ILI USIKWAME KIROHO KUTOKANA JAMII MBAYA INAYOKUZUNGUKA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.


 Walawi 18:3 "Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao."


◼️Katika Andiko hili MUNGU anawakataza watu wake kufuata Matendo ya kabla hajawaokoa na Wala wasifuate Matendo ya jamii ya Sasa wanayoishi nayo isiyomcha yeye.


➡️Hata wewe Inawezekana kabla Hujampokea YESU KRISTO na kuokoka ulikuwa unaishi Maisha ya dhambi ukifuata jamii Yako au Ukoo wako au Ndugu zako, ukishaokoka hutakiwi kufuata Matendo ya zamani.


◼️Yaone mambo ya zamani maovu yaone kuwa si kitu Tena Sasa.


Wafilipi 3:8 "Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua KRISTO YESU, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate KRISTO;"


◼️Lakini pia kama MUNGU amekupa kuishi eneo fulani wakati huu iwe umepanga au umejenga hutakiwi kuishi kwa kufuata mitindo ya Maisha ya wanaokuzunguka ambao hawamchi MUNGU.


➡️Sasa Inawezekana umehamia eneo ambalo jamii nzima hapo ni waabudu shetani.

Inawezekana Ndugu zako wote ni waabudu sanamu tu.


✔️✔️Mtu yeyote anayekataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake huyo anaabudu shetani.

Nje na KRISTO YESU Kuna shetani na sio vinginevyo.


◾Sasa ufanyeje ili usikamatwe na tabia zao mbaya jamii wanaokuzunguka?


1. Usifanye Agano na watu wabaya..


Kutoka 23:32-33 " Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako."


➡️Usifanye Agano nao ili isiwe tanzi kwako.


2. Usiende kwenye Ibada za kishetani za jamii inayokuzunguka, Waisraeli walikaribishwa wakanasa.


Hesabu 25:2-3 " kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli."


➡️Waisraeli walipokaribishwa wakanasa baadae Cha ajabu wakajikuta wanaanza kuabudu miungu, wakasahau  Matendo makuu ambayo MUNGU wa Mbinguni alikuwa amewatendea.


Waamuzi 2:11 "Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali."


➡️Kwa kosa hilo ikapelekea hasira  ya MUNGU kwao na adhabu kwao.


Waamuzi 2:20 "Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu;"


3. Usiingie katika Ndoa na Mtu wa jamii hiyo ya waabudu shetani, Wala Usikubali Mtoto wako akaoa au kuolewa na Mtu wa jamii hiyo.


Kumbu 7:3-4 " binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya BWANA juu yenu, naye atakuangamiza upesi."


➡️Kuoana na Mwabudu shetani ni kumkaribisha shetani katika Maisha Yako.


➡️Samson alimkaribisha Delilah mwabudu miungu akaharibu hatima yake kwa kumletea Wafilisti waliomtesa.


Waamuzi 16:18 "Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.'


➡️Ahabu alimkaribisha Yezebeli akaharibu hatima yake njema.


1 Wafalme 21:25-26 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)


◼️ Usikubali kuoana na Mtu asiye na YESU KRISTO Wala Usikubali Mtoto wako akaoana na Mtu anayempinga YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake.


4. Kataa ushawishi wowote wa dhambi kutoka kwa Mtu anayeabudu shetani.


Mithali 1:10 "Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali."


◼️ Usikubali Mtu yeyote akakushawishi kutenda dhambi nawe ukatenda, akikushawishi kataa na hata ikilazimisha kuvunja urafiki naye vunja ili usimkose MUNGU katika KRISTO YESU.


5. Enenda kwa ROHO MTAKATIFU katika Maisha Yako eneo hilo.


Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."


◼️ROHO MTAKATIFU ndio hitusaidia kuzijua dhambi na kuziacha kama tukimtii.


◼️Ukimtii ROHO MTAKATIFU umemtii MUNGU Mwenyewe, hivyo katika Maisha Yako yote enenda kwa ROHO MTAKATIFU.


6. Baki na msimamo wako thabiti kwa YESU KRISTO.


1 Wakorintho 16:13 ''Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari."


◼️Ayubu katika jamii isiyomcha MUNGU yeye alibaki akimcha MUNGU.


Ayubu 1:1 "Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, NI MMOJA aliyemcha MUNGU, na kuepukana na uovu."


◼️Lutu katika mji wa Wazinzi, mashoga na Wafiraji yeye alibaki upande wa MUNGU hata akapata kibali Cha MUNGU.


Mwanzo 19:21-22 " Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari."


◼️Hata wewe haijalishi jamii inayokuzunguka inaamini tu mizimu na majini, Wewe baki na YESU kwa utakatifu na Imani thabiti.


7. Uwe Mtu wa Maombi ili kushinda majaribu ya watu hao wanaokuzunguka wasiomcha MUNGU wa Mbinguni.


Mathayo 26:41 "Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu."


◼️ Maombi ni Maisha ya Mkristo.

◼️ Maombi ni mkono mrefu zaidi wa kupokea kutoka kwa MUNGU.


Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe

Comments