![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Tunamfahamu zamani Kulikuwa na Manabii ambao MUNGU aliwatumia kwa kazi yake, na Manabii hawa hawakuhitaji kujiita "Nabii" ila Watu wote waliwajua kwamba ni "Manabii" kwa sababu ya kazi zao.
Mfano
1 Samweli 3:20-21 " Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa BWANA. Naye BWANA akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa BWANA akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la BWANA. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote."
◼️Lakini pia Leo Kuna Manabii wa MUNGU ambao MUNGU amewaweka katika Kanisa ili waifanye kazi ya Injili ya KRISTO kupitia huduma yao ya Unabii.
Waefeso 4:11-12 " Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe;"
➡️Lakini pia Biblia Iko wazi sana kwamba ingawa Manabii wa kweli wapo lakini pia Manabii wa uongo ni wengi.
Mathayo 7:15-16 " Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?"
➡️Zamani Watu hawakushughulika sana na Manabii wa uongo maana waliwajua mapema kutokana na kazi zao lakini Leo Manabii wa uongo ni wengi kuliko Manabii wa kweli.
➡️Kipimo Cha kwanza Cha Nabii wa Uongo ni kusema jambo kwamba litatokea Kisha lisitokee.
Yeremia 14:14 "Ndipo BWANA akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao."
➡️Inafikia hatua Leo hata Nabii wa kweli anaitwa Nabii wa Uongo kwa sababu sehemu kubwa zaidi ya manabii Leo ni waongo na wasanii tu.
➡️Lakini pia wapo Leo Manabii wa kweli kabisa lakini kwa kuiga na kufuata mkumbo wametoka kwenye kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU na hii inaongeza kusemwa vibaya kwa huduma ya Kinabii.
Hebu ngoja tupitie tafakari hizi ili Ndugu unielewe.
◼️Manabii wote wa kwenye Biblia walikuwa wanatoa unabii wenye uelekeo wa watu kutubu na kumrudia MUNGU au kutengeneza na MUNGU.
➡️Manabii wa Leo wengi zaidi na inawezekana ni wote unabii wao wanaoutoa ni kuhusu tu mafanikio ya kimwili.
Kama ni hivyo hakika kuna pahali hakuko sawa katika Kanisa la MUNGU.
Wagalatia siku moja waliambiwa ni nani aliyewaroga?
Wagalatia 3:1 "Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao YESU KRISTO aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?"
Inavyoelekea sana itafikia hatua ya Kanisa la Leo kuambiwa ni nani aliyewaroga?
➡️Leo kuna manabii mfano mtandaoni huku jumbe zao ni za kusema tu " Watu 100 wa kwanza Ku like post hii watapata pesa nyingi mwezi huu
" Mara "Andika Amen ili upate upako" andika "Napokea ndio utapata kibali na Mali"
Hayo ni maneno laini yadanganyayo.
Isaya 30:10 "wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;"
➡️Hii ndio tofauti kubwa sana kati ya Manabii wa Biblia na manabii wa sasa.
◼️Hebu ona Nabii Isaya kama sehemu ya manabii wa Biblia anasema Isaya 1:16-17 " Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane."
➡️Nabii wa Leo hata unaweza kumfuatilia mwaka mzima na usimuone popote anaongoza watu sala ya toba au anakemea dhambi.
Hebu ndugu niambie kwa Mara ya mwisho ulimsikia lini Nabii katika Kanisa la Leo analionya Kanisa juu ya uzinzi na uasherati au analionya Kanisa juu ya dhambi?
Ni Manabii wachache sana wanaofanya hivi.
Hakika kama ni hivi hakuko sawa katika Kanisa la MUNGU.
◼️Hadi nakuletea ujumbe huu mfupi nimepitia Biblia na kuona manabii karibia wote na ujumbe wao ulikuwa na lengo la kutaka watu watubu na wamgeukie MUNGU huku wakiwa wakamilifu.
➡️Nabii wa Leo anakuambia tu "pokea gari" hata kama wewe ni mzinzi na unaisaliti ndoa yako.
Hakika hakuko sawa katika Kanisa wakati huu kama watu wako busy tu na kutabiriwa uongo.
◼️Ndugu, YESU KRISTO anaokoa, ukimwamini Leo na kutubu dhambi na kuziacha, hakika unaokoka.
Bwana YESU KRISTO ambaye ndio mwenye Kanisa la waenda Mbinguni anasema tuwapime Manabii na Kwa kazi zao tutajua tu kama ni Manabii wake au Manabii wa shetani.
Mathayo 7:20-21" Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni."
◼️Ndugu, jitenge mbali na Nabii wa Uongo.
◼️Usifanyie kazi maelekezo ya uongo ya Nabii wa Uongo.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments