![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Ni dhambi kufanya dhambi hata kama hujajua hiyo kama ni dhambi.
Walawi 5:17 "Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake."
◼️Ukifanya kitu ambacho MUNGU amezuia ni dhambi hata kama hukujua kama ni dhambi.
◼️ Chochote ambacho MUNGU amekataa katika Neno lake ukikitenda hata bila kujua ni dhambi.
✓✓Hivyo ni jukumu lako kujifunza mafundisho ya Biblia Takatifu katika KRISTO YESU ili ujue Nini ni dhambi ili uiepuke dhambi hiyo.
✓✓Ni Muhimu Kila Mtu anayejua kwamba jambo fulani ni dhambi, ni Muhimu Mtu huyo akawaambia na watu wengine ili wajue ni dhambi ili wasije kusema walitenda kwa sababu hawakujua.
Ndio maana Mwandishi mmoja wa Zaburi anaomba akisema "Unitakase na Mambo ya Siri"
Zaburi 19:12 "Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri."
◼️Ndugu ni jukumu lako kujua Nini ni dhambi na Nini sio dhambi.
Ngoja Mimi Leo nikuonyeshe dhambi mbili ambazo watu wengi hawajui Kama ni dhambi mbaya sana.
➡️Dhambi ya kwanza.
Ni dhambi kutokumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako hata kama unafanya mambo mema kiasi gani ila dhambi hiyo ukiendelea nayo hadi mwisho wa Maisha Yako huwezi kamwe kwenda uzima wa milele.
Yohana 3:36 "Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya MUNGU inamkalia."
◼️Kama ghadhabu ya MUNGU inakukalia kwa sababu hujamwamini YESU kama Mwokozi wako maana yake kwa tendo hilo umefanya dhambi mbele za MUNGU na dhambi hiyo haiondoki hadi umpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Leo Kuna watu wengi hawamwamini Bwana YESU KRISTO kama Mwokozi wao ndio maana hawataki kuokoka, hawamwamini kwa sababu hawajui bila YESU KRISTO hawawezi kamwe kuupata uzima wa milele hata kama wana dini zao nzuri.
Biblia Iko wazi sana katika Yohana 3:16-18 kwamba " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."
◼️Hata kama huibii watu, huzini, husemi uongo, huendi kwa waganga wa kienyeji, sio kahaba hiyo ni sawa kabisa na unafanya vyema lakini kama katika siku za Maisha Yako hutampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuishi katika Neno lake huwezi kamwe kuuona uzima wa milele.
Marko 16:15-16 ”Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.Aaminiyena kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”
Kumbuka"Asiyemwamini YESU atahukumiwa"
Kumwamini YESU ni Nini?
◼️Kumwamini YESU KRISTO inahusisha mambo mawili kumkubali kama Mwokozi wako binafsi na kumpokea kama Mwokozi wako binafsi.
Hivyo anayemwamini YESU ni Mtu yule anayemkubali kama Mwokozi wake Kisha akachukua hatua ya kumpokea kama Mwokozi wake.
Leo Kuna mamilioni ya watu wana dini zao na madhehebu yao na wanafariji watu kwamba Mungu ni mmoja, ni kweli MUNGU wa kweli ni mmoja naye amejifunua kupitia KRISTO YESU Pekee, usipompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako katika siku za Maisha Yako huwezi kamwe kuingia uzima wa milele.
1 Yohana 5:11-12 "Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima."
Nimekujulisha jambo hili ambalo ni la MUNGU kabisa ili Sasa kama unadhani Wanaookoka kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao wanajifurahisha Leo tambua hawajifurahishi ila wanataka uzima wa milele wakidumu kuisha maisha matakatifu ya Wokovu.
➡️Dhambi ya pili.
Kutoa mimba ni dhambi mbaya sana.
Kutoa mimba mbele za MUNGU ni dhambi ya kuua kama wauaji wengine.
Kumbu 5:17 "Usiue."
Mtoto anakuwa binadamu hai tangu akiwa tumboni hivyo ukimuua umemuua Mtu kama watu wengine.
Kuna watu Biblia inasema wamejaa Uuaji, baadhi yao ni watoa mimba.
Warumi 1:29 "WAMEJAWA NA udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na UUAJI, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,"
Katika utumishi wangu kwa KRISTO Kwa miaka 18 tangu nimeanza nimezungumza na Wanawake wengi sana baadhi yao Tena walio wengi hawajui Kama kutoa mimba ni dhambi.
Ndugu Niko hapa Leo kukujulisha kwamba kutoa mimba ni dhambi mbaya sana.
➡️Dada mmoja hata miaka 30 alikuwa hajafikisha lakini aliniambia siku Moja kwa kinywa chake kwamba amewahi kutoa mimba nyingi sana ila anazokumbuka tu ni 10.
➡️Mama mmoja Yuko katika Ndoa yake na wamezaa watoto 4 hivyo hawataki kuzaa zaidi hivyo kila akibeba mimba anaitoa Tena wakati Mwingine bila hata kumshirikisha Mume wake, yaani anaona ni kawaida tu.
➡️Dada mmoja msomi mwenye kazi nzuri siku Moja akaniambia nimuombee ili miaka 2 baadae afunge Ndoa na mchumba wake, wakati ananimbia maneno hayo ROHO MTAKATIFU aliniambia pale pale kwamba Mtu huyo ametoa mimba na nimuonye.
Nikamwambia Dada yule akasema ni kweli ametoa mimba siku chache kabla na sababu ya kutoa mimba ni kwamba yeye na Mchumba wake wanaheshimika sana na walishaapiana hawawezi kuzaa kabla ya Ndoa lakini wanaishi pamoja miaka kadhaa hivyo ameshabeba mimba nyingi sana na zote alizitoa.
Ndugu zangu, Niko hapa kuwaambia kwamba kutoa mimba ni dhambi ya mauaji, Wewe huna tofauti na jambazi anayevamia watu na kuua.
Kuna watu Leo wako kuzimu wakijiandaa kwenda jehanamu kwa sababu hawakutubia Uuaji wao.
Ufunuo 9:21 "Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao."
Kuna mwaka fulani kipindi fulani kwa miezi kadhaa nilipata msukumo rohoni wa kumuuliza Kila ninayemuombea kwa simu kama amewahi kutoa mimba, asilimia zaidi ya 98 wote walisema wamewahi kutoa mimba nikawaongoza sala ya Toba na hivyo nikagundua Inawezekana kabisa Watoto wanaozaliwa Duniani ni wachache kuliko watoto wanaouawa kwa kutolewa mimba, inatisha sana.
Sasa Leo unakuta Mtu wa Kanisani kabisa lakini ni mzinzi na anapopata mimba kwa kuogopa kutengwa au kushuka heshima yake kwa binadamu anatoa mimba.
Ndugu heshima za Wanadamu Zina mwisho wake ambao ni kaburi, je baada ya hapo itakuwaje?
Kama ulikuwa hujui kama kutoa mimba ni dhambi basi nakujulisha Leo kwamba ni dhambi mbaya sana.
Kumbuka watakaokuwa jehanamu ni pamoja na wauaji.
Ufunuo 22:15 "Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya."
Ndugu, nafasi ya kutubu unayo Leo, tubu na amua kuokoka upya kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Kama utaisikia Sauti ya MUNGU kupitia somo hili usifanye Moyo wako kuwa mgumu, mpokee YESU KRISTO na Anza upya na Wokovu wake utasamehewa dhambi zote hata kama ulitoa mimba 200.
Ndugu zangu ni jukumu kwa kila anayefahamu kwamba kitu fulani ni dhambi, ni jukumu lake kuwaeleza wengine ili Wasiukose uzima wa milele.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments