![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Walawi 26:1 "Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu."
◼️Ni Neno la MUNGU ndilo linakataza watu kuweka jiwe ili kulisujudia Wala kuweka chochote kinachoonekana kwa macho na kukisujudia.
◼️Kusujudu ni nini?
➡️Kusujudu ni kutoa heshima anayostahili MUNGU wa Mbinguni tu.
◼️Hivyo ukisujudia kitu chochote maana umekipa heshima anayostahili MUNGU wa Mbinguni tu, ni jambo baya sana.
Heshima ndio huonyesha ukuu wa huyo unayemsujudia, kuinamisha kichwa ni ishara tu.
◾Sasa wapo watu kwa kujua au kutokujua husujudia watu, mawe, Sanamu au vitu vya namna yeyote vinavyoonekana, hiyo ni dhambi mbaya.
◼️◼️Ndugu nakuomba uwe kama Mordekai aliyekataa kumsujudia Mwanadamu mjinga aitwaye Hamani.
Esta 3:2-5" Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana."
◼️◼️Ndugu, nakuomba uwe kama akina Meshaki na wenzake waliokataa kusujudia sanamu ya mfalme iliyotengenezwa na Wanadamu.
Danieli 3:12-13,18 " Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. .................. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha."
◾Ni kitu Cha ajabu sana Mwanadamu anaona kitu kilichoumbwa na MUNGU anaanza kukisujudia mfano mawe, jua n.k badala ya kumsujudia MUNGU aliyeumba.
◾Ni jambo la ajabu sana Mwanadamu anasujudia kitu ambacho hakina uhai kilichotengenezwa na yeye au na Mwanadamu mwenzake.
◼️◼️Ndugu,usiwasujudie Wanadamu, usimsujudie Mwanadamu wa aina yeyote.
◼️◼️MUNGU ni mmoja tu na alijifunua kwa Wanadamu kwa njia ya YESU KRISTO, usimsujudie Mungu Mwingine yeyote nje na huyu MUNGU.
◼️◼️Ndugu, usitafute sanamu au jiwe au kitu chochote kilichotengenezwa na Wanadamu ukakiabudu.
◼️◼️Ndugu, usitafute miungu mingine ili kuisujudia.
Isaya 44:15 "Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia."
➡️Waisraeli kipindi fulani MUNGU alitaka kuwaangamiza wote kwa sababu ya kuabudu ndama iliyotengenezwa kwa Heleni na pete za watu.
Kutoka 32:7-10 " BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwan6a akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu."
✔️✔️Ndugu usifuate sanamu ili kuisujudia.
✔️✔️Ndugu usifuate jiwe lililo mji wowote Duniani ili kulisujudia au kulipa heshima.
◼️◼️Heshima ya kusujudu mpe MUNGU Baba wa Mbinguni Pekee.
◼️◼️Heshima ya kusujudu mpe Bwana YESU KRISTO pekee maana hata Malaika Mbinguni humsujudia.
Waebrania 1:6 "Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa MUNGU."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments