![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."
Leo tunajifunza kuhusu ROHO MTAKATIFU kupitia maswali haya matano (5);
1. ROHO MTAKATIFU ni nani?
2. Faida za kupokea ROHO MTAKATIFU ni zipi?
3. Alama ya ROHO MTAKATIFU ndani ya Mtu ni ipi?
4. Matendo ya ROHO MTAKATIFU ni yapi?
5. ROHO MTAKATIFU anaingiaje ndani ya Mtu?
Yohana 4:24 "MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli."
➡️Kwa ujumla ROHO MTAKATIFU ni Roho wa MUNGU ambaye ana madaraka kamili na uamuzi kamili kwenye Maisha ya Wateule wa KRISTO waliompokea.
Warumi 8:9 "Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake."
◼️Kwa ujumla kama Kuna Mkristo hamhitaji ROHO MTAKATIFU katika Maisha yake huyo bado hajawa Mkristo.
◼️Hivyo Kila Mkristo aliyeokoka inampasa kumpokea ROHO MTAKATIFU ambaye pia sehemu nyingine ya maandiko anaitwa ROHO wa MUNGU au ROHO wa KRISTO.
◼️Ni Muhimu sana kuwa na ushirika na ROHO MTAKATIFU
◼️Kanisa la kweli la MUNGU Duniani huagizwa Kuenenda katika ROHO MTAKATIFU na sio vinginevyo.
Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."
◼️ Ahadi ya MUNGU tangu zamani ni kwamba Bwana YESU Alipokuja kuokoa Wanadamu aliondoka kwenda Mbinguni, ila alipoondoka alisema atakuja ROHO MTAKATIFU ambaye atakuwa na sisi Kanisa Milele.
Yohana 14:15-17 " Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba BABA, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu."
➡️Faida za ROHO MTAKATIFU kwenye Maisha Yako ukimpokea.
Ziko faida nyingi 10 katika ya nyingi ni hizi;
1. ROHO MTAKATIFU atakuongoza katika maamuzi sahihi dhidi ya watu wabaya ambao wanachukia Injili ya KRISTO YESU.
Mathayo 10:18-20 " nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.
Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni ROHO wa BABA yenu asemaye ndani yenu.
◼️ROHO MTAKATIFU katika wakati ule ule anaweza kukufundisha yakupasayo kuzungumza.
Luka 12:12 "kwa kuwa ROHO Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema."
2. ROHO MTAKATIFU hutoa karama na vipawa kwa Watumishi wa MUNGU ili Wamtumikie Bwana YESU.
1 Wakorintho 12:8-11 " Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye."
3. Mwanadamu atakuwa na uwezo wa kusema kwa uwezo wa ROHO MTAKATIFU
Marko 12:36 "Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa ROHO MTAKATIFU, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako."
◼️Daudi kwa uwezo wa ROHO MTAKATIFU alisema mambo kuhusu YESU yatakayotokea Baadae na yakatokea, Daudi alijuaje habari za YESU wakati aliishi zaidi ya miaka 700 kabla Bwana YESU KRISTO hajatokea?
Jibu ni kwamba ROHO MTAKATIFU alimpa Daudi kusema mambo ya kweli ya baadae kwa sababu ROHO MTAKATIFU anaijua baadae yote kuhusu Mbinguni na Duniani, ni Muhimu sana kumhitaji ROHO MTAKATIFU kwa kila Mtu anaitwa Mkristo.
◼️ Mfano Mwingine ni huu kuhusu Zakaria.
Luka 1:67-69 " Na Zakaria, baba yake, akajazwa ROHO MTAKATIFU, akatabiri, akisema, Atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake."
4. ROHO MTAKATIFU ndiye atatuongoza kufika Uzima Wa Milele, hivyo ni lazima kuwa naye kama unahitaji uzima wa milele
Yohana 3:5-6 " YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa ROHO ni roho."
5. Watumishi wa kweli wa MUNGU wa Mbinguni ni wale wenye ROHO MTAKATIFU na wanamfuata.
Yohana 3:34 "Kwa kuwa YEYE ALIYETUMWA na MUNGU HUYANENA MANENO ya MUNGU; kwa sababu hamtoi ROHO kwa kipimo."
◼️ROHO MTAKATIFU humshuhudia Bwana YESU hivyo tukitaka tuwe kweli Watumishi wa YESU basi tuwe na ROHO MTAKATIFU.
Yohana 15:26 "Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa BABA, huyo ROHO wa kweli atokaye kwa BABA, yeye ATANISHUHUDIA.''
Ni Muhimu sana sana kuwa na ROHO MTAKATIFU
6. ROHO MTAKATIFU hutoa Nguvu za MUNGU hivyo tukitaka tuwe na nguvu za MUNGU tumhitaji ROHO MTAKATIFU
Matendo 1:8 "LAKINI MTAPOKEA NGUVU, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi."
◼️Hata kuhubiri kwa ujasiri unamhitaji ROHO MTAKATIFU ili ufanye hivyo katika kusudi la MUNGU.
Matendo 4:31 "Hata walipokwisha kumwomba MUNGU, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa ROHO MTAKATIFU, wakanena Neno la MUNGU kwa ujasiri."
7. ROHO MTAKATIFU hututakasa.
Warumi 15:16 "ili niwe mhudumu wa KRISTO YESU kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya MUNGU kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na ROHO MTAKATIFU."
8. ROHO MTAKATIFU hutufunulia mafumbo ya rohoni
1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."
9. ROHO MTAKATIFU huwafundisha Watumishi wa MUNGU mambo sahihi ya kuhubiri
1 Wakorintho 2:13 "Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na ROHO, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni."
10. ROHO MTAKATIFU kukupa uhakika juu ya watu unaotaka Kushirikiana nao
◼️Mfano hai ni huu
Matendo 11:12 "ROHO akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;"
◼️Hata Kuwa na uwezo wa kuwa na Ufunuo juu ya watu wabaya yaani mawakala wa shetani ROHO MTAKATIFU hutoa ufunuo huo ili kukulinda Mteule wa KRISTO YESU Mwokozi.
◼️Mfano hai ni huu ambapo Paulo katika ROHO MTAKATIFU alimjua mchawi anayelaghai ili waondoke kwa YESU KRISTO.
Matendo 13:8-10 "Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa ROHO MTAKATIFU, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za BWANA zilizonyoka?
➡️ Alama ya Mtu kuwa na ROHO MTAKATIFU.
Ziko alama nyingi, baadhi tu ni hizi.
1. Mtu kuwa na hekima au akili aliyokupa ROHO MTAKATIFU ambayo wapinga Injili hawawezi kuishinda.
Matendo 6:10 "lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo ROHO aliyesema naye."
2. Alama nyingine ya Mtu kuwa na ROHO MTAKATIFU ni kunena kwa lugha katika ROHO MTAKATIFU, hivyo kama hujafikia hatua hii Jifunze kuhusu ROHO MTAKATIFU na omba sana utafanikiwa kufikia hatua ya kunena kwa lugha katika ROHO MTAKATIFU.
Mfano hai ni huu
Matendo 2:4 "Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka."
3. Alama nyingine ni Mtu kuwa na Maono ya MUNGU.
Mfano hai ni huyu Stefano aliyeona Maono ya Mbinguni kwa sababu ya kujaa Nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Matendo 7:55 "Lakini yeye akijaa ROHO MTAKATIFU, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa MUNGU, na YESU akisimama upande wa mkono wa kuume wa MUNGU."
4. Alama nyingine ni pale anapokukataza rohoni baadhi ya mambo au vitu ambavyo havikufai au ni mabaya, hiyo ni ishara ya ROHO MTAKATIFU ya wazi.
◼️Mfano hai ni huu ambapo ROHO MTAKATIFU aliwaruhusu akina Paulo kuhubiri Maeneo mengi sana lakini eneo Fulani kwa muda huo Kwa sababu ambazo ROHO MTAKATIFU mwenyewe anazifahamu aliwakataza kwa muda ule, labda wangedhurika au kulikuwa kumeandaliwa mabaya kwa ajili yao, Kumsikiliza ROHO MTAKATIFU Kuna faida kuu.
Matendo 16:6 "Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na ROHO MTAKATIFU, wasilihubiri lile neno katika Asia."
◼️Mfano hai Mwingine ni huu ambapo Watu wa MUNGU katika ROHO MTAKATIFU walimwambia Paulo asiende Yerusalemu kwa wakati ule.
Matendo 21:4 "Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa ROHO asipande kwenda Yerusalemu."
5. Ishara nyingine ni pale unapopata Neema ya ROHO MTAKATIFU kuzungumza na Wewe ndani Yako.
Matendo 10:19-20 "Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. ROHO akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma."
6. Ishara nyingine ni pale unapoomba katika ROHO MTAKATIFU
Warumi 8:26 "Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa."
◼️Yaani umejaa Nguvu za ROHO MTAKATIFU unajikuta unaomba muda mrefu sana wakati hizo Nguvu zikiondoka huwezi kuomba muda huo hata ukijilazimisha huwezi.
7. Ishara nyingine ni pale unapogundua tabia Yako au ya Mtu Mwingine imebadilishwa na ROHO MTAKATIFU na kuwa na matunda ya ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:22-23 " Lakini tunda la ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria."
➡️ ROHO MTAKATIFU huingiaje ndani ya Mtu?
1. Mtu aliyeokoka anayeishi Maisha Matakatifu na ni Mtu wa Maombi anaweza kumpokea ROHO MTAKATIFU kwa kuwekewa Mikono na Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO, yaani wakati wakimuombea ROHO MTAKATIFU anaweza kuingia ndani yake
Mfano hai ni huu
Matendo 8:17 "Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea ROHO MTAKATIFU."
2. Mteule wa KRISTO ambaye ameuweka Moyo wake tayari kumpokea ROHO MTAKATIFU anaweza kumpokea wakati Neno la MUNGU likihubiriwa.
◼️Mfano hai ni huu wakati Petro anahubiri waliokuwa wanamsikiliza ROHO MTAKATIFU aliingia ndani yao.
Matendo 10:44 "Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno."
◼️Mfano hai Mwingine ni huu ambapo Mtumishi wa MUNGU alipoanza tu kuhubiri watu wakapokea ROHO MTAKATIFU.
Matendo 11:15 " Ikawa nilipoanza kunena, ROHO MTAKATIFU akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo."
Ndugu, mhitaji sana sana ROHO MTAKATIFU kama unataka uwe mshindi Duniani, safari ya Wokovu kwako isiwe ngumu na ili uufikie uzima wa milele.
Kumbuka Mwanadamu kwamba hata kama una marafiki wengi, una Ndoa au Watoto au una watu wako wa Karibu sana wengi, siku ukiondoka Duniani wote watakuacha na siku Chache sana baadae watakusahau lakini kama ukiokoka kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako ROHO MTAKATIFU atakuwa na Wewe milele, yaani hata wakati unaondoka kwenda uzima wa milele utakuwa naye, huyo ndio Pekee ambaye hatakuacha hata ukiondoka Duniani kama unaye na unamtii.
Yohana 14:16-17 " Nami nitamwomba BABA, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili AKAE NANYI HATA MILELE; ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu."
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments