MATOKEO 4 YA KUMTEGEMEA MUNGU DHIDI YA ADUI ZAKO AU JUU YA TATIZO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

Yeremia 17:7 "Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake."

◼️Kuna faida za ajabu katika kumtegemea MUNGU katika KRISTO YESU.

Zaburi 71:6 "Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima.'

◼️Kuna Neema ya ajabu ya ushindi ukichagua kumtegemea MUNGU katika KRISTO YESU.

◼️Kuna ushindi mkubwa mbele ya adui zako wenye Nguvu sana kama ukiamua tu kumtegemea Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Mfano  hai ni huu
2  Nyakati 16:8 "Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? Lakini, kwa kuwa ulimtegemea BWANA, aliwatia mkononi mwako."

Hawa Wakushi na Walubi walikuwa na nguvu sana na walikuwa na majeshi yenye zana nzito za kivita ili kuwapiga Israel lakini Israel walishinda bila Nguvu kubwa ya kijeshi kwa sababu tu walimtegemea MUNGU wa Mbinguni.
Hata Mimi Peter Mabula nakuambia rafiki yangu unayesoma somo kwamba ukiamua kumtegemea Bwana YESU KRISTO utawashinda wachawi na watu wabaya wote hata kama wana Nguvu kubwa sana kwa Sasa.
Hao wana Nguvu kwako na sio kwa MUNGU hivyo mtegemee MUNGU mwenye Nguvu utashinda kwa Jina la YESU KRISTO Mwokozi.

✓✓Kama hujawahi kuwa na akili ya kumtegemea MUNGU wa Mbinguni nakuomba kuanzia Leo tubu Kisha Anza kumtegemea.

Matokeo ya kumtegemea MUNGU wa Mbinguni.

1. MUNGU kukutoa kwenye eneo la tatizo na kukuponya dhidi ya tatizo.

2 Samweli 22:19-21 " Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa."

2. Unaopigana nao MUNGU atawafanya wakuogope hata bila kujua kwanini wanakuogopa.

2 Nyakati 13:18 "Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea BWANA, Mungu wa baba zao."

3. MUNGU kuwapiga adui zako kwa sababu umemtegemea.

2 Mambo ya Nyakati 14:11-14 " Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe MUNGU wetu, asikushinde mwanadamu. Basi, BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia. Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; nao wengi wakaanguka wa Wakushi hata wasiweze kupona; kwa sababu waliangamizwa mbele za BWANA, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka mengi sana."

 4. MUNGU atakulinda dhidi ya adui zako hata kama wana Nguvu sana.

Isaya 26:3-4 "Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele."

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments