![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Tunafahamu baada ya shetani kuwadanganya Wanadamu wa kwanza ilipelekea Wanadamu hao kufukuzwa katika bustani ya MUNGU, ilipelekea pia kuzaa kwa uchungu na ilipelekea pia kuanza kula kwa jasho.
Yaani utavipata vitu kwa kuvitolea jasho au kwa kufanya kazi.
Mwanzo 3:16-17 " Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;"
◼️Lakini jambo Muhimu zaidi kujua ni kwamba Wanadamu wote na katika Vizazi vyao vyote wana uadui na shetani milele.
Mwanzo 3:15 "nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino."
✓✓Uadui huu kati ya Wanadamu na shetani umewekwa na MUNGU Mwenyewe.
Matokeo yake ni kwamba.
1. Shetani ni wa kumpinga daima na sio kumkumbatia.
Yakobo 4:7 "Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia."
2. Shetani ni miungu hivyo haitakiwi kumwabudu.
Kutoka 20:3 "Usiwe na miungu mingine ila mimi.'
◾Usije ukathubutu kamwe kumwabudu shetani.
3. Shetani ni muongo daima na Kila asemacho Lengo ni kumpotosha Mwanadamu.
Yohana 8:44 'Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.''
✔️ Usikubali uongo wa shetani kwa namna yeyote ile?
4. Bwana YESU KRISTO alikuja ili aziharibu kazi zote za shetani hivyo ungana na Bwana YESU KRISTO awe Mwokozi wako ili ushiriki kuziharibu kazi za shetani katika jamii.
1 Yohana 3:8 "atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi."
5. Shetani amejaribu kuleta Ibada za sanamu nyingi ili kuwe na urafiki katika yake na baadhi ya Wanadamu wajinga, Ndugu Hakikisha sio Wewe unayeshiriki Ibada za sanamu.
1 Wakorintho 10:14 "Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.''
6. Shetani ana mbinu nyingi ili kuwatenga Wanadamu na MUNGU, Ndugu unapomgundua shetani jitenge naye mbali.
2 Wakorintho 11:14 "Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru."
7. Mwisho wa shetani na Malaika zake ni jehanamu hivyo Usikubali kuungana nao huko.
Ufunuo 20:10 "Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele."
◼️Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako ili utengane na shetani milele.
◼️Weka akilini mwako kwamba Kuna uadui wa kudumu kati ya Wanadamu na shetani hivyo usimpe nafasi shetani katika Maisha Yako kwa namna yeyote ile na kwa eneo lolote lile la Maisha Yako.
✓✓Kamwe usimpe nafasi shetani katika Maisha Yako yote.
Waefeso 4:27 "wala msimpe Ibilisi nafasi."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments