KANISA LA MUNGU TUWENI NA UMOJA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.


◼️Umoja katika KRISTO huleta ukamilifu.


Waefeso 4:3-7 " na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

 Bwana(YESU ) mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni BABA wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.


◼️Kanisa la KRISTO duniani tunatakiwa kuwa na umoja ndipo Injili ya KRISTO itazaa matunda vyema. 


Biblia inasisitiza kuhusu umoja katika wateule wa MUNGU.

Zaburi 133:1" Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja."


◼️Kanisa la MUNGU tukiwa na umoja katika kazi ya MUNGU tutafanya vyema sana na kazi yetu katika Injili itazaa matunda mema mengi sana.


Yohana 17:21 "Wote wawe na umoja; kama wewe, BABA, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma."


➡️Leo kumekuwepo na Baadhi ya maeneo ya ajabu sana maana watumishi wa MUNGU ndio wanaofanya kampeni ili watu wasiende kwenye mafundisho ya Mtumishi wa MUNGU mwenzao.

 Sio kwamba Mtumishi huyo anafundisha injili nyingine bali anafundisha Injili ya kweli ya KRISTO YESU iokoayo.

Umoja umeondoka hadi shetani ameingilia kati ili kuzuia Injili ya KRISTO.


➡️Leo Kuna madhehebu ya kiroho Mchungaji Yuko tayari kumzuia Binti kuolewa na Kijana kutoka dhehebu lingine safi la Kiroho na hakuna tatizo lolote la kiroho.


◼️Kibiblia Kila Binti au Kijana ameruhusiwa na MUNGU kuoana na yeyote ambaye hajaingia katika Ndoa, sharti la MUNGU ni Moja tu kwamba aolewe au kuoa kutoka katika jamii ya ndugu zake yaani Wateule wenzake wa KRISTO.


Hesabu 36:6 "BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao."


◼️Yaani Binti Usikubali tu kuolewa n mpagani au mpinga KRISTO na Kijana Usikubali tu kuoa mpagani au mpinga KRISTO, ila dhehebu tofauti na lako MUNGU hajakataza kama Mtu huyo ameokoka na anaishi Maisha Matakatifu.


➡️Leo kuna baadhi ya madhehebu katika maeneo yao wakisikia kuna mkutano wa Injili katika maeneo yao na Mhubiri anatokea dhehebu lingine wanaanza kushawishi watu ili wasihudhurie mkutano huo wa Injili, hiyo ni roho ya mpinga KRISTO.


1 Yohana 2:18 "Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho."


◼️Kwanini tunashindwa kujua kwamba YESU KRISTO aliyehubiriwa Kanisa la Rumi ndio huyo huyo aliyehubiriwa Kanisa la Filipi au Kolosai.

Je mbona hatuoni Kanisa la Efeso wakikataza Watu wao kuoana na Wakristo wa Kanisa la Korintho?


➡️Leo baadhi ya Madhehebu hufundisha kuwaona Madhehebu mengine ni wapagani wakati na wao wameokoka.

Yaani Mtu aliyeokoka na anaishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa KRISTO unamwita mpagani kisa hayuko katika dhehebu lako?

Huo ni utoto kabisa.


Yohana 1:12-3 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."


Tulikofikia sasa ni mbali sana, haipaswi kuwa hivyo.

Ndugu zangu, nawasihi Mimi niliye Mdogo kabisa Tena Muumini tu Kanisani naomba Kanisa la KRISTO tuwe na umoja.

Kwa kazi yangu ya huduma ya kazi ya MUNGU kama Mwalimu kwa miaka hii 18 tangu mwaka 2008 nimekutana na makumi ya watu au hata mawia ambao wengine Kanisa kimewatenga kwa sababu tu wamefunga Ndoa na watu wa Madhehebu mengine ya kiroho.

Kuna watu hadi familia zao na Wazazi wao wametengwa kwa sababu tu walipohamia mkoa au mji Mwingine na kukuta dhehebu lao halipo wakajiunga na dhehebu lingine safi la Kiroho ili waendelee kumwabudu MUNGU, jambo hilo ni kosa kwa dhehebu lao la Kwanza na kusababisha kutengwa familia nzima.

Leo Kuna watu wanasema wameokoka na YESU ni Mwokozi wao lakini hawasalimiani, mifano hii ni michache katika mingi sana.


1 Wakorintho 1:10-11 " Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu YESU KRISTO, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu."


Leo katika baadhi ya madhehebu wanawafundisha watu kuliona dhehebu lao ni la muhimu kuliko hata YESU KRISTO Mwokozi.

Watu wanakuja kumhubiri YESU anayeokoa kisha wewe unafanya kampeni za kuwazuia watu kuokoka, ni mbaya sana na hiyo ni roho ya mpinga KRISTO.


Na wengine chuki hizi huja kwa sababu ya upako wa MUNGU kwa Mtumishi tofauti na Wewe au ana huduma tofauti na Yako au ana Neema kubwa sana kuliko Wewe.

Ni vizuri sana Kila Mtu kukubaliana na alichopewa na MUNGU ili asiwachukue wengine walio na kazi kubwa kuliko yeye.


1 Wakorintho 12:4-12 " Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na BWANA ni yeye yule.

 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana.

 Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule;

 mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja;

 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na KRISTO."


◼️Ndugu zangu Kanisa la kweli la YESU KRISTO ni lazima tuwe na umoja.


Hata Bwana YESU alituombea umoja.

Yohana 17:11 " Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo."


Mimi Peter Mabula ninachojua ni kwamba aliye wa KRISTO kweli lazima afurahie watu kuokoka hata kama wamehubiriwa na Mhubiri Mwingine.


Ukimuona Mtumishi au Mkristo anachukua watu kuokoka au anazuia watu kuokolewa na Bwana YESU ujue mtu huyo ni mpinga Kristo.

Kanisa la MUNGU lazima tuwe na umoja.


Na kipimo Cha kuonyesha kwamba Kanisa Lina umoja ni pale tutakapowaona wengine walio Kanisa ni Bora kuliko sisi.


Wafilipi 2:3" Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake."

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe

Comments