UTAJUAJE KAMA UNAPAMBANA NA NGUVU ZA GIZA KWENYE ULIMWENGU WA ROHO?

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 


Karibu tujifunze kwa ufupi Neno hili la MUNGU aliye hai.


Utajuaje kama unapambana na nguvu za giza kwenye ulimwengu wa roho?


1.  Pale mtu au watu wanapotumika kama kikwazo ili kukuzuilia baraka Fulani kwenye maisha yako.


Mathayo 16:23 "Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya MUNGU, bali ya wanadamu."


Nguvu za giza zinakuwa ndani ya watu hao ili hizo nguvu za giza zipambane na wewe kukuzuilia mipango yako mizuri au baraka zako.


1 Timotheo 5:15" Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani."


Watu watakaotumiwa na nguvu za giza kukuzuia au kukuonea wanaweza kujijua kama wanatumiwa na nguvu za giza na wanaweza pia kutumiwa na nguvu za giza bila wao kujua.


Luka 22:3 "Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara."


2. Pale unapopata mashambulizi rohoni juu ya jambo Fulani au juu ya baraka fulani unayoihitaji.


Ayubu 4:14-16 " Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote.  Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena,"


3. Pale unapoona kuna kizuizi cha siri cha kukuzuia wewe kupata baraka fulani.


1 Wathesalonike 2:18 " Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia."


4. Pale ROHO MTAKATIFU anapokujulisha iwe kwa ndoto au maono au mazingira au kwa Neno lake au kwa ufunuo wa ROHO MTAKATIFU juu ya nguvu za giza unazitakiwa kupambana nazo.


1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."


5. Pale wakala wa shetani au mwanadamu anayetumika kipepo anapokutisha au kukulaani au kukutamkia mabaya na ukajua kwamba hakutakii mema.


Zaburi 41:5-7 " Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea? Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena. Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya."


Ukiona hivyo ujue huyo atatumia nguvu za giza kupambana na wewe.


6. Unapokuwa na mapepo au unapogundua umerogwa au umefungwa maagano ya giza n.k


Luka 6:18 "na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa."


7. Kama ukoo wenu familia kumewahi kufanyika matambiko, mazindiko, Mikataba ya kishetani n.k


Iwe viifanyika kipindi umeshazaliwa au kabla hujazaliwa.


2 Wafalme 17:17 "Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha."


8. Unapokaa eneo ambalo linatawaliwa na nguvu za giza.


Ufunuo 2:13 "Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani."


Ukiwa mtaa au mji au eneo au familia au ukoo ambapo kuna kiti cha enzi cha shetani, yaani kuna wachawi, waganga wa kienyeji, wanajimu, ibada za sanamu, kunakofanyika matambiko na mazindiko, kuna madhabahu za giza, kuna sehemu nyingi za kuabudia dini zinazompinga YESU KRISTO ujue huko shetani amejiimalisha sana na  mawakala wa shetani ni wengi huko.


Ndugu, ukiona hivyo ujue unapambana na nguvu za giza kwenye ulimwengu wa roho.


Dawa ni kupambana nao kwa maombi katika jina la YESU KRISTO, huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu.


Yohana 14:13-14 " Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."


MUNGU akubariki sana.


Nitafafanua siku moja somo hili.


By Peter Mabula.


Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.


+255714252292

Comments