![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
✓✓Mambo haya hapa chini yanaweza kumuunganisha Mtu na Madhabahu za giza yaani Madhabahu za kishetani.
◼️Lengo la ujumbe huu ni Wewe ujue ili hata siku Moja usije ukanaswa kwenye kujiunganisha na Madhabahu za giza na Madhabahu za kishetani kwa Jina lingine.
✓✓Madhabahu za giza hazitakiwi kuhusika na Wewe kamwe.
Madhabahu za giza ni chanzo kikuu Cha mabaya mengi kwa watu wengi hivyo Jifunze Neno la YESU ili ujitenge daima na Madhabahu za giza.
Mambo 7 yanayoweza kumuunganisha Mtu na Madhabahu za giza.
1. Sadaka uliyotoa kwa waganga wa kienyeji au kwa makuhani wa kipepo wengine wote. Au sadaka walizotoa wazazi wako au watu kwa mawakala wa shetani huku na wewe ukihusishwa.
Zaburi 106:37 "Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani."
◼️Biblia inasema hawa walitoa Sadaka zao kwa mashetani na Kwa njia hiyo walikuwa wamewaunganisha na Watoto wao kwa mashetani kupitia Sadaka, ni kitu kibaya sana ambacho kingetesa hadi kizazi Chao.
Ndugu Watumishi wa Bwana YESU wanapokukataza kwenda kwa Waganga wa kienyeji ni kwa faida Yako maana kwa waganga unaweza hata kuunganisha na Watoto wako kwa shetani.
1 Wakorintho 10:20 "Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa MUNGU; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha BWANA na kikombe cha mashetani."
Biblia inaonyesha kwamba wako watu walitoa Sadaka kwa shetani, ni jambo la hatari sana.
◼️Tangu zamani MUNGU wa Mbinguni anaonya Watu wake wasije wakatoa sadaka kwa miungu.
Ukitoa sadaka kwa miungu maana yake umetoa sadaka kwa shetani hivyo utakuwa umeingia Agano la kipepo na shetani.
Kutoka 34:15 "Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake."
◼️Biblia kwa habari ya Utoaji Sadaka au Zaka inakutaka utoe kule ambako MUNGU katika KRISTO YESU Yuko.
Kumbu 12:11 "wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa BWANA."
✓✓Usitoe Sadaka zako na Zaka zako sehemu ambayo huna uhakika kama MUNGU wa Mbinguni Yuko.
✓✓Usitoe sehemu ambako YESU KRISTO hayuko.
Kama YESU huko hayuko ujue Yuko shetani na majini yake ambayo kwa sadaka Yako yataanza kukutesa.
✓✓Usitoe sehemu ambako ROHO MTAKATIFU hayuko.
2. Jina lenye uhusiano na nguvu za giza.
Mithali 22:1 "Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu."
◼️Jina ni kitu Cha thamani sana.
Jina ndio utambulisho wa kipekee unaokutofautisha Wewe na wengine.
Biblia inakutaka uchague Jina jema kuita kila Mtoto wako.
✓✓Sasa yapo majina ambayo yana muunganiko na nguvu za giza kwa sababu ya watoaji wa majina hayo.
Mfano Jina la Mtoto ametoa Bibi na ni mchawi na anajua kwanini anatoa Jina hilo.
✓✓Majina ya kurithi yaliyounganishwa na nguvu za giza.
✓✓Majina ambayo ili mumpe Mtoto inabidi kwanza wazee waulize kwa mizimu, yaani Jina limetokana na mizimu ndio unampa Mtoto.
Mfano hai ni Mtu aliitwa Ethbaali katika andiko hapa chini, maana ya Ethbaali ni kuhani wa Baali, na Kumbuka Baali ni shetani.
Mtu wa namna hiyo lazima aje awe Mtumishi wa Shetani kwa sababu ya maana ya Jina lake kuunganishwa na shetani.
1 Wafalme 16:31" Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia."
Huyu Ethbaali alikuwa Mtumishi wa Shetani kama Jina lake lilivyo na akawafundisha hadi Watoto wake akina Yezebeli kuwa Watumishi wa shetani, Jina Lina Nguvu sana.
◼️Ndugu, ushauri wangu kwako ili kujitenga mbali na majina yaliounganika na nguvu za giza it's Watoto wako majina mema yaliyo katika Biblia.
✓✓Yaani hakikisha chanzo Cha Jina lako au la Mtoto wako ni Biblia Takatifu.
3. Viapo au nadhiri za kipepo.
Habakuki 3:9 "Uta wako ukafanywa wazi kabisa; Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti; Ukaipasua nchi kwa mito."
✓✓Biblia inasema viapo walivyopewa kabila fulani vilikuwa neno thabiti, je kama vilikuwa viapo vibaya vilivyofanyika kwenye Madhabahu za giza ingekuwaje?
◼️Maana yake kabila lile wangetembea chini ya Nguvu za Giza.
✓✓Viapo ni aina fulani ya Nadhiri na kazi ya Nadhiri ni kudai ili yaliyotamkwa yatimie, vipi kama ni viapo vibaya?
Uwe na uhakika itakuwa hivyo hivyo.
Ingawa sio Nadhiri zote ni viapo.
Wako watu kwa sababu ya Hasira au kwa sababu ya kutokujua au kwa sababu ya kuhitaji msaada hujikuta wamefanya viapo vya kipepo.
Bibi mmoja asiye na YESU siku Moja aliapa kwa mganga wa kienyeji kwamba Binti akizaa Mtoto wa kike, huyo Mtoto atarithi mikoba yake. Yaani Bibi kwa kiapo anamkabidhi mjukuu wake mambo ya kichawi. Mtoto huyu katika Maisha yake kabla hajaokoka alikuwa anateswa sana na Nguvu za giza wakidai wanamtambua ni malikia wao hivyo hatakiwi kukwepa majukumu ya kipepo.
Viapo vya kipepo vitayafanya mapepo yawe na uhalali na wahusika.
YESU KRISTO Mwokozi anakataza mambo ya kiapo kama hujui unaapa nini na kwa nani.
Mathayo 5:34" lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha MUNGU;"
4. Maagano ya kipepo ya kabla yako au baaada ya wewe kuwa umezaliwa.
Isaya 28:15 "Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;"
✓✓Agano na mauti litaleta roho za mauti.
roho za mauti ni Nguvu za giza ambazo zitamtesa Mtu Kwa sababu ya Agano
✓✓Agano au patano lolote na kuzimu litaleta Nguvu za giza ambazo hutoka kuzimu zije kwenye Maisha ya Mtu husika.
◼️Ndugu, katika maisha Yako Usikubali kamwe kufanya Agano lolote la kishetani.
◼️Agano la kishetani litaleta Nguvu za giza kwenye Maisha Yako hivyo Usikubali kamwe kufanya Agano lolote la kipepo.
Usifanye Agano na Mawakala wa Shetani wa aina yeyote.
◼️Kama hujaokoka Nakuomba okoka Leo ili maagano ya kishetani yasikufuatilie Tena. Mkimbilie YESU KRISTO Mwokozi utakuwa huru kabisa, mbali na maagano ya kishetani.
Yohana 8:36 "Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli."
5. Kuishi eneo ambalo limetawaliwa na miungu na wewe hujui namna ya kujitenga na nguvu za giza.
Waamuzi 2:11-12 " Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika."
◾Biblia inasema Watu hawa walijiunganisha na miungu ya watu waliokuwa Karibu yao hivyo wakamkasirisha MUNGU wa Mbinguni.
✓✓Hawa walikaa eneo ambalo linatawaliwa na nguvu za giza wakajikuta wamenaswa wakamsahau MUNGU wa Mbinguni.
✓✓Ndugu, ikiwa unaishi eneo ambalo linatawaliwa na dini zilizo kinyume na KRISTO YESU ujue eneo hilo Madhabahu za giza ni nyingi, Usikubali kamwe kunaswa na Madhabahu za giza.
6. Kuiabudu au kuitumikia au kuifuata miungu.
Kutoka 23:13 "Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako."
◼️MUNGU wa Mbinguni anawakataza Wanadamu wote kuiabudu miungu, kuitumikia Wala kuifuata.
✓✓kwanini?
Kwa sababu Kuabudu miungu ni kujiunganisha na nguvu za giza.
◼️Miungu ni dini zote zilizo kinyume na Wokovu wa KRISTO YESU.
◼️Ndugu Hakikisha unamwabudu MUNGU wa Mbinguni ambaye amejifunua katika KRISTO YESU pekee.
◼️ Ondoa miungu kwenye Maisha Yako, Anza kumtumikia MUNGU wa Mbinguni katika KRISTO YESU.
1 Samweli 7:4 "Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake."
7. Kuwa na madhabahu za giza za ukoo, familia au kabila.
Waamuzi 6:25 "Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;"
◼️Andiko hili linaonyesha mambo mengi yakiwemo Madhabahu ya shetani ya familia maana ilikuwa ndani ya familia.
◼️ Madhabahu ya shetani ya Ukoo maana Wana ukoo walikuwa wanakuja kuabudu miungu hapo.
◼️ Madhabahu ya shetani ya Mji maana watu wa Mji ule walikuwa wanakusanyika kuabudu miungu hapo.
✓✓Kujihusisha Kwa namna yeyote kuabudu miungu ni kukaribisha Nguvu za giza kwako.
Ndio maana MUNGU wa Mbinguni kwa kuwasaidia hawa akamwambia Gideon aivunje Madhabahu hiyo ya shetani.
Gharama za kiroho za kiroho za kuangusha Madhabahu za giza huhusisha Sadaka ndio maana Gideon akaambiwa na MUNGU atoe Sadaka katika kuivunja ya shetani.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ushauri, Maombezi, Whatsapp n.k)
Share ujumbe huu kwenye magroup ya Whatsapp uliyopo.
Ubarikiwe

Comments