ATAKAYEWAENDEA WAAGUZI WA MIZIMU ATATENGWA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

 Walawi 20:6 "Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake."

◼️Andiko hili ukilisoma katika tafasiri ya BHN kinasema " Atakayewaendea waaguzi wa mizimu na Wachawi atatengwa na watu wake"

◼️Jambo la kuwaendea waganga wa kienyeji wanaotumia mizimu na majini ni jambo baya sana na ni machukizo kwa MUNGU.

Leo wapo watu wanajiita ni Waganga wa kienyeji, ukiwaendea hao ni machukizo kwa MUNGU.

◼️◼️Ndugu, YESU KRISTO anatosha  Kwa uponyaji na kukupa mahitaji Yako  huhitaji Waganga wa kienyeji.
Bwana YESU KRISTO anasema Mkimbilie yeye, achana na Waganga.

Mathayo 11:28 ''Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.''

✓✓Wewe unayesoma ujumbe huu kataa Kwa namna yeyote ile kuhusika na mizimu  ya ukoo au  au kwenda kwa mganga wa kienyeji maana mganga hutumia mizimu.
Biblia inakukataza kutaka kauli kutoka kwa mizimu.

Kumbu 18:10-12 " Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako."

◾Mtu anayetumia mizimu Biblia inamuita mwenye pepo na huyo hupandisha pepo.

◾Kwa waganga wa kienyeji Kuna mambo mengi yakiwemo kuchanjwa chale, Biblia inakataza mambo hayo.

 Walawi 19:28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.

◼️Ndugu, katika Maisha Yako yote Usikubali kuwaendea waganga wa kienyeji maana hao ni mawakala wa shetani na hutumia Nguvu za giza na mizimu.

 Walawi 19:31 "Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments