![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ukisoma Kutoka 2:24 unagundua mambo kadhaa, jambo mojawapo Muhimu sana katika hayo kwenye andiko hilo ni MUNGU kukumbuka agano lake na Ibrahimu.
Kutoka 2:24" MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo."
◾Inawezekana agano hili Ibrahimu aliliona la kawaida tu lakini mbele za MUNGU lilikuwa agano kubwa na ambao MUNGU alikuja kulikumbuka Baadae na Agano hilo likasababisha baraka kuu kwa uzao wa Ibrahimu.
Sasa ni mambo gani yalitokea baada ya MUNGU kulikumbuka Agano lake na Ibrahimu au ni mambo gani yaliambatana baada ya Agano hilo kukumbuka?
1. MUNGU alipokumbuka Agano hilo aliwaona Waisraeli ambao wametokana na Ibrahimu.
Kutoka 2:25" MUNGU akawaona wana wa Israeli, na MUNGU akawaangalia."
◼️Kuwaangalia huku hakukuwa kwa kawaida, MUNGU alipowaangalia Waisraeli alipanga mambo mengi mazuri juu yao na aliyatimiza.
2. MUNGU alipokumbuka Agano hilo alimwinua Musa ili awe kiongozi kuwatoa Waisraeli Misri.
Kutoka 3:4-5,10 "BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, MUNGU akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri."
✓✓Hii ilikuwa faida kwa Waisraeli kwa sababu ya Agano la MUNGU na Ibrahimu.
✓✓Vipi Bwana YESU KRISTO akikumbuka Agano ulilofanya kwa MUNGU na akainua watu kwa ajili Yako katika unachohitaji?
Ngoja nikupe ushuhuda mfupi juu ya MUNGU kumwinua Mtu kwa ajili Yako.
Siku Moja Mimi Peter Mabula nilikuwa katika wakati mgumu sana kifedha, nilikuwa na uhitaji mkubwa sana na nilikosa tumaini lakini siku hiyo hiyo jioni Kuna Mtu akanitumia Tsh 350,000 akisema amekosa amani muda mrefu akihimizwa rohoni anitumie kama Sadaka, alipotuma ndipo amani ikaja. Nilimshangaa MUNGU na nilicheka rohoni kwa fulani.
Mtu huyu Wala hakujua kama Nina uhitaji na Wala sikumuomba lakini yeye mwenyewe bila ushawishi wowote wa kibinadamu aliinuliwa na MUNGU kwa ajili Yangu ili nifanikiwe na nikafanikiwa.
Sasa vipi MUNGU akikuinulia watu 10 kwa sababu tu amekumbuka Agano ulilofanya miaka iliyopita?
Hakika ni jambo jema.
✓✓MUNGU alipokumbuka Agano na Ibrahimu alifanya mambo mengi mojawapo kuwainuliwa Waisraeli watu wa kuwasaidia kama akina Musa.
3. MUNGU alijitambulisha kama MUNGU wa Ibrahimu.
Kutoka 3:15 "Tena MUNGU akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, MUNGU wa Ibrahimu, MUNGU wa Isaka, MUNGU wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote."
◼️Ni kawaida Mtu kusema MUNGU wa Mbinguni ni MUNGU wake lakini ni jambo kubwa mno na lililobeba mambo mengi MUNGU Mwenyewe kusema ni MUNGU wa Mtu fulani.
Kwangu Mimi ni watu 4 tu ambao MUNGU alijifunua kwangu kama MUNGU wao, ila kukuondolea maswali moyoni ngoja nikutajie watu hao maana MUNGU wa Mbinguni alijifunua kwangu kama MUNGU wao, ni Askofu Moses Kulola, Mwl Christopher Mwakasege, Askofu Josephat Gwajima na Mchungaji Elly Botto, haina maana kwamba ni hao tu kwa Tanzania nzima ila ni hao nilifunuliwa Mimi binafsi kulingana na kile MUNGU alikuwa ananifundusha, kunipa uhakika na ili nijijue katika wito, Naamini hata Wewe umefunuliwa kulingana na mazingira Yako au kulingana na kile ROHO MTAKATIFU alitaka kukufundisha. Mimi Naamini Kuna mamia elfu ya Watumishi wa KRISTO ambao MUNGU alijifunua kwa baadhi ya watu kwamba yeye ni MUNGU wa hao Watumishi.
✓✓Ni jambo kubwa mno Tena limebeba mengi MUNGU Mwenyewe kusema yeye ni MUNGU wa fulani.
Ilitokea kwa Waisraeli MUNGU akasema ni MUNGU wa Ibrahimu.
Kutoka 3:6 "Tena akasema, Mimi ni MUNGU wa baba yako, MUNGU wa Ibrahimu, MUNGU wa Isaka, na MUNGU wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia MUNGU."
4. MUNGU alimwandaa Haruni ili kumsaidia Musa kwa faida ya Waisraeli.
Kutoka 4:15 "Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya."
✓✓Mipango hii yote inayoleta faida kwa Waisraeli kuondoka Misri ni kwa sababu ya Agano la MUNGU na Ibrahimu.
5. Farao aliambiwa na MUNGU Waisraeli ni akina nani
Kutoka 4:22 "Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;"
✓✓Inawezekana Farao aliwatambua Waisraeli ni watumwa wake tu lakini MUNGU Waisraeli kwa MUNGU ni tofauti kabisa na mawazo ya watu wajinga kama Farao wanavyowaza, ni hiyo kwa sababu ya Agano la Ibrahimu ndio maana Waisraeli wanaitwa wana wa Agano.
◼️Vipi Wewe Mteule wa KRISTO siku Moja MUNGU amwambie mchawi au mganga wa kienyeji anayejaribu kukusumbua, MUNGU amwambie "Huyu ni Mwanangu usimguse" Nina hakika huyo mchawi atakimbia na hatakufuatilia tena, hata akijaribu kukufuatilia atapigwa na MUNGU, ni kwa sababu ya Agano lako na Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
6. Musa akafanya Miujiza kwa Nguvu za MUNGU
Kutoka 7:10-13 " Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao........"
✓✓Musa alifanya Miujiza mingi kwa sababu alikuwa ndani ya Agano la MUNGU.
◼️Hata wewe Mteule wa KRISTO unayemtumikia kwa uaminifu Kuna Miujiza itaambatano na Wewe kwa sababu uko ndani ya Agano la Damu ya YESU KRISTO.
2 Wakorintho 3:6 "Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha."
7. Farao piga Moja tu la MUNGU lingemwondoa ili asiwazuie Israel ila MUNGU alitaka kuonyesha Nguvu zake kupitia Farao
Kutoka 9:16 "lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote."
✓✓Hii Ina maana hakuna namna Farao na jeshi lake wangeshinda mbele ya Wana wa Agano.
Agano na MUNGU wa Mbinguni lins Nguvu sana.
8. Majira kwa Israel yalibadilika
Kutoka 12:2 "Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu."
Huwa nafurahi sana nikisoma andiko hili, yaani Wamisri na Waisraeli walikuwa wanaishi nchi Moja lakini kila Mtu na majira yake, mwaka wake, tarehe yake yaani mfano Mmsiri angepanga jambo baya kwa mwisraeli limpate tarehe labda ni 7 February unakuta kwa Waisraeli tarehe hiyo ni 10 January na siku Kuna ratiba tofaauti kabisa, mipango hiyo isingefanikiwa.
Vipi kwako Mteule wa KRISTO tarehe fulani mchawi akakupangia jambo baya na tarehe hiyo MUNGU akawa amekupangia jambo lingine?
Ni uhakika jambo la mchawi halitafanikiwa kamwe.
Kwa Waisraeli tarehe zilibadilika kwa sababu MUNGU alianzisha kalenda yao mpya kinyume na kalenda za wachawi wa Misri, Bwana YESU KRISTO anzisha kalenda mpya kwangu na familia yangu kinyume na kalenda zote za Wachawi, mizimu na nguvu za giza.
9. Mwanzoni Mpya mzuri wa Ibada safi ulianza
Kutoka 12:16,21 " Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.................. Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka."
◼️Agano na MUNGU wa Mbinguni ni agano lenye faida kuu.
◼️Agano na MUNGU linaweza kusababisha ushindi wa ajabu.
◼️Agano na MUNGU linaweza kuwa chanzo Cha mabaya kuzuiliwa.
Kutoka 12:23 "Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi."
◼️MUNGU akupe Neema ya Ajabu ndani ya Agano lake na Wewe katika KRISTO YESU.
◼️MUNGU wa Mbinguni akutoa katika matatizo yote kwa sababu ya Agano lako mbele zake.
Kutoka 12:42 "Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za BWANA kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa BWANA, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao."
◼️MUNGU wa Mbinguni akupe Neema katika agano la Damu ya YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO mkama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments