![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Kujifunza Neno la MUNGU lakini kutoka kwenye maoni yangu binafsi.
Nasema Tena ni Maoni yangu binafsi kama Peter Mabula juu ya watu kutengwa Kanisani.
◾Kabla sijasema Maoni yangu ni kwamba nimewahi kushuhudia watu kadhaa wakitengwa katika Makanisa niliyokuwa naabudu yaani nilipokuwa naishi Zanzibar niliona watu wakitengwa na hata nilipohamia Dar es salaam nilishuhudia pia watu kadhaa wakitengwa.
◾Binafsi nililidhika na wote waliotengwa na Kanisa na maamuzi Yale yalikuwa na faida kwa wahusika na Kwa Kanisa.
Mfano hai nilishuhudia Dada mmoja ambaye tulikuwa tunaimba nae kwaya na alikuwa mwimbishaji mzuri sana na Kiongozi wa Ibada, Kuna wakati alionywa na Viongozi wa Kanisa juu ya uasherati maana Kuna watu walimuona katika mazingira mabaya na yeye akakiri.
Baadae akaendelea na tabia hiyo na kupata mimba ambayo hata kuitoa hakuweza maana Mtumishi wa MUNGU Mmoja alimwambia "kwa sababu umeonywa sana wakati huu ukizini utapata mimba na haitatoka" ni kweli miezi mingi baadae alizini na kupata mimba hivyo ikapelekea kutengwa miezi 6.
Wakati wa kutengwa kwake miezi 6 alipewa na Kanisa masharti haya;
1. Kila Ibada ahudhurie bila kukosa katikati ya wiki na jumapili.
2. Kanisani akae kwenye benchi nyuma ya Kanisa na aliwekewa benchi lake, hairuhusiwi kwenda mbele ya Kanisa Wala kusimama eneo la madhabahuni hapo Kanisani.
3. Huduma zote alizokuwa anazifanya Kanisa aache yaani aache kuimba kwaya, kuongoza Ibada, n.k
4. Uongozi aliokuwa nao Kanisani kwenye Idara ya Vijana na kwaya aliondolewa Uongozi huo.
5. Hairuhusiwi kushika mic,kutoa ushuhuda au kueleza lolote mbele ya Kanisa Kanisani.
6. Akakikishe anasoma sana Biblia ili ajifunze kumcha MUNGU wa Mbinguni.
7. Akiendelea na dhambi atafutiwa ushirika na Kanisa yaani Kanisa litamhesabu kama Mtu wa mataifa hadi miezi 6 ipite.
8. Akionyesha utii na kumcha MUNGU kifungo chake kitafutwa hata kabla ya kufikisha miezi 6.
➡️Mimi baada ya kuisikia hukumu hiyo niliona ni sawa maana baada ya Tangazo hilo kwa Mtu huyo Wana Kanisa waliotaka kuhama Kanisa kama Kanisa halichukui hatua kukemea dhambi ya uzinzi kwa vitendo kwa Mtu huyo ambaye wameshamuona mara nyingi, watu hao hawakuhama Tena Kanisa.
➡️Watu wa nje ya Kanisa ambao walikuwa wanalitukana Kanisa kwamba wao na Kanisa ni ngoma droo kwa sababu ya uasherati wa Mtu mmoja, watu hao walipojua hatua Kanisa limechukua hatua gani hawakulitukana Tena Kanisa.
➡️Ingekuwa aibu sana na ajabu Dada yule kuendelea na kuimba Kwaya au kuongoza Ibada akiwa na mimba yake ambayo watu wote wanajua chanzo ni dhambi ya uasherati, wachanga kiroho wangeona ni kawaida tu kukosea maana unakosea Kisha unaendelea na huduma hamna tatizo, ingekuwa rahisi kwao kuikimbilia dhambi maana ushawishi wa nje juu ya dhambi hiyo ni mkubwa.
◾Sasa hapa chini ndio Maono yangu juu ya Kanisa kutenga watu.
◼️Ni vizuri kutenga watu ndani ya Kanisa kwa baadhi ya dhambi hasa dhambi Zenye madhara kwa Kundi na mhusika huzifanya mara kwa mara hata kama anaonywa yeye haachi maana pia Mtu mmoja anaweza kusababisha Kanisa Zima kutukanwa.
1 Wakorintho 5:6 "Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima?"
◼️Ila Sasa wanaostahili kutengwa sio Waamini wapya Bali ni hawa chini wakitenda dhambi zinazofedhehesha Kanisa na za mara kwa mara.
1 Wakorintho 5:1-2 " Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo."
◼️Kuna watu kwa dhambi za mwendelezo hasa uzinzi wanazifanya Kila mara miaka yote hadi wanaweza kutenga vibaya na Kanisa.
1 Wakorintho 5:5 "kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana YESU."
◼️Ninajua hadi Kanisa limtenge Mtu huwa sio Kwa kosa la mara ya kwanza tu au kosa la siku Moja ila sehemu kubwa ambao hutengwa ni kwa makosa mabaya endelevu.
Bwana YESU alitoa kanuni za wakosaji kwamba inabidi wapitie hatua 3 hatua kama wakiendelea na makosa yao mabaya hatua ya 4 ni kufutiwa ushirika na Kanisa yaani wanakuwa wapagani au wanahesabiwa Wapagani.
Mathayo 18:15-17 " Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo.
La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru."
Hatua hizi 4 ni hizi;
1. Wewe peke Yako kumuonya juu ya dhambi yake akiacha umefanikiwa hivyo huhitaji kamwe kawenda hatua ya pili.
✔️✔️Zingatia sana hii
Mtu akiendelea na Uovu wake baada ya Wewe Pekee Yako kumuonya nenda hatua ya pili, asiposikia nenda hatua ya 3 ambayo inahusu Kanisa Zima na asipoacha Uovu huo Kanisa linaingia hatua ya 4.
2. Wewe na Mtu mmoja au wawili au watatu mnaenda pamoja kumuonya kutokana na Uovu wake mbaya
3. Kanisa Zima kuhusika kuonya Mtu huyo ili aache Uovu wake.
➡️Kanisa Zima maana yake Viongozi wa Kanisa kuchukua hatua ikiwemo hata Mtu kutengwa kwa muda
4. Hatua ya 4 ni Mtu huyo kuhesabiwa kama mpagani.
◼️Sasa sehemu kubwa kwa maoni yangu wanaopaswa kutengwa wakifanya dhambi zinazofedhehesha Kanisa za mwendelezo ni hawa
1. Mchungaji au Mama Mchungaji.
2. Wenye vyeo vyovyote vya Uongozi Kanisani ngazi zote Mfano wazee wa Kanisa, mashemasi na Viongozi wa Idara .
3. Wahudumu Kanisani kama Wahubiri na waimbaji.
4. Washirika wa Muda mrefu Kanisani ambao ambao sio wachanga kiroho na wameshafundishwa sana Neno la MUNGU.
✔️Lengo la kutengwa ni ili walio chini yao wasione kuizoelea dhambi ni kitu Cha kawaida.
Hata Miriamu Mwimbaji maarufu zaidi katika Taifa la Israel ilibidi atengwe siku Saba Kwa kosa lake ambalo lingeibua waasi wengi.
Hesabu 12:14 "BWANA akamwambia Musa, Je! Kama baba yake angalimtemea mate usoni tu, hangaliona aibu muda wa siku saba? Na afungwe nje ya kambi muda wa siku saba, kisha baada ya hayo ataletwa ndani tena."
◼️Muumini mchanga hatakiwi kutengwa kwa mtazamo wangu.
➡️Changamoto kwa baadhi ya Makanisa wanaotengwa zaidi ni wale ambao sio Viongozi wanapokosea makosa yanayostahili kutengwa.
Viongozi wao baadhi hukosea na hawayengwi.
◼️Kwanini Mtu atenge na Kanisa?
1. Kutengwa ni njia ya awali itakayomuoondoa mhusika kwenye nafasi zake za Uongozi ili asiambukize Kundi analiliongoza maana dhambi inazaa na Ina uwezo wa kjambukiza.
Yakobo 1:15 "Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti."
2. Kutengwa ni sehemu ya onyo ili kumpa nafasi mhusika kujutia na kutengeneza na MUNGU.
Mfano ni watu wa Ninawi walijitengs kwa ajili ya Maombi MUNGU akawasamehe.
Yona 3:10 "MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende."
3. Kutenga ni kuonyesha uwajibikaji wetu kwa MUNGU na Kwa jamii inayokuzunguka ili jamii nayo Ione namna ambavyo Kanisa linachukia dhambi.
Mfano hai ni Musa aliwanywesha majivu ya miungu wali walioabudu miungu.
Kutoka 32:20 "Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli."
4. Kuna watu ambao ni Watumishi kwa kutenda dhambi muda mrefu hufikia hatua ya hutengwa na MUNGU, hivyo Kanisa halitakiwi kuwakumbatia waliotengwa na MUNGU na hawana Moyo wa Toba.
Tito 3:10-11 " Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe."
◼️Mwisho Mtu anayechukia kutengwa aichukie kwanza dhambi inayoweza kumfanya kutengwa.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments