MAOMBI YA KUMSIHI MUNGU.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi.

 MUNGU amenipa neema ya kufafanua kidogo kuhusu maombi ya kusihi.

2 Nyakati 6:40 "Na sasa, Ee MUNGU wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa."

Tuanze na Neno kusihi lina maana gani?

✓✓Kusihi ni kuongea na mtu kwa namna ya tofauti ili akubali kutimiza jambo ambalo hataki kulifanya au hataki kulifanya kwa uharaka.

Kumsihi MUNGU ni nini?

1. Kumsihi MUNGU ni kumuomba MUNGU ukitaka akubali kutimiza haki yako inayothibitishwa na Neno lake , iliyokuwa imeshikiliwa na maadui zako kwenye ulimwengu wa roho.

2. Kumsihi MUNGU  ni kumwambia MUNGU kipekee ili kwa neema yake tu akutendee muujiza ambapo maamuzi mabaya kuhusu wewe yameshatolewa tayari.

Yaani unamsihi MUNGU atengue hukumu ambayo tayari imeshatolewa tayari.

Mfano Hezekia ambaye siku zake za kuishi duniani zilikuwa zimekoma ila akamsihi MUNGU ili MUNGU afute mpango wa kwanza wa kumuondoa Hezekia duniani na sasa MUNGU ampe neema mpya ya kuishi.

Ni kweli MUNGU akamsikia Hezekia katika maombi yake ya kusihi, MUNGU akamuongezea miaka 15 ya kuishi.

2 Wafalme 20:3 "Nakusihi, BWANA, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana."

Yapo mambo mengi inawezekana unatakiwa umsihi MUNGU.

✓✓Katika maombi kuna  maombi  ya kumsihi MUNGU.

✓✓Kuna maombi ya vita yaani maombi ya kutumia mamlaka ya KRISTO iliyo ndani yako ili kuamuru nguvu za giza ziachie au kuamuru jambo fulani litokee, hayo ndio kwa jina lingine yanaitwa maombi ya vita.

✓✓Kuna maombi ya kutumia jina la YESU KRISTO  ukizungumza na tatizo ili liondoke na kweli linaondoka.

Kiunganishi cha maombi yote ni kuomba katika ROHO MTAKATIFU na katika jina la YESU KRISTO.

Sasa kama wateule wa KRISTO inatupasa kuomba katika ROHO MTAKATIFU.

Yuda 1:20 "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,"

◼️Kuna wakati ROHO MTAKATIFU anakupa kukemea lakini kuna wakati ROHO MTAKATIFU anakupa kusihi, yote ni maombi muhimu sana.

Siku moja nilikuwa katika vita kubwa ya kiroho na nilitamani niombe maombi ya vita ili kuzikomesha nguvu za giza lakini nilipooanza kuomba nilishangaa rohoni sipewi kukemea bali napewa kuzungumza na MUNGU. Yaani badala ya kukemea nguvu za giza nikapewa kumsihi MUNGU na nikashangaa ushindi wa MUNGU baada ya kusikia maombi yangu ya kusihi, hicho kipigo  kwa nguvu za giza kikawa kikubwa kuliko hata ningekemea.

Kuna siku pia nilikuwa namsihi MUNGU lakini nilipoanza tu kumsihi MUNGU rohoni nikabadilishiwa maombi na kuanza kukemea nguvu za giza na matokeo yakawa makubwa sana.

Nini nataka kusema?

✓✓Ni kwamba maombi yote ni sahihi na ni maombi muhimu sana kama unaomba katika ROHO MTAKATIFU.

Maombi ya kusihi ni muhimu sana, maombi ya kuzungumza na tatizo kimamlaka  ili hilo tatizo  litoke ni muhimu, maombi ya kuamuru ni muhimu na maombi ya vita ni muhimu sana.

 ◼️Nakuomba usiwe mtu wa kuomba maombi ya aina moja tu bali msikilize ROHO MTAKATIFU katika maombi ili akusaidie namna ya kuomba kulingana na hitaji husika.

Kuna watu leo wanajua tu kuomba maombi ya vita kiasi kwamba wanakemea hata wanapoongea na MUNGU ndio maana hawajibiwi.

Kuna watu pia wanaomba tu maombi ya kusihi hata pale ambapo ROHO MTAKATIFU anataka wakemee wakitumia mamlaka ya jina la YESU KRISTO, watu hao hawapokei hata kama wamesihi muda mrefu.

◼️Ndugu, maombi yote ni muhimu sana ukiomba katika ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.

Inawezekana kabisa katika hitaji lako unatakiwa uombe maombi ya kumsihi MUNGU.
Inawezekana wachawi wanakutesa, ukimsihi MUNGU na akakuridhia maombi yako unaweza ukashangaa hao wachawi wanapata madhara wote hata kama wako mia.

Inawezekana umesingiziwa kesi , umehukumiwa ila umekata rufaa, kisha unamsihi Bwana YESU KRISTO akunusuru na jela, hayo ni maombi ya kusihi.

Inawezekana Mume wako anakufukuza kisha anamchukua rafiki yako ili awe mkewe badala yako, unaingia katika maombi ya kumsihi MUNGU.

✓✓Maombi ya kumsihi MUNGU ni moja ya maombi muhimu kama zilivyo aina nyingine za maombi.

Unaweza ukamsihi MUNGU katika maombi ya kawaida na unaweza ukamsihi MUNGU ukiwa katika maombi ya kufunga.

Maombi ya kumsihi MUNGU ni  maombi ya kuzungumza na MUNGU na  yana kauni zake pia.

Unapoomba maombi ya kusihi zingatia haya.

1. Usikemee maana huwezi kukemea ukiwa unaongea na MUNGU.

Yakobo 1:5 "Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa MUNGU, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa."

✓✓usikemee unapoomba maombi ya kuzungumza na MUNGU. 
Usikemee unapozungumza na MUNGU. 

2. Katika maombi hayo ongea na MUNGU tu.

Zaburi 118:25 "Ee BWANA, utuokoe, twakusihi; Ee BWANA, utufanikishe, twakusihi."

✓✓Katika maombi ya kusihi  usizungumze na tatizo, usizungumze na maadui zako, usizungumze na shida yako,  usizungumze na nguvu za giza,  usizungumze na kifungo chako bali zungumza na MUNGU kwa njia ya kumsihi  ili akushindie na utashinda  kwa jina la YESU KRISTO. 

3. Dai haki yako kwa MUNGU ukimkumbusha MUNGU kupitia Neno lake.

1 Wafalme 8:26 "Sasa, Ee MUNGU wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu."

Solomoni  hapa  anamsihi MUNGU huku akimkumbusha MUNGU juu ya Neno lake alilomwambia Daudi baba yake .

Hata wewe msihi MUNGU huku ukimkumbusha juu ya ahadi aliyokuambia kwa ndoto au maono au kwa ufunuo wa ROHO MTAKATIFU. 

Msihi MUNGU huku ukimkumbusha ahadi yake kwako ndani ya Biblia.  

4. Mweleze Bwana YESU akufanyie nini.

Marko 5:22-23 " Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake,
 akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi."

Yairo alimsihi Bwana YESU ili amponye binti yake na akaponywa. 

✓✓Bwana YESU hata leo yuko tayari kukuponya, kukutendea muujiza na kukujibu hitaji lako,  fanya kama Yairo kwa kumsihi Bwana YESU ili atende hitaji lako. 

5. Katika maombi ya kusihi tanguliza toba kuhusu wewe na tubu kuhusu chanzo cha tatizo unalotaka liondoke.

Waamuzi 10:15 "Wana wa Israeli wakamwambia BWANA Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu."

Inawezekana unafahamu aina nyingi za maombi, leo nakufundisha aina mojawapo ya maombi muhimu sana ambayo ni maombi ya kusihi.

Ndugu, pale unapopata nafasi ya kuomba maombi ya kumsihi MUNGU hakikisha unamsihi MUNGU kweli kweli na kwa kutumia neno lake na ahadi zake kwako.

Mfano ni kwamba ahadi ya MUNGU kwenye Neno lake ni kwamba wewe ufunge ndoa .

Mwanzo 2:24 "Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja."  kama imeshindikana kwa maombi mengine basi leo msihi MUNGU kwamba akupe mwenzi wa ndoa kama ahadi ya MUNGU katika Neno lake inavyosema.

✓✓Kumbuka MUNGU huliangalia Neno lake ili alitimize.
Yeremia 1:12 "Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize."

✓✓ Na Neno la MUNGU huwa halimrudii MUNGU bure.
Isaya 55:11 "ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma." Hivyo penda sana kuomba ukitumia Neno la MUNGU na ahadi za MUNGU kulingana na mahitaji yako.

Ahadi ya MUNGU ni kwamba wewe uwe kichwa na sio mkia yaani uwe mshindi na sio mshindwa.

Kumbu  28:13 "BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;" 

Basi kwanini wachawi wanachezea akili zako hadi umekuwa mtu wa kufeli tu bila sababu? 

✓✓Basi unaweza kumsihi MUNGU ukimuomba akufanye kuwa kichwa na sio mkia katika masomo yako.

✓✓Ahadi ya MUNGU ni kukulinda kama unamtegemea katika KRISTO YESU na unaishi maisha matakatifu.

Isaya 26:3 "Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini."

✓✓Hivyo kama maadui wanakutisha unaweza kumsihi MUNGU ukimkumbusha ahadi yake ya kukulinda kwa sababu tu unamwamini na unamtegemea yeye.

✓✓Ahadi ya MUNGU ni kuzaa na kuongezeka.

Mwanzo 1:28 "MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."

✓✓Hivyo unaweza kumsihi MUNGU akupe uwezo wa kuzaa na kuongezeka.
Ndugu  inawezekana umedhulumiwa haki zako, msihi MUNGU maana kumsihi MUNGU kunaweza kutatua tatizo lako hata kama tatizo ni kubwa kiasi gani.

Inawezekana unaumwa sana, inawezekana uko katika vita kubwa sana ya kiroho n.k

Kumsihi MUNGU kuna maana sana, unaweza ukashinda kirahisi sana.

Ngoja nikuonyesha baadhi ya watumishi  wa MUNGU katika Biblia walioomba maombi ya kumsihi MUNGU  naye MUNGU akafanya mambo makubwa sana kwao.

1. Akida alimsihi Bwana YESU aponye na akaponya. 

Mathayo 8:5-8,13 "Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia,
  AKAMSIHI, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. YESU akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. .....  Naye YESU akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile."

2. Danieli alimsihi MUNGU  akapona kufa mbele za simba wakali wenye njaa kali.

Danieli 6:11,16,22 " Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danielii akiomba dua, na KUSIHI mbele za MUNGU wake. .....  Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danielii, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danielii, MUNGU wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. ...... MUNGU wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno."

3. Elisha alimsihi MUNGU awapige upofu maadui zake na ikawa hivyo hhivyo.

2 Wafalme 6:18 "Na walipomtelemkia Elisha akamwomba BWANA, akasema, Uwapige, NAKUSIHI, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha."

4. Kwa kusihi Musa alimuombea Miriamu ili aponywe ukoma akaponywa. 

Hesabu 12:13 "Musa akamlilia BWANA, akasema, Mpoze, Ee MUNGU, NAKUSIHI sana."

5. Eliya alimsihi MUNGU afufue mtoto na MUNGU kweli akamfufua mtoto huyo.

1 Wafalme 17:21-22 " Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, NAKUSIHI, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena.  BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka."

Mimi Peter Mabula Naamini ni zamu yako rafiki yangu  leo kumsihi MUNGU kwa ajili ya mahitaji yako na MUNGU atakutendea muujiza unaouhitaji.

Kumbuka Musa alimsihi MUNGU kwa ajili ya Waisraeli 

Hesabu 14:19 "Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa."

leo ni zamu yako kumsihhi MUNGU katika KRISTO YESU na utafanikiwa sawasawa na maombi yako.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri n.k).
Ubarikiwe 

Comments