![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibuni Tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Inawezekana kabisa kutokea kwamba katika wakati fulani katika Kundi fulani pakawa hakuna Kiongozi.
Waamuzi 18:1 "Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila ya Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hata siku hiyo urithi wao haujawaangukia kati ya kabila za Israeli."
◼️Kiongozi mzuri anayemcha MUNGU katika KRISTO YESU ni Mtu wa Muhimu sana katika Kundi au Kanisa.
Waamuzi 5:2 "Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini BWANA.''
➡️Tunachoangalia Leo mambo gani yatatokea ikiwa hakuna Kiongozi.
Ngoja nianze na ushuhuda huu.
Rafiki yangu mmoja ambaye yupo Kanisa fulani katika Kijijini Mkoa fulani siku Moja alinisimulia mambo ambayo ilibidi nimshauri yeye ndio awe Kiongozi katika Kanisa hilo ambalo Mchungaji alilikimbia na hakuwa ameweka Viongozi watakaochukua nafasi yake baada ya kukimbia.
Nilimwambia rafiki huyu achukue nafasi ya uongozi hadi Askofu atakapokuja ili Sasa uanze utaratibu wa kupata Mchungaji wa kudumu, hata namba za Askofu aliyekuwa nazo ni Mchungaji Pekee katika Kanisa la Washirika zaidi ya 50 hivyo hawakujua wafanyeje.
Kisa kilianzia wapi hadi Mchungaji akakimbia?
Mchungaji yule alikuwa anachunga Kanisa hilo hapo Kijijini bila tatizo na kazi ya MUNGU ilikuwa inaendelea vizuri kabisa, alishuhudia watu mitaani na akawa na bidii katika Injili ya KRISTO hivyo watu wengi wakaokoka na kujiunga na Kanisa.
Mchungaji baadae akasikia Kuna sehemu ya kazi Ina maslahi makubwa hivyo ghafla tu akatangaza anahama mkoa huyo na kwenda mkoa wa mbali, hapo hapo akaondoka.
Wakati anahama ghafla Kanisa lilikuwa na washirika zaidi ya 50 na hakuwa ameweka Viongozi wasaidizi na wakati anahama ilikuwa siku ya jumanne na jumatano jioni Kuna Ibada Kanisani hapo.
Jumatano ilipofika watu wengi walikuja Kanisani Ibadani wakiwa hawajui kama Mchungaji hayupo, watu wale wakafungua Ibada kwa Maombi, wakaimba nyimbo za kumsifu na kuabudu MUNGU Kisha wakakaa wakisubiri Mhubiri apande madhabahuni kufundisha Neno la MUNGU na Kwa sababu Mhubiri wa kudumu alikuwa ni Mchungaji walijua yupo. Wakiwa wanaangaliana muda ukaenda ikabidi watawanyike kwenda majumbani kwao.
Hali ile iliendelea kwa wiki kadhaa na watu hawakuacha kuja Ibadani ila wakifika ni kuomba na kuomba Mhubiri haonekani.
Ndipo rafiki huyu akanipigia simu na kunieleza wafanyeje, nikamwambia awakusanye wote na awe anawafundisha Neno la MUNGU, yeye akasema ni sio mzoefu na hakuwa na uwezo wa kuandaa Neno la MUNGU na kuhubiri, nikawa namtumia masomo yangu na MUNGU akawapa Neema Kanisa lile watu wakawa wengi na nguvu za MUNGU zikawa zinaonekana.
Rafiki huyu alilazimika kuwa Mchungaji na Kiongozi kwa sababu Kundi likikimbiwa na Kiongozi, alifanya hivyo kwa muda mrefu, zaidi ya Miaka 2.
➡️Rafiki ulishawahi kujiuliza Mchungaji ghafla Kanisani akiondoka itakuwaje?
➡️Ulishawahi kujiuliza Kanisa likiwa bila Mchungaji litakuwaje?
➡️Ulishawahi kujiuliza Idara ya Vijana au Idara ya Wanawake Kanisani zikiwa hazina Viongozi itakuwaje?
◾Hapa chini ni mambo yanayoweza kutokea ikiwa Kundi fulani halina Kiongozi.
1. Kundi kama halina Kiongozi Kila Mtu atajifanyia yale anayoona yanafaa machoni pake yeye hata kama mengine ni mabaya.
Waamuzi 17:6 "Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe."
◼️Kama hakuna Kiongozi utaratibu mzuri unakuwa haupo na Kunakuwa na vurugu na migongano ya mara kwa mara na hakuna Mtu wa kusuruhisha.
2. Kama hakuna Kiongozi ni rahisi Kundi kujichagulia Kiongozi hata ambaye sio sahihi kiroho au kujichagulia Kiongozi aliye kinyume na KRISTO YESU Mwokozi.
➡️Mfano hai Waisraeli walipokaa muda wa siku kadhaa bila Musa ambaye alikuwa Kiongozi wao wakajichagulia miungu ndio iwe Kiongozi wao.
Kutoka 32:1 "Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata."
➡️Hawa aliona Musa amechelewa kurudi kutoka mlimani wakaona kama Musa amechelewa kurudi katika nafasi yake ya uongozi kwa ujinga sana wakachagua miungu iwaongoze.
◼️Kama Kundi likiwa halina Kiongozi ni rahisi watu wale kujichagulia hata Kiongozi asiyefaa.
3. Kama hakuna Kiongozi ni rahisi kuibuka migogoro baina yenu na mnapopishana au kukosana huwa hakuna msuluhishi au hakuna mpatanishi.
Yakobo 4:1 "Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?"
◼️Kama Kiongozi hayupo hakuna Mtu wa kuwaweka sawa watu waliokosana katika Kundi.
4. Kama kundi linapokuwa halina Kiongozi ni rahisi mno watu wale kukengeuka , kwenda kimwili na kuliacha kusudi Takatifu la MUNGU katika KRISTO YESU.
➡️Mfano hai ni Waisraeli ambao walikengeuka maana Kiongozi wao Musa alikuwa hayupo.
Kutoka 32:23 "Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata."
◼️Kama Musa angekuwepo hawa Waisraeli wasingeabudu Ndama ya dhahabu iliyotengenezwa kwa hereni na pete Zenye miungu ya Misri, maana vitu hivyo ni rahisi kuwa na roho ya miungu nyuma yake.
◼️Musa angekuwepo wasingetengeneza Kiongozi mpya wa ajabu ambaye ni miungu ya hereni na pete.
Mambo Muhimu ya kufanya kwa ujumla wake.
1. Ukiwa Kiongozi sahihi wa kiroho Hakikisha unaandaa Watu wanaoweza kufanya kazi nzuri ya MUNGU wakati utakapokuwa haupo.
◼️Mfano hai ni huu Eliya katika nafasi yake ya kiuongozi aliambiwa amwandae Elisha ambaye atachukua nafasi yake kipindi akiondoka Duniani.
1 Wafalme 19:15-16 " BWANA
akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako."
◼️Uongozi wa kiroho kwa Elisha haukuuanza hadi Eliya alipoondoka Duniani.
◼️Kiongozi kama kweli unaitakia mema kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU ni Muhimu sana kuandaa watu ambao wanaweza kufanya kazi ya MUNGU hata wakati Wewe haupo.
Nimewahi kushuhudia Kanisa Moja likitawanyika na eneo la Kanisa kugeuzwa Kwa kazi nyingine baada ya Mchungaji kuondoka.
◼️Sasa Ina maana gani umemtengenezea Bwana YESU KRISTO Wateule wake wengi Kisha ukiondoka wote wanarudi Duniani?
Kazi yako ya kujionea fahari mbele ya MUNGU ni ipi Sasa hapo?
1 Wathesalonike 2:19 "Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji ya kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu YESU, wakati wa kuja kwake?"
◼️Kiongozi andaa Mtu akayechukua nafasi Yako Kipindi haupo, umesafiri kwa dharula ,umesafiri kihuduma muda mrefu, au umesafiri kifamilia muda mrefu, umepata dharula ya Maisha au hata umeondoka Duniani.
2. Andaa Mtu atakayechukia nafasi Ukiwa haupo na mtambulishe kwa Kundi.
Hesabu 27:18-21 " BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia."
◼️Hii ya kuandaa Mtu ni nzuri sana wa kuchukua nafasi kiuongozi kama Wewe Kiongozi hutakuwepo.
Nakumbuka siku Moja mwaka kama sio 2010 basi 2011 nikiwa Zanzibar Mchungaji wetu alisafiri kihuduma kwenda Uganda mwezi mzima, kabla hajaondoka aliniita Mimi na rafiki yangu mmoja mbele ya Kanisa jumapili akasema "Mimi naondoka naenda kwenye huduma Uganda, Kanisa nalikabidhi kwa hawa Watumishi, jambo lolote linalomhusu Mchungaji au Uongozi wa Kanisa waambie hawa"
Niliogopa na kuwaza sana na kufikiri sana baada ya hapo, na kweli akiwa hayupo kulitokea majukumu ya kichungaji tuliyafanya hadi aliporudi.
➡️Viongozi wa namna hii ni wachache sana maana Viongozi wengi wakiondoka Kanisa huliacha mikononi mwa Mama Mchungaji hata kama Yuko mbali na Kanisa na hana utumishi ndani yake au Uongozi ndani yake.
➡️Sio Mama Wachungaji wote wanaweza kuwa Viongozi wazuri, Mama Wachungaji wengine hawakuitiwa uchungaji.
Baadhi ya Mama Wachungaji ni washirika wazuri sana Kanisani, waombaji na watu Muhimu Kanisani lakini hawakupewa kuwa Viongozi wa kiroho hivyo Mchungaji ni vyema apambanue ili kuliacha Kundi katika hali nzuri.
Kwa Wachungaji wengi kushindwa kuandaa watu akiondoka anamwachia Kanisa Mama Wachungaji inapelekea Mchungaji akisafiri muda mrefu na washirika nao wanasafiri kiakili hivyo hata Kanisani hawaji hadi Mchungaji arudi.
➡️Je unadhani watu kama hao wakati Mchungaji hayupo wakikutana na Watumishi walio mawakala wa shetani itakuwaje?, watapandikizwa mambo mabaya ambayo yanaweza kuja hata kulivuruga Kanisa baadae.
3. Kiongozi Mkuu ni ROHO MTAKATIFU hivyo inapotokea ghafla kwenye Kundi lenu hakuna Kiongozi Ombeni kwa MUNGU na sio kwenda kimwili ili kupata Kiongozi sahihi.
Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."
4. Katika Maisha Kila Mtu awe Kiongozi au asiwe Kiongozi, Kiongozi wa Sasa au Kiongozi wa baadae ni Muhimu sana kumtegemea MUNGU kwanza na sio Wanadamu.
Mika 7:5 "Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari."
◼️Kivyovyote vile Usikubali MUNGU akachukia nafasi ya Mwanadamu katika Maisha Yako.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments