MAMBO 10 YA MUME KUJUA KATIKA NDOA YAKE.

 

Peter na Jemimah Mabula 
Watenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Je Wewe ni Mwanamume?

Mhubiri 7:28 "ambayo bado nafsi yangu nikali nikiitafuta, nisiione; mwanamume mmoja katika elfu nimemwona; ........"

Leo nazungumza kuhusu Mwanaume.

➡️Inawezekana wewe ni Mwanamume na uko katika Ndoa, Jifunze Neno la MUNGU hili 

➡️Inawezekana wewe ni Mwanamume ila hujaoa, Jifunze Neno la MUNGU hili kwa faida Yako wakati utakapoingia katika Ndoa Takatifu.


MAMBO KUMI YA MUME KUJUA KUHUSU NDOA YAKE.


1. Kumpenda Mke wako.

Wakolosai 3:19 "Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao."

◼️Kumpenda Mke Wako ni Amri ya MUNGU hivyo ifuate daima amri hii ya kumpenda Mke Wako.

Waefeso 5:28 "Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe."

2. Kuishi na Mke wako kwa akili njema.

1 Petro 3:7 "Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."

◼️Hii Ina maana mpe Mke Wako heshima moyoni Mwako, kwa Ndugu na Kwa jamii, Fanya mambo yanayoongeza heshima ya Mke Wako.

◼️Kuishi na Mke Wako kwa akili maana yake usiende kiroho tu kuhusu suala la Ndoa, akili yako nzuri inahitajika sana pia.


3. Baki kuwa kichwa cha familia yako.

Waefeso 5:23 "Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili."

◼️Kuwa kichwa Cha familia maana Baki kuwa Kiongozi wa familia Yako na Ndoa Yako.

➡️Kuwa kichwa Cha familia sio maneno ni vitendo.

◼️Usikubali Mkeo ndio akawa Kiongozi Mkuu wa familia Yako kwa sababu yeye ndio sababu Pekee ya kipato Cha familia yenu huku Wewe umelala tu, hii maana yake usimbebeshe Mkeo majukumu yakupasayo Wewe wakati Wewe upo, ni heri msaidiane kama MUNGU amembariki mkeo kazi au ujuzi au akili vinavyoleta kipato.

◼️Timiza Wajibu wako kwa mkeo na Watoto.
Fanya kazi ili kuwa na kipato ili utimize majukumu Yako ya kuitunza familia Yako, hapo utakuwa kichwa Cha familia.


4. Mtambue MUNGU ili aisaidie familia yako, Mjue MUNGU wa kweli na Mwabudu yeye daima.

1 Yohana 2:14 "Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. .........."

◼️Aliye tangu mwanzo ni MUNGU.
◼️Aliye tangu mwanzo ni Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

◼️Ukimtambua aliye tangu mwanzo utachagua kuwa chini yake hivyo utaifanya familia Yako yote kumwabudu yeye MUNGU daima katika KRISTO YESU, hiyo ni faida kubwa kuliko zote kwako na Kwa uzao wako baada Yako.

➡️Mfano hai wa Mtu aliyemtambua MUNGU na kufundisha kizazi chake kumcha MUNGU ni Ibrahimu.

Mwanzo 18:17-19 " BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? KWA MAANA NIMEMJUA YA KWAMBA ATAWAAMURU WANAWE, NA NYUMBA YAKE BAADA YAKE WAISHIKE NJIA ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake."

◼️Ibrahimu aliwekeza familia yake kwa MUNGU ndio maana hadi Leo kizazi Cha Ibrahimu Kila Mtu anakifahamu ingawa Ibrahimu aliishi miaka 3,000 iliyopita, lakini Vizazi vya watu waovu walioishi katika wakati wa Ibrahimu hakuna anayewafahamu Leo.

◼️Kwanini unamfahamu Ibrahimu na kizazi chake, ni kwa sababu Ibrahimu alimtambua MUNGU aliye tangu mwanzo kuwa ni MUNGU wake na akafundisha kizazi chake kuambatana na MUNGU 


5. Kuachana na Baba yako na Mama yako ili ukaanzishe familia yako.

Mwanzo 2:24 "Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja."

◼️Lengo la MUNGU Kila Mwanaume baada ya kufika wakati wa kuoa  atoke kwa Wazazi wake akaanzishe familia yake mwenyewe.

◼️Hakikisha Mwanamume unakuwa Mume wa namna hiyo, anzisha familia Yako.
Kama unaishi kwa Wakwe zako au kwenu  usiridhike Anza mipango ya kuishi na familia Yako mwenyewe.


6. Uwe mtu wa kuwarudi watoto wako.

Kumbu 8:5 "Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo BWANA, Mungu wako, akurudivyo."

◼️Kuwarudi Watoto wako maana yake wakikosea wasamehe na kuwaelekeza upya ili waendelee kumcha MUNGU na wafanya mambo mazuri uyatakayo.

◼️Kuna Watoto wengi Leo wanatembea kwenye laana ya Wazazi wao kwa sababu wazazi hao hawana tabia ya kuwarudi Watoto wao.

◼️Mtoto akikosea muonye na hata kumpa adhabu ndoto iwapasao Watoto ili tu asirudie kufanya makosa, ila msamehe ili aendelee kufanya mambo mazuri mbele za MUNGU na mbele za Wanadamu.

◼️Usimlee Mtoto wako kama Mayai maana yai likipasuka huwezi kulitengeneza, mlee Mtoto wako wa kiume, mlee kama Mwanaume ili akue kama Mwanaume Mcha MUNGU na abaki kama Mwanaume daima katika Maisha yake yote.

7. Usimwache Mkeo.

1 Wakorintho 7:11 "lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe."

◼️MUNGU hataki wanandoa waachane na hata ikitokea wameachana hawatakiwi kuingia kwenye Ndoa nyingine, hivyo hakuna haja ya kumuuacha mkeo kama unajua huna ruhusa ya MUNGU ya kuoa Mke Mwingine.


8. Hakikisha unakuwa Mume wa Mke mmoja tu.

Tito 1:6 "ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii."

◼️Mbele za MUNGU Mwanaume wa mke mmoja ndio hutambulika, na tangu Mwanzo MUNGU aliumba Ndoa ya Mke mmoja kwa Mume mmoja tu, sio zaidi ya hapo.

Marko 10:6-8 " Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja."

◼️MUNGU hakuumba Mume mmoja kwa wake zaidi ya mmoja Wala hakuumba Mke mmoja kwa Waume wengi lakini kama maandiko yanavyosema hapo ni kwamba MUNGU aliumba Ndoa ya Mke mmoja kwa Mume mmoja na sio zaidi ya hapo.

◼️Mwanaume Hakikisha unakuwa katika Ndoa ya Mke mmoja tu.
Usiishi kwenye uongo wa wapinga KRISTO.


9. Usimtamani Mwanamke mwingine nje na Mke wako.

Mathayo 5:28 "lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake."

◼️Biblia inakataza kumtamani Mwanamke asiye Mke Wako.
Shika kanuni hii ya Neno la MUNGU Wewe Mwanaume.

◼️◼️Zingatia kumtamani mkeo wa Ndoa tu na sio vinginevyo.


10. Tambua kwamba maombi yako kwa MUNGU kuna wakati hayawezi kujibiwa kamwe kama utakuwa unamuonea Mke Wako.

1 Petro 3:7 "Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."

◼️Usimuonee Mkeo ili Maombi Yako yasizuiliwe, zingatia hiyo daima.
Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments