![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️MUNGU anaweza kuingilia Mamlaka yeyote Duniani na kubadilisha Uongozi au kuufuta Uongozi.
◼️MUNGU anaweza kuingilia cheo chochote Cha Mtu na kumtoa mhusika Kisha kumweka Mtu Mwingine.
◼️Kwa ujumla tu Kila aliyeko kwenye Uongozi au utawala katika nafasi fulani akiwa mtenda mema, huyo huyo anatawala kwa msaada wa MUNGU.
Mithali 8:16 "Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia."
◼️Kwa sababu MUNGU ni MUNGU wa wote wenye mwili anaweza kufanya maamuzi ya namna yeyote kama atakavyopenda yeye wakati wowote.
Yeremia 32:27 "Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?"
◼️MUNGU anaweza kufanya maamuzi yeyote wakati wowote, anaweza hata kumtoa Mtu katika madaraka fulani na kumweka Mtu Mwingine vile atakavyo yeye MUNGU.
Ngoja tuangalie mifano hii.
1. MUNGU alimtoa Sauli kwenye ukuu wa Nchi akamweka Daudi.
1 Samweli 13:14" Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru."
◼️Haijalishi Sauli alikuwa ameweka mizizi kiasi gani katika serikali ili kubaki madarakani miaka yote lakini MUNGU alipotaka kumbadilisha alimbadilisha maana MUNGU anaweza kumtoa Mtu katika madaraka fulani na kumweka Mtu Mwingine.
◼️Sababu ya Sauli kuondolewa katika Uongozi na MUNGU ni makosa yake mabaya mbele za MUNGU.
1 Samweli 15:17-19 " Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.
Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA?"
2. MUNGU alimtoa Eliya katika Nafasi ya Unabii katika Taifa na kumpa Elisha.
1 Wafalme 19:15-16 " BWANA akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako."
◼️Sababu za MUNGU kumtoa Eliya katika Nafasi hiyo ni kwamba Muda wa Eliya kukaa Duniani ulikuwa umeisha hata kama hakuwa mzee sana.
2 Wafalme 2:5" Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni."
◼️Kuna Watumishi wa MUNGU huwa hawaamini kama muda wao umeisha hata hawamuombi MUNGU juu ya watu watakaochukua nafasi yao ya utumishi ili wawaweke tayari kuchukua nafasi wakati wakiondoka wao, hivyo Watumishi Hawa wakiondoka huacha migogoro.
◼️Wewe Mtumishi mwaminifu wa Bwana YESU KRISTO ambaye umetumika miaka mingi sana ROHO MTAKATIFU akikupa Neema andaa watu aliokuambia ambao watachukua nafasi Yako ili Injili iendelee kwenda mbele hata wakati Wewe haupo.
3. Vashti alipisha nafasi ya Umalikia kwa Esta kwa Sababu ya Wokovu wa Israeli.
Esta 1:12 "Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake."
◼️Chanzo Cha vashti kuondolewa katika nafasi ni sherehe tu ya Kawaida ambayo ilifanyika Kisha yeye kuitwa na mfalme akakataa.
Esta 2:17 "Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti."
◼️Hii ikapelekea Mfalme kuchagua Mke Mwingine ambaye ni Esta lakini nyuma ya Esta kuchukua nafasi ya Vashti kulikuwa na kusudi la MUNGU.
Esta 4:14 "Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?"
◼️Kumbe Esta aliujilia Ufalme kwa ajili ili awe msaada wa Waisraeli katika kipindi hicho na ikawa hivyo maana aliyetaka kuwaua akafa yeye Waisraeli wakapona.
Esta 8:17 "Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia."
◼️Taratibu za kibinadamu za Wakati ule wa akina Vashti na Esta ziliruhusu Talaka hivyo MUNGU akapitishia kusudi lake kwa kutumia kamba za kibinadamu maana wakati Mwingine MUNGU hutumia kamba za kibinadamu kutimiza kusudi lake.
Hosea 11:4 "Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao."
◼️Kwa sasa talaka hairuhusiwi, ni kifo tu ndio kinaweza kuwatenganisha Wana Ndoa.
Marko 10:6-9 " Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.
Basi alichokiunganisha MUNGU, mwanadamu asikitenganishe."
◼️MUNGU wa Mbinguni anaweza kumbadilisha Mtu yeyote katika nafasi aliyopo na kumweka Mwingine.
◼️Ndugu, uliye na cheo, nafasi au madaraka Ishi vizuri na watu wote maana mwamuzi ni MUNGU anaweza kuamua vyovyote atakavyo wakati wowote.
◼️Na njia za MUNGU kumtoa Mtu katika nafasi yake na kumpa Mwingine Ziko nyingi, Kuna watu hufa kumbe ili wapishe Nafasi Mfano ni Sauli.
◼️Kuna watu njia zao za kubadilishwa ni kufukuzwa kama Vashti ili tu kupisha nafasi kwa Mtu aliyekusudiwa na MUNGU.
◼️Ndugu ujumbe wa Leo ni ili kukufanya uendelee kumcha MUNGU katika KRISTO YESU hata kama una madaraka makubwa sana na utajiri mkubwa.
1 Timotheo 6:17-19 " Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini MUNGU atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.
Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli."
◼️Usijivunie kazi Bali Mche MUNGU ambaye ana uwezo wa kukuondoa katika nafasi hiyo muda wowote.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments