MIUNGU MIGENI KATIKA MIILI.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU, Inawezekana sio Kila Mtu atabarikiwa na Chakula Cha kiroho Cha Leo ila kwa sababu ni Neno la MUNGU wa Mbinguni fanyia kazi.

Ukisoma Mwanzo 35:2-4 unaona Yakobo akiwaambia watu wa familia yake waondoe miungu migeni iliyo katika miili yao.

✓✓Miungu hiyo migeni imetajwa majina ambayo ni baadhi ya  vitu vya kuvaa mikononi na vile vya masikioni.
Vitu vya kuvaa masikioni  Biblia ya BHN imeita "Sanamu za miungu ya kigeni" 

Huwa najiuliza sana je kiroho kulikuwa na Nini nyuma ya hereni za masikioni hadi zikasababisha zitumike kutengenezwa sanamu ya ndama ya kuabudiwa wakati wa safari ya Waisraeli hadi MUNGU akataka kuwaangamiza?

✓✓Kulikuwa na nguvu nyingine nyuma ya hereni hizo za masikioni.

Ukisoma Kutoka 33:5 MUNGU anawaambia Waisraeli wavue mapambo?

◼️Je Leo sio makosa kuvaa hayo mapambo aliyokataza MUNGU?

Je kwanini Shanga, heleni na vitu vya kuvaa mikononi viitwe miungu?
◼️Ni kwa sababu vimetokana na miungu na sio MUNGU wa Mbinguni.

✓✓Hata ukifanya uchunguzi Leo watengenezaji wengi wa vitu hivyo ni wapinga KRISTO.

Najua ujumbe huu ni mgeni kwa mamilioni ya Wanawake wavaa heleni, shanga, vikuu, kutoboa pua lakini kama ROHO MTAKATIFU akisema na Wewe kupitia ujumbe huu fanyia kazi.

Najua ujumbe huu ni mgeni masikioni mwa Wanaume wanaovaa hereni na kuvaa mapete mengi ya kichawi lakini ni saa ya kubadilika kama unataka kumpendeza MUNGU wa Mbinguni.

✓✓Ushauri wangu vaa mkononi saa tu maana hiyo ni kwa ajili ya kuangalia muda.

✓✓Ushauri wangu usivae kitu chochote shingoni Wala masikioni popote na siku zote.

Yakobo alipozingatia kuhakikisha familia yake wameondoa miungu migeni mambo haya yalitokea baada ya hapo.

1. Baada ya tukio la Yakobo kuondoa miungu migeni katika miili ya familia yake MUNGU alimtokea.

Mwanzo 35:9 "MUNGU akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki."

2.Baada ya tukio hilo la kuondoa miungu migeni Yakobo alibadilishwa Jina na kuitwa Israeli.

Mwanzo 35:10" MUNGU akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli."

3. Baada ya tukio hilo la kuondoa miungu migeni Yakobo alibarikiwa na MUNGU.

Mwanzo 35:11-13 " MUNGU akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako. Na nchi hii niliyowapa Ibrahimu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo. MUNGU akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye."

✓✓Ndugu, kama Biblia imeita mapambo kuwa miungu migeni ujue ni kweli ni miungu migeni, jitenge na miungu migeni kuanzia Leo ukiisikia Sauti ya MUNGU kupitia somo hili.

Najua nakufundisha ujumbe mzuri sana Leo ila umekuwa ujumbe mgumu sana kwako kwa sababu tangu umezaliwa, ulipopata akili ulikuta wazazi wako wameshakutoboa masikio tayari na kukuunganisha na maroho yaliyo nyuma ya heleni hizo ndio maana kuelewa katika majira haya na vigumu sana.

Najua Kuna watu unawaheshimu sana na wao huvaa kila siku hiyo miungu migeni lakini kama miungu migeni hiyo sio mpango wa MUNGU basi chagua kumtii MUNGU wa Mbinguni.

◼️Sijasema vitu hivyo ni dhambi ya Moja kwa Moja ila kama MUNGU alikataza basi ni vyema kumtii MUNGU na sio Wanadamu.

✓✓Wakati Yakobo anaondoa miungu migeni hata Torati ilikuwa haijaanza hivyo usidanganywe kwamba labda katazo hili ni la torati, Ndugu sio torati.

✓✓Fanya hata utafiti hata Leo utashangaa wanaouza shanga ni jamii ya wapagani na waabudu miungu, huwezi kumkuta Mtu aliyeokolewa na Bwana YESU KRISTO na ana ROHO MTAKATIFU anauza shanga, shanga ni miungu migeni iliyotokana na shetani.

✓✓Ndio maana Biblia inakataza hata kuvaa vikuku, lulu za dhahabu katika miili na inawataka watu wasipendelee vitu hivyo.

1 Timotheo 2:9 "Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;"

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments