MAMBO YANAYOLETA LAANA KWA MTU.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.

Karibuni tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.


◼️Ukisoma Kumb 11:26-28 unaona mbele ya Kila Mtu Kuna baraka na laana .

Biblia inasema  " Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua."


➡️Baraka itatokana na Mtu kusikiliza maagizo ya MUNGU na kuyatenda, na laana ni pale Mtu hatasikiliza maagizo ya MUNGU na badala yake Mtu huyo akakengeuka akamwacha YESU KRISTO na kuiandama miungu mingine.


✔️✔️Kwa njia hiyo tunagundua Kuna mambo yanaweza kuleta laana kwa Mtu.


2 Petro 2:14 "wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;"


◼️Kumbuka pia Kuna baadhi ya laana hazikai kwa Mtu ila zinakaa katika vitu vya Mtu, Ndugu mhitaji sana ROHO MTAKATIFU na omba uwe na macho ya rohoni ili kuona na kugundua ili kuondoa laana hiyo.


➡️Kumbuka hata Ardhi tu inaweza ikalaaniwa.


Mwanzo 3:17 "Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ARDHI IMELAAMIWA KWA AJILI YAKO; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;"



➡️Unakumbuka Bwana YESU aliulaani Mti?


Mathayo 21:19-20 " Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara?"


 ◼️Mifano hii miwili ikufundishe kwamba laana inaweza ikawa katika vitu hata kama anayevitumia hana hiyo laana, madhara atayapata hata kama yeye hana laana.


◼️Kuishinda laana ya namna hii ni kutubu, kuomba MUNGU akuonyeshe na kutatua tatizo kiroho.


◼️Katika maandiko Kuna Ardhi fulani ililaaniwa na Mtu  yeyote ambaye angejenga hapo laana iambatane naye na maneno yalitotoka wakati wa laana ni kwamba atakayejenga hapo afiwe mapema na Mtoto wa kwanza na wa Mtoto wa mwisho ikawa hivyo hivyo.


➡️Hii ilitokea hapa baada ya watu wa Yeriko kumsumbua Joshua hadi aoatamka laana.


Yoshua 6:26 "Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo."


➡️Mtu mmoja bila kujua miaka mingi Baadae akajenga pale na laana ile ikampata kama ilivyotamkwa.


1 Wafalme 16:34 "Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni."


◼️Ndugu katika Maisha Yako unamhitaji sana YESU KRISTO Wala usifanye masihara ili iwe usalama wako katika maeneo mengi ya Maisha.


◼️Ndugu mambo mengine msikilize sana ROHO MTAKATIFU ili akusaidie namna ya kuepuka laana na kuishinda laana ya maeneo au ya vitu.


 ◼️Mambo yanayoweza kuleta laana kwa Mtu ni haya;


1. Kuiacha njia ya MUNGU  ambayo ni KRISTO Kwa kufuata miungu mingine nje na MUNGU wa Mbinguni aliyejifunua katika KRISTO YESU.


Kumbu 11:28 "na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua."


◼️Ndugu, ukimwacha YESU KRISTO umeamua kufuata laana.


◼️Ukifuata miungu na kumuacha YESU KRISTO ujue umefuata laana.


◼️Kumwacha YESU KRISTO ni chanzo kikuuu Cha laana kwa watu wengi.


Kumbu 28:20 "BWANA atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo."


◼️◼️Kuishinda laana ya namna hii ni Wewe kurudi kwa YESU tubu, okoka na Anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.


2. Kuwa Mtu Mwovu.


Mithali 3:33" Laana ya BWANA i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki."


➡️Maana ya Mtu Mwovu ni Mtu katili anayewafanyia wengine ukatili.


➡️Mtu Mwovu ni Mtu dhalimu na anayenyanyasa watu.


◼️Ukitaka kuwa na laana ya MUNGU haraka sana basi fanyia wengine ukatili, wanyanyase watu walio Wanyonge ukidhani utakaa salama, hakika hutakaa salama maana laana ya MUNGU utakuwa nayo.


◼️Ndugu, kama unateswa na laana hii kwa sababu ya ukatili uliowahi kuufanya kwa watu  dawa ni kuwaona Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO wakuongoze sala ya Toba, okoka Kisha Anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO, unaweza pia baada ya hapo ukawaomba msamaha uliowakosea kama wapo ili na wao wakuachilie, kama hawapo Duniani tubu kwa MUNGU na Anza kumpendeza MUNGU katika KRISTO YESU.


3. Kama ni Mtumishi na haumpi MUNGU heshima yake.


Malaki 2:1-2 " Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema BWANA wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni."


◼️Ni kosa kubwa sana kwa Mtumishi wa MUNGU kutokumpa MUNGU heshima yake, ni kujitafutua laana harafu baadae unaanza kulalamika.


➡️Leo Kuna  Watumishi hadi wanafanya Maombi bila kutaja Jina la YESU KRISTO, kwa sababu Wana Nguvu za MUNGU basi Kuna kanuni za kiroho wameanza kuzidharau, ni mbaya sana maana ni kujitafutia laana.


◼️Kumbuka ni YESU KRISTO ndio mwenye Kanisa na ni yeye ndiye amekuchagua umtumikie Hakikisha hujipi utukufu Wewe.


4. Laana ya kutokutoa fungu la kumi kwa MUNGU.


Malaki 3:9-10 " Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la."


 ◼️Laana hii hufungulia umaskini na  uhitaji.


◼️Laana hii hupiga uchumi na vyanzo vya mapato ya Mtu.


◼️Laana hii husababisha ulinzi wa MUNGU kuondoka kwenye Mali za Mtu, kazi,kipato, biashara au chanzo Cha uchumi wake.


✔️✔️Ndugu jitenge mbali na miungu ili ukwepe laana katika Maisha Yako, Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi na laana zote zitafutika kama pia baada ya hapo hutaendelea na Matendo ambayo husababisha laana.


✔️✔️Ndugu, Acha kuwafanyia watu Wanyonge ukatili na unyanyasaji ili ukwepe laana.


✔️✔️Ndugu uwe mtii kwa MUNGU hata kwa Mali zako na MUNGU atazilinda daima.


Mithali 3:9-10 " Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya."


Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe

Comments