MUNGU AAMUE KATI YANGU MIMI NA WEWE.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

1 Samweli 24:12" BWANA atuamue, mimi na wewe, na BWANA anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako."

◼️Haya ni Maneno ya Mtu aliyekuwa anatafutwa muda mrefu ili auawe.
Maneno hayo yana maana kwamba "MUNGU ATUAMUE MIMI NA WEWE"

◼️Huyu ni Daudi ambaye bila kosa lolote alikuwa anatafutwa kuuawa na Mfalme Sauli na alikuwa amekoswa kuawa mara kadhaa.

1 Samweli 18:11 "Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili."

◼️Huyu ni Daudi ambaye bila kosa aliundiwa Kundi la Askari ili wamtafute na kuhakikisha wamemuua bila hatia yeyote.

1 Samweli 19:1 "Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi."

◼️Maneno haya ni ya Mtu aliyelazimika kutoroka kwao pazuri na kwenda kuishi uhamishoni na  akikwepa kuuawa na Mfalme.

1 Samweli 22:1 "Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko."

◼️Haya ni Maneno ya Mtu  ambaye hakuwa na chuki na Mtu ila mfalme anamtafuta amuue akaamua kukimbilia kwa Mtumishi wa MUNGU na ikabidi yeye na Mtumishi wa MUNGU baadae wakimbie Tena wote kwenda kuishi eneo lingine, na Kumbuka Mtumishi huyu anayekimbia ndiye aliyemwapisha Mfalme ili kuchukua Ufalme wake.

1 Samweli 19:18 "Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi."

◼️Haya ni maneno ya Mtu ambaye wakati Mwingine alilazimika kuishi katika Mashamba na kujificha katika mapango baada ya kumkimbia Mfalme aliyetaka kumuua kwa wivu tu bila kosa lolote.

1 Samweli 20:24 "Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula."

◼️◼️MUNGU ATUAMUE MIMI NA WEWE, Ni maneno ya Mtu aliyeonewa wivu na Mfalme bila kosa lolote.

1 Samweli 18:9 "Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile."

➡️Kweli nimeamini Kuna watu wana Neema kubwa, Wana Nyota Kali na kibali kikuu hadi wanaonewa wivu na Mkuu wa Nchi, hii ni ajabu.
Yaani Kijana Mchunga Ng'ombe ,Kondoo na mbuzi anaonewa wivu na Mkuu wa Nchi yake.

◼️Daudi alitafutwa Kila mahali ili auawe bila kosa lolote, wakati Mwingine Mfalme alitumia Wanajeshi elfu Moja ili tu ampate Daudi na kumuua lakini haikuwezekana kwa sababu MUNGU wa Mbinguni alimlinda.

1 Samweli 24:1 "Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu."

◼️Kwa sababu ya chuki ya Mfalme kwa Mtu asiye na hatia MUNGU wa Mbinguni akawa upande wa Kijana asiye na hatia na siku Moja ya ajabu Mfalme bila kujua akaingia katika mtego wa kufanywa lolote na Kijana huyo lakini Kijana huyo hakumfanya lolote.

1 Samweli 24:3 "Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana."

◼️Daudi alikuwa na Nafasi ya kumuua Sauli lakini Daudi Akamwambia tu Sauli Neno gumu sana kwamba "MUNGU ATUAMUE MIMI NA WEWE " na kilichofuata baada ya pale ni kitu kibaya sana kwa Mfalme.

➡️Mfalme na nyumba yake yote wakafa, yaani Ukoo aliouanzisha Sauli ukaisha wote isipokuwa mjukuu wake mmoja kilema Jina lake Mefiboshethi ndio akabaki hai.

2 Samweli 9:13 "Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula sikuzote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili."

◼️Na Kumbuka  aliyemaliza familia nzima ya Sauli sio Daudi, hata alipokufa Sauli Daudi Wala hakufurahi Bali aliumia ila kisasi Cha MUNGU ndicho kilifanya kazi kwa sababu ya makosa ya Sauli.

◼️Daudi hakutaka kulipa kisasi mwenyewe Bali alimkabidhi MUNGU kisasi chake na MUNGU akamlipia kisasi hicho.

1 Samweli 24:12" BWANA atuamue, mimi na wewe, na BWANA anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako."

◼️Neno hili "MUNGU AAMUE KATI YANGU MIMI NA WEWE" ni Neno gumu sana, Mimi Peter Mabula nasema hivyo kwa sababu nimewahi katika Maisha yangu kuiona Nguvu ya MUNGU kupitia Neno hilo, hata Leo usiku Kuna kitu nimeona ndio nikakuletea somo hili.

➡️Leo usiku kabla sijakuandalia somo hili niliota Ndoto, katika Ndoto hiyo niliona Mama mmoja ambaye alikuwa anamdai Baba mmoja pesa millioni Moja ya Tanzania, Baba yule akaamua kumdhulumu yule Mama, katika ndoto hiyo Mimi nilikuwa kama mtazamaji ambaye naona Matukio yote ila wao hawanioni, Mama yule baada ya kugundua amedhulumiwa Akamwambia yule Baba kwamba "MUNGU aamuae kati yangu Mimi na Wewe" baada ya pale nikaona yule Baba akaenda kukopa sehemu nyingine pesa na kupewa nyingi zaidi ya milioni 9 lakini alipochelewesha kulipa nikaona wale wanaomdai wanauza nyumba yake ambayo ilikuwa kubwa sana na Ina eneo zaidi ya heka, akawa hana hata pa Kuishi, Mimi kwa Sauti ndani ya Ndoto nikasema "Inawezekanaje huyu Mtu awe hana pa Kuishi wakati alikuwa na nyumba nzuri kama pa Waziri?" Ndoto ikaishia hapo.

➡️Licha ya hayo Neno hilo katika Maisha yangu nimewahi kulitumia kwa watu wawili tofauti walionitukana sana kutokana na Masomo yangu ya Neno la MUNGU ambayo ninapost Kila siku Mtandaoni na niliona matokeo mabaya kwa wahusika ngoja nikuelezee kuhusu mmoja wao.

➡️Mtu huyo alikuwa Mtu maarufu kidogo Mtandaoni ambaye Kila akiona somo langu nimepost anaenda kwenye comments ananitukana kwa maneno mengi, alifanya hivyo kwa muda mrefu nikawa simjibu ila najisikia vibaya.

Nikawa nawaza kibinadamu kwamba " Yaani naandika somo hata masaa 8 somo Moja ili watu wafunguliwe na kumpokea YESU KRISTO lakini huyu kama huwa ananivizia Kila nikiweka tu somo yeye wa kwanza kwenye comment na Kwa kunitukana"

Siku Moja alipofanya hivyo nikataka nimjibu Kwa ukali lakini nikawa naandika ile nataka kupost mara naacha lakini ghafla moyoni mwangu ukaja ujumbe huu "MUNGU wa Mbinguni aamue kati yangu Mimi na Wewe"

Hayo ndio yalikuwa majibu yangu siku hiyo baada ya kunitukana Mtu huyo.

Baada ya kuandika hivyo sikumuona Tena Mtandaoni Mtu huyo tangu wakati huo hadi Leo zaidi ya miaka 12, kwa sababu matusi yake yalikuwa mabaya na ya kudhalilisha, Kuna wakati nilikuwa nakumbuka na ku search mitandaoni sikuwahi kumwona, kisasi Cha MUNGU ni kibaya sana.

Kwanini nimekuletea Neno hili?

◼️Najua watu wataabishaji wapo wengi hata katika Maisha Yako Wewe mwenye haki unayeishi Maisha Matakatifu katika KRISTO YESU Mwokozi;
Mfano Mtu anakuonea bila kosa, amekufukuzisha kazi kwa boss kwa kupeleleka uongo uliofanyiwa kazi, anaonewa familia yenu, amewadhulumu au Mtu anawatishia kuwaua bila hatia.

Ndugu fanyia kazi ujumbe huu na utamuona MUNGU wa Mbinguni.
Fanya kama yanayosema katika andiko hili ukimweleza kwa Kinywa chako huyo anqyekutaabisha bila kukosea.

1 Samweli 24:15 "Basi BWANA atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako."

◼️Wewe usibebe chuki kwa waliokuudhi, Wala usiwapangie mabaya, Wewe mkabidhi MUNGU kisasi chako Kisha endelea kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi, Ishi kwa upendo, amani Utakatifu na utaona MUNGU atakachokifanya.

Warumi 12:19 "Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA."

◼️Kilichotokea kwa Sauli kwa kumuonea Daudi bila kosa ni fundisho kwa waonezi wote katika miji au mitaa n.k

◼️MUNGU anaweza akaamua kati yako na huyo Mtu mwenye Nguvu sana anayekunyanyasa, Wewe ambaye unanyanyaswa, kisasi Cha MUNGU ni kibaya sana.

1 Wathesalonike 4:6 "Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu BWANA ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana."

◼️Tunajifunza kwamba usilipe kisasi Wewe Bali mkabidhi MUNGU kisasi chako kama Daudi na MUNGU atakulipizia kisasi hicho kwa Mtu huyo anayekutesa au kukuonea.

◼️Kumbuka ukilipa kisasi Wewe kimwili ni dhambi hivyo usilipe kisasi ila mkabidhi MUNGU atakulipizia kisasi kwa uzito hata kuliko ambao ungelipa Wewe, pona ya Mtu huyo ni labda tu kama atamua kumpokea YESU KRISTO kama  Mwokozi wake na kuokoka ndipo atasalimika na kisasi Cha MUNGU hiyo haitakusumbua Wewe maana MUNGU atakubariki na kukupa furaha pia.

◼️Kuna watu wanapitia mazingira magumu sana kwa sababu za kuonewa, Ndugu ujumbe huu unakuhusu usilipe kisasi Bali mkabidhi MUNGU kisasi chako Kisha endelea kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.

Kumbu 32:35 "Kisasi ni changu mimi, na kulipa, Wakati itakapoteleza miguu yao; Maana siku ya msiba wao imekaribia, Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka."

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe



Comments