![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Ukweli ni kwamba Uzima wa Milele Mwanadamu yeyote hawezi kuupata akiwa nje na KRISTO YESU.
Yohana 10:10-11" .......... mimi(YESU) nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo."
◾Sababu kwanini Uzima wa Milele Mtu yeyote na wa dini yeyote hawezi kuupata nje na KRISTO YESU ni hizi;
1. MUNGU Mwenyewe aliweka njia Moja tu ya kuwafanya Wanadamu waupate Uzima wa Milele, njia hiyo ni YESU KRISTO Kwa kumpokea kama Mwokozi na kuishi katika yeye.
Yuda 1:3 "Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie IMANI WALIYOKABIDHIWA WATAKATIFU MARA MOJA TU."
◼️Ndio maana Siku Bwana YESU KRISTO anaukamilisha Wokovu wetu wale Watakatifu walioishi kabla ya wakati huo walifufuliwa na kupelekwa Paradiso ili baada ya hapo asiwepo Mwanadamu yeyote atakayepita njia nyingine yeyote kwa ajili ya Uzima Wa Milele
Mathayo 27:52-53 " makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi."
◼️Yaani njia nyingine zote za kumfanya Mwanadamu kwenda Uzima Wa Milele zilifungwa ili Sasa njia Moja na ya milele ambayo ni YESU KRISTO ianze, hivyo baada ya Bwana YESU KRISTO kuukamilisha Wokovu hakuna njia nyingine Tena ya uzima wa milele nje na yeye.
Waefeso 1:5-7 " Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya YESU KRISTO, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa(YESU). Katika yeye huyo(YESU), kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake."
2. YESU KRISTO ndio anaandaa makazi ya Watakatifu Mbinguni, hivyo hawezi kumuandalia makazi Mtu aliyemkataa kama Mwokozi.
Yohana 14:3 "Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo."
◼️Bwana YESU KRISTO anaandaa makazi Mbinguni kwa ajili ya walio wake sio walio nje, walio nje makazi yao ni Jehanamu.
Ufunuo 22:15 "Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya."
◼️Ukitaka uwe na makazi Yako Mbinguni ili siku ukiondoka Duniani uende huko basi Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi Wako Leo na Anza kuishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wake.
Tuliookoka tuna uhakika na makazi yetu Mbinguni, Ndugu na Wewe Mpokee YESU KRISTO Leo ili makazi Yako Mbinguni yaanze kuandaliwa.
Wafilipi 3:20-21 " Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana YESU KRISTO; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake."
3. Kitabu Cha Uzima Cha Mbinguni ni Cha Bwana YESU KRISTO hivyo ambao majina yao yamo humo ni Watakatifu waliookoka wakiwa Duniani.
Ufunuo 21:27 "Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo."
◼️Kitabu Cha Uzima ni Kitabu ambacho majina ya Watakatifu wote waliowahi kuishi Duniani huandikwa, hivyo Wanadamu wote na wa dini zote kama watataka majina yao yaandikwe kwenye Kitabu Cha Uzima ni lazima wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi.
◼️Nje na YESU KRISTO hakuna Uzima wa milele.
Ndugu Hakikisha Jina lako limeandikwa katika Kitabu Cha Uzima Mbinguni.
Wafilipi 4:3 "Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima."
4. Ni Jina la YESU KRISTO pekee kwa ajili ya Uzima wa Milele, hakuna Jina lingine Wanadamu wamepewa na MUNGU Kwa ajili ya Uzima wa Milele ila Jina Moja tu la YESU KRISTO.
Matendo 4:12 "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."
◼️Na aliyetoa Jina la YESU KRISTO Kwa ajili ya Wokovu wa Wanadamu wote Duniani ni MUNGU Mwenyewe, ukijitenga na YESU KRISTO ujue umejitenga na MUNGU Mwenyezi.
Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa MWANAWE PEKEE, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma MWANA ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."
◼️◼️Ndugu, ikitokea ukajifunza ujumbe huu wa Leo baada ya kujifunza Hakikisha umempokea Bwana YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.
Warumi 5:1-2 " Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa MUNGU, kwa njia ya Bwana wetu YESU KRISTO, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa MUNGU."
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe na unaweza kushare ujumbe huu kwa watu wanaokuhusu ili wajifunze.

Comments