya hii sababu chafu ya kutokuridhika.
Kuna wanandoa leo hadi wanatamani wake zao au waume zao wafe ili wafunge ndoa na watu wapya, kumbe tatizo ni roho ya kutokuridhika na kutosheka.
Kama uko kwenye ndoa huwa mawashauri "Muombee mwenzi wako na kumshauri, mtengeneze kwa utakatifu na mfundishe kwa utakatifu ili atimie katika viwango vyako hata uridhike naye"
Kabla ya uchumba ridhika kwanza rohoni mwako na mtu huyo ndipo ukubali kuingia naye katika uchumba.
Sisi Wateule wa KRISTO tunayo sheria ya KRISTO ambayo inasema ndio yetu na iwe ndio , sio yetu na iwe sio.
Usikubali kubadilika badilika kwa sababu ya tabia zako mbaya.
Yakobo 5:12 "Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu."
9. Jiandae kuingia katika ndoa na sio vinginevyo.
Kuna watu wanatafuta wachumba huku wao wenyewe hawako tayari kuingia katika ndoa, ndugu naomba usiwe wewe.
◼️Kama unafikia hatua ya kutafuta mchumba hakikisha uko pia tayari kuingia katika ndoa.
Leo kuna wanafunzi wana wachumba harafu wana mpango wa kuoana miaka kumi ijayo. Uchumba wa namna hiyo utawavurugia masomo na uchumba huo unaweza kuwa chanzo cha mtu kutenda dhambi na kufeli maisha, uchumba kama huo unaweza kuja kuvunjika katika kipindi kigumu na kuleta maumivu kwa mmoja.
Mfano baada ya masomo sekondari mmoja anaenda chuo au anapata kazi na kupata mtu mpya kwenye kazi na wewe huna kazi, anaweza kukuacha na kukuletea maumivu mabaya.
Huu ni mfano mmoja tu kati ya mifano hai mingi ya madhara ya kuwa na mchumba huku hauko tayari kwa ndoa wakati huo.
Ndugu jifunze kwa Ahusuero ambaye alipompenda Esta miongoni mwa mabinti wengi mpango wake ulikuwa ndoa na sio vinginevyo.
Esta 2:17 "Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti."
Ndio maana baada ya kumpenda akamuoa ndio maana Biblia inasema akawa malkia yaani mke wa mfalme, mtu hawezi kuwa malkia yaani mke wa mfalme kama hajaolewa na mfalme huyo. Hivyo Esta alikuwa malkia baada ya kuolewa na mfalme Ahusuero, lengo la Ahusuero lilikuwa ni ndoa na sio vinginevyo.
Hata wewe unapoanzisha uchumba lengo lako liwe Ndoa na sio vinginevyo, anzisha uchumba kipindi ambacho uko tayari kufunga ndoa.
Leo kuna mpaka watu wako katika uchumba miaka 8 au 5 wakidai wanachunguzana, huo ni uongo.
Uchumba mzuri ni ule wa kati ya miezi 6 hadi mwaka mmoja na nusu muwe mmefunga ndoa.
Uchumba wa muda mrefu sio mzuri na una madhara mengi mengi huku ukiwa hauna faida.
Hivyo sasa ni heri Mtu anapochukua maamuzi ya kuwa na mchumba basi iwe ni wakati yuko tayari pia kufunga ndoa miezi michache inayofuata.
Mimi Peter Mabula naamini unaweza kumchunguza mtu kwa miezi michache kama anakufaa na ukiridhika naye kabla ya kumweleza basi unamweleza.
✓✓Kuna watu walichunguzana kwa miaka 6 lakini ndoa yao haikudumu hata mwaka wakaachana.
Ndugu ni heri ukijiridhishe tu kwamba ni MUNGU amekupa huyo, ukiridhika hivyo basi anzisha uchumba na baada ya muda mfunge ndoa.
Leo kuna watu wanateseka sana kwa sababu wameingia katika uchumba na watu ambao hawako tayari kufunga ndoa wakati huo hivyo mnajikuta wewe unataka mfunge ndoa huku mchumba wako hataki na hayuko tayari, sasa huo ni uchumba gani?
Sasa kama mtu anaanzisha uchumba harafu hayuko tayari kwa ndoa, uchumba huo ni wa nini kwake?
Ndugu inawezekana ndio wewe, unamtesa mchumba wako maana yeye anataka mfunge ndoa huku wewe hauko tayari kufunga ndoa.
Ndugu mmoja siku moja alinipigia simu akisema "Mtumishi Mabula, mimi nina mchumba muda mrefu, sasa naomba uniombee ili nianze masomo na kisha nikipata kazi tuoane" Nikamuuliza unasoma muda gani? Akasema miaka miwili lakini baada ya hapo nikipata kazi basi hata nikifanya kazi miaka miwili tena basi tutaoana.
Hawa ndio baadhi ya aina ya wachumba katika ulimwengu wa leo.
Ndugu anza uchumba na mtu kipindi tu uko tayari kwa ndoa.
Asante kwa kila mmoja ambaye ni mhusika anasoma somo hili, roho yangu sasa ina amani.
MUNGU akukumbuke na kukusaidia ili uiendee ndoa takatifu yenye upendo na furaha ya kudumu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji, whatsapp n.m).
Ubarikiwe.

Comments