
Na Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
➡️Manabii wote watu kweli tangu zamani zote humshuhudia YESU KRISTO kuwa ndiye Mwokozi na ni katika yeye tu ndio Wanadamu hupata ondoleo la dhambi.
Matendo 10:43 "Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi."
◼️Hivyo Nabii yeyote aliyekuja kabla ya YESU KRISTO au aliyekuja baada ya YESU KRISTO, Nabii huyo kama ni Nabii wa kweli wa MUNGU kipimo ni anasema Nini juu ya YESU KRISTO, kama Nabii huyo anakataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake na njia ya uzima wa milele huyo Nabii sio wa MUNGU Bali wa shetani.
➡️Ndugu Fanya utafiti na ukigundua Nabii wako anakataa Wokovu wa KRISTO kwa watu wote, huyo Nabii wako ni tapeli na alitumwa na shetani.
◼️Manabii wote wa MUNGU hushuhudia YESU KRISTO ni Mwokozi wao na wa ulimwengu wote.
➡️ YESU KRISTO ni mmliki wa ulimwengu wote ambaye mataifa yote wanatakiwa kumtii.
Mwanzo 49:10" Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii."
Na kama hujui ni kwamba hata uumbaji huu tunaoufahamu wa Dunia na Wanadamu wote, uumbaji huu ilifanyika kwa Njia yake na kwa ajili yake yeye Bwana YESU.
Wakolosai 1:15-17 " naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.
Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye."
◼️Hivyo Ukiona watu wowote hawamtii YESU KRISTO ujue ni kujitoa Ufahamu tu ila ipo siku Mataifa yote watamtii kama andiko hapo juu linavyosema.
◼️ Mwanadamu yeyote mwenye Akili timamu hawezi kumkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake.
◼️Watu wengi walio nje na YESU KRISTO ni kwa sababu ya kuwaheshimu wazazi wao au watu wao wa Karibu waliowafundisha dini za kitofauti zilizo kinyume na KRISTO na zilizo machukizo kwa MUNGU.
◼️Kama Wanadamu wote tuliumbwa kwa ajili ya KRISTO kama maandiko yamavyosema hapo juu ujue Mtu anayemkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake Mtu huyo anakuwa amejitenga na uzima wa milele.
◼️Mtu yeyote Duniani hata kama ana dini yake nzuri kiasi gani kama Mtu huyo hatampokea YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake Mtu huyo hataupata uzima wa milele kamwe.
◼️Rafiki kama unauhitaji uzima wa milele hakika tambua unamhitaji YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako.
➡️ Bwana YESU atamiliki Ufalme wa milele unaotawala Dunia nzima, ukijitenga nae umejitenga na hatima Yako ya furaha milele.
Ufunuo wa Yohana 11:15 "Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa BWANA wetu na wa KRISTO wake, naye atamiliki hata milele na milele."
◼️Umeshawahi kujiuliza kwamba watu wa dini zote unazozijua hatima yao itakuwa mikononi mwa Bwana YESU, waliomkataa kama Mwokozi wao wataenda jehanamu na waliomkubali kama Mwokozi wao na wakaishi Maisha ya Wokovu wake wataenda uzima wa milele.
Mathayo 25:31-33 " Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;
na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;
atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto."
➡️Hapo ndipo unagundua dini zipo kwa faida ya aliyezileta lakini YESU KRISTO yupo kwa ajili ya uzima wa milele.
➡️Uamuzi ni wako ufuate dini tu bila YESU Kisha uende jehanamu au umfuate YESU KRISTO Kwa ajili ya uzima wa milele?
Maamuzi sahihi Yako Moyoni Mwako.
Mimi nilichogundua Neema ya Wokovu umewafikia watu wengi sana labda bado Wewe tu uliyeshupaza shingo humtaki YESU.
Nimewahi kuwaongoza sala ya Toba watu wengi sana hasa Wanawake kutoka dini za kinyume na KRISTO.
Mtu mmoja akiwa Mashariki ya Kati alinitafuta akaniambia kwamba Bwana YESU KRISTO amemtokea na Akamwambia kama anataka uzima wa milele ampokee kama Mwokozi wake na aanze kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wake, Mtu yule alinitafuta nikamuongoza sala ya toba akaokoka na Leo ni Mke wa Mchungaji baada ya miaka mingi kupita, alivyokuwa ananiambia niligundua jambo Moja Neema ya MUNGU imefunuliwa kwa watu wengi na baadhi yao wamechukua hatua za kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi labda bado Wewe tu ambaye humtaki YESU kwa sababu hutaki kudharauliwa na Ndugu zako.
Ndugu ni heri Ndugu wakudharau kwa ajili ya YESU Kisha uje uende uzima wa Milele kuliko Ndugu wakupongeze Kisha jehanamu ya moto Milele.
Mama mmoja jijini Tanga ambaye Mumewe ni kiongozi wa dini zilizo kinyume na KRISTO, Mama huyu aliumwa na akawa katika hatari ya kufa, Binti yake ikabidi aanze kutafuta msaada wa Maombi mtandaoni maana familia yao ni watu wanaoheshimika katika dini yao, akanitafuta na kuniunganisha na Mama yake. Yule Mama akamkubali YESU na ikawa baadhi ya siku mmewe akiwa Ibadani anaongoza Ibada yeye ananipigia nimfundishe Biblia na kumuombea, yote kwa yote ni kwa sababu Neema ya Wokovu wa KRISTO umefunuliwa, Ndugu Wewe Wala huna kizuizi ila humtaki YESU, kwanini?
◼️Ndugu, kama kweli unautaka uzima wa milele Mkimbilie YESU KRISTO Kwa ajili ya Wokovu utaokoka.
Kama umeusoma ujumbe huu na hujaokoka nakuomba kimbilia Kanisani ukaokoke.
Hakuna njia ya mkato kwenda Mbinguni na hakuna njia nyingine ya uzima wa milele Bali njia ni Moja tu YESU KRISTO.
Matendo 4:12 "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."
◼️Ndugu, ukimfuata YESU umefuata uzima wa milele, amua Leo kumfuata utaokoka.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe
Comments