![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. Pichani Mwl Peter Mabula akiwa na Watumishi wenzake katika Kanisa la Kawe Pentecostal Church(KPC) Mwaka 2013 |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Namshukuru MUNGU kwa neema yake kwangu na uzima wake.
◼️Ninachotaka kukuambia ni kwamba usisahau kuwaombewa watumishi wa MUNGU ambao MUNGU amewapa Neno kwa ajili yako, hata kama ni Mimi nimewahi kukubariki kwa Neno la MUNGU angalau Mara moja tu nakuomba usisahau kuniombea, kumbuka shetani kufuatilia chanzo cha kuleta maarifa ya ushindi ili akifanye chanzo hicho kisilete Neno la MUNGU.
✓✓Ndio maana Mtume Paulo ingawa alikuwa na Upako sana au Nguvu za ROHO MTAKATIFU sana lakini hakuacha kuwaambia Kanisa ili wamuombee katika Maombi yao.
Wakolosai 4:3 "mkituombea na sisi pia, kwamba MUNGU atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya KRISTO, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,"
Yawezekana hujaelewa.
Ngoja nikupe ushuhuda wangu binafsi Mimi Peter Mabula ili uone vita ya Watumishi ili upate mzigo wa kuwaombea.
Nakumbuka kwa miaka hii 13 tangu mwaka 2012 ambayo nimekuwa nikiandika masomo ya Neno la MUNGU, MUNGU amenipa neema hadi leo ni zaidi ya masomo 1400 nimefundisha, sio kazi rahisi hata kidogo na adui hataki kuona Neno la MUNGU linamsaidia mtu au linamfanya mtu anafunguliwa.
Nakumbuka kwa miaka hii 13 nimetumia computer 7 na kwa sababu adui hakutaka computer 5 ziliharibika vibaya ghafla .
Computer ya kwanza iliungua ghafla hakukuwa na namna ya kutengenezeka, computer ya pili na ya tatu na ziliharibika vibaya sana hata hazikuweza kufanya kazi.
Hata computer ya nne nayo adui hakutaka neno liwafikie watu ikaharibika vibaya bila kuguswa, computer ya tano nayo iliharibika ghafla tu.
Katika maombi niliona siku moja nguvu za giza zikirusha vitu ndani ya computer yangu ili isifanye kazi.
Kwanini ninasema haya?
◼️Usisahau kuwaombea Watumishi wa MUNGU ambao ROHO MTAKATIFU anawapa Neno kwa ajili Yako.
◼️Usiwasahau Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO ambao unapojifunza Neno wanalofundisha unajulishwa rohoni ni Neno kwa ajili Yako.
Kwanini nimesema unatakiwa kuwaombea watumishi waaminifu wa MUNGU katika KRISTO YESU?
◼️Sababu ni hizi;
1. Adui hutaka kumpiga Mchungaji(anayetoa huduma ya Neno la MUNGU) ili kondoo(Watu wa MUNGU) wasipate tena Neno la kuwasaidia.
Mathayo 26:31 "Ndipo YESU akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika."
2. Adui huzuia Neno la MUNGU ili lisiwafikie watu wakafunguliwa.
1 Wathesalonike 2:18 "Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia."
3. Adui hufunga milango ili Neno la KRISTO lisisambae zaidi likawasaidia wengi.
Wakolosai 4:2-4 " Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba MUNGU atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya KRISTO, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena."
4. Mawakala wa shetani hufanya vita kubwa na watumishi wa MUNGU ili kuwanyamazisha.
Yeremia 18:18 "Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote."
5. Watumishi wa MUNGU hupingwa na maadui wengi.
1 Wakorintho 16:9 "kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao."
◼️Kwa ajili ya hilo inakupasa sana kuombewa Watumishi wa MUNGU waaminifu ili wamshinde shetani anayewazuia kuisema kweli ya KRISTO.
✓✓Kumbuka MUNGU hulituma Neno ili likuponye na likutoe kwenye maangamizo, Zaburi 107:20 "Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao."
◼️Sasa Neno litaletwa na MUNGU kupitia Mtumishi aliyebeba kusudi kwa ajili yako ili upone na utoke kwenye maangamizo, sasa akizuilika huyo Mtumishi ujue hutapona na hutatoka kwenye maangamizo, unahitaji sana kuwaombea Watumishi wa Bwana YESU KRISTO walio wa kweli ili wasizuilike.
✓✓Mtumishi anaweza kupitia mazingira magumu sana lakini akiwa anakufundisha au kukuombea unaweza usijue kama yuko katika mazingira magumu.
Biblia inasema mambo haya kuhusu Mtumishi.
2 Wakorintho 6:4-10 " bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa MUNGU; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika ROHO MTAKATIFU, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya MUNGU; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa; kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote."
✓✓Mtumishi anaweza kunenewa mabaya, kuzushiwa uongo n.k
✓✓Mtumishi anaweza kutajirisha wengi kwa kuwaombea, kuwatamkia baraka na kuwafundisha Neno la MUNGU.
Hata kama yeye kwa wakati huo hana hizo baraka.
◼️Unahitaji sana kuwaombea watumishi wa MUNGU waaminifu.
Hata Mimi nahitaji maombi yako sana sana.
✓✓Kuna wakati huwa natamani kutafuta kundi la watu la Maombi ambao Mimi nitakuwa nawaombea na wao wananiombea na kuombea huduma yangu.
✓✓Ni rahisi sana kuona mtumishi akiombea watu wengi sana na MUNGU anawatendea watu hao lakini ni ngumu kumuona mtu amefunga na kuomba ili kumuombea Mtumishi wa MUNGU.
◼️Maombi kwa watumishi yanahitajika sana sana.
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments