![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Ukisoma Matendo 12:3-17 unaona Nguvu ya Maombi inavyofanya kazi.
◼️Unaona Petro akiwekwa gerezani na Mfalme wakati wa Pasaka na Lengo la Mfalme lilikuwa baada ya Pasaka amtoe na kumsulubisha mbele za watu.
◼️Tunaona Kanisa likiomba kwa juhudi kwa ajili ya Petro.
Matendo 12:5 "Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba MUNGU kwa juhudi kwa ajili yake."
◼️Tunaona Maombi yakasababisha Malaika aje kumtoa Petro gerezani (Matendo 12:7)
◼️Wakati Petro ameshatolewa gerezani Kanisa liliendelea kuomba bila kujua kwamba Petro wanayemuombea ameshatoka gerezani tayari(Matendo 12:12)
◼️Ingawa Kanisa walikuwa waombaji wazuri waliomba Petro atoke gerezani lakini hata walipomuona Petro hawakuamini kama ndiye Petro na kama kweli ametokea gerezani(Matendo 12::14-15)
◼️Hawa waliomba ila mashaka yalikuwa mengi kwao.
Hata Leo Kanisa na watu wa MUNGU katika KRISTO YESU Kila mahali wanafanya Maombi Kila mara ila ni vizuri pia Kila Muombaji kutambua mitindo au style za MUNGU kujibu Maombi.
➡️Nimetafuta neno la kiswahili lenye maana ya "Style" ili nieleweke zaidi nimepata neno "Mitindo" hivyo kama hujaelewa "Mitindo ya MUNGU kujibu Maombi" basi maana yake ni "Style/Staili ya MUNGU kujibu Maombi"
Zaburi 118:5 "Katika shida yangu nalimwita BWANA; BWANA akanijibu akaniweka panapo nafasi."
✔️Maana ya mtindo ni namna ya kufanya jambo, hivyo Mitindo ya MUNGU kujibu Maombi maana yake atafanyaje wakati wa kujibu.
◼️MUNGU husikia Maombi ya Wateule wake katika KRISTO YESU.
Zaburi 66:20 "Na ahimidiwe MUNGU asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake."
➡️Mfano hai ni hapa ambapo MUNGU alisikia Maombi ya Yona akiwa ndani ya tumbo la Nyangumi chini ya maji baharini.
Yona 2:7 "Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nalimkumbuka BWANA; Maombi yangu yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu."
◾Mitindo ya MUNGU kujibu Maombi ya Wateule wake katika KRISTO YESU.
1. Kujibu Maombi muda ule ule unaomba.
➡️Mfano hai ni Maombi ya Paulo ya kutoa mapepo ndani ya kijakazi mmoja yalijibiwa wakati ule ule na mapepo yakatoka muda ule ule.
Matendo 16:18 "Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la YESU KRISTO, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile."
◼️Maombi ya kuondoa Nguvu za giza ndani ya watu mengi hujibiwa wakati ule ule.
Marko 1:27 "Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!"
➡️Kuna Maombi hujibiwa wakati ule ule unaomba, Mfano hai Mwingine ni Maombi ya Eliya ya kushusha moto yalijibiwa muda huo huo anaomba.
1 Wafalme 18:36-38 " Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe MUNGU katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe MUNGU, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji."
2. Kujibiwa kabla hujaomba.
Isaya 65:24 "Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia."
◼️Hapa ni ile Nia tu ya kuhitaji Kitu fulani ukasema moyoni " ngoja nije niombe kwa MUNGU au nifunge kwa ajili ya kitu fulani" yaani wakati unawaza tu kutafuta muda wa kuomba MUNGU anajibu.
Mathayo 6:8 "Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba."
◼️MUNGU anaweza akajibu hata mawazo Yako tu kabla hata hujaomba.
◼️Kabla hujaomba MUNGU anaweza akakujibu maana yeye anajua yote.
◼️MUNGU anaweza akatenda mambo makubwa kuliko hata ambayo utaomba.
Waefeso 3:20 "Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;"
3. Kujibiwa baada tu ya kumaliza kuomba.
➡️Mfano hai ni huu
2 Wafalme 6:17 "Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote."
➡️Elisha aliomba Maombi ya kufumbua macho ya Gehazi na alipomaliza tu kuomba MUNGU akajibu pale pale, alipomaliza tu kutamka majibu ya MUNGU yakatokea.
➡️Mfano Mwingine MUNGU alimsikia Hezekia akajibu kwa kuwaponya watu.
2 Nyakati 30:20 "BWANA akamsikia Hezekia, akawaponya watu."
➡️Mfano Mwingine ni Hezekia na Isaya waliomba na MUNGU siku hiyo hiyo akamtuma Malaika kuwaangamiza adui zao.
2 Nyakati 32:20-21 " Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.
Naye BWANA akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga."
◼️Ndugu omba kwa MUNGU katika Jina la YESU KRISTO ukiamini maana Maombi mengine MUNGU hujibu mara tu Wewe ukimaliza kuomba.
4. Kujibiwa Maombi wakati wa tendo la Imani la maelekezo ya ROHO MTAKATIFU rohoni.
◾Ngoja nikupe mifano hai 4 ili unielewe vizuri.
➡️Petro alimuombea kilema lakini alipofanya tendo la Imani la kumnyanyua ndipo kilema kikaondoka.
Matendo 3:6-7 "Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu."
➡️Hamani ili apone ukoma mahitajio ya ulimwengu wa roho ilikuwa aende mtoni kujichovya mara Saba.
2 Wafalme 5:14 "Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa MUNGU; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi."
◾Unaweza ukajiuliza kwanini hadi aende mtoni ndipo apone, kwanini asiwekewe tu mkono na Watumishi wa MUNGU akapona? Hata Mimi Peter Mabula sijui ila ni vizuri sana tukamwelewa MUNGU.
◾Ndugu mwelewe MUNGU na Mitindo yake ya kujibu Maombi, Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ni wa Muhimu sana katika Maombi.
➡️Wakoma hawakupona wakati ule ule ila walipoenda kujionyesha kwa kuhani kama walivyoambiwa ndipo walipona.
Luka 17:12-14 " Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee YESU, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika."
➡️Hata Waisraeli wakati wa Yehoshafati ilibidi wakafanye tendo la Imani la Ufunuo ili kushinda vita( 2 Nyakati 20:13-17"
◾Hata wewe unaweza Mfano ukaombewa na baada ya Maombi ukasikia msukumo wa kushuhudia Injili mitaani kumbe tendo hilo la Imani limebeba Muujiza wako.
◾Mfano unaweza ukaombewa na ndani Yako ukasikia msukumo wa Sadaka fulani ya kipekee kumbe hilo ni tendo la Imani linaloleta majibu Yako ukizingatia.
◼️Mfano hai ni Raheli ambaye alijibiwa muda mrefu baada ya kuanza kuomba.
Mwanzo 30:22-23 " MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu."
➡️Ukiangalia muda wa Maombi kwa Raheli tangu ameanza ulikuwa umepita muda mrefu maana waliolewa wakati mmoja yeye na Leah lakini Leah alizaa Watoto wengi kabla ya Raheli hajazaa Mtoto wake wa kwanza, muda wote huo Raheli alikuwa anaomba kupata Mtoto.
◼️Sasa yapo Maombi hujibiwa baadae sana baada ya kuwa umeomba na sababu kuu ya MUNGU ni kusudi lake litimie kwa wakati, Mfano hai Yusufu Mtoto wa Raheli angezaliwa kabla ya Reuben Mtoto wa kwanza wa Leah Inawezekana Yusufu huyu asingeweza kuishi kwa potifa, asingeweza kuwa Kiongozi Mkuu misri n.k hivyo MUNGU alijibu Maombi ya Raheli baadae sana kwa ajili ya kile Yusufu alichokuwa amekibeba.
➡️Lakini wapo ambao akiomba tu anajibiwa majira hayo hayo kama ilivyotokea kwa Leah ambaye hata alipoomba apewe Mtoto wa tano alijibiwa haraka tu huku mwenzako aliyeomba miaka mingi alikuwa hajajibiwa hata Mtoto mmoja.
Mwanzo 30:17 "MUNGU akamsikia Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano."
◼️Ndugu, mwelewe MUNGU ikitokea hajajibu mahitaji Yako Fulani kwa wakati uliokuwa unautaka Wewe, ila usiache kuomba maana siku akijibu utapata kitu kilicho Bora wakati Mwingine kuliko hata vitu kumi ambaye ungevipokea mapema.
6. Kujibiwa Maombi wakati wa kukumbukwa Agano au nadhiri au Sadaka ya wakati wa Maombi.
◼️Kwenye Maombi ikitokea ROHO MTAKATIFU akakupa Ufunuo wa Agano au nadhiri au Sadaka Fanya kama alivyokuambia maana Kuna majibu mengine ya MUNGU huja wakati wa kukumbukwa sadaka au nadhiri au Agano ulilofanya na MUNGU kabla.
➡️Mfano hai MUNGU alijibu kwa wazawa wa Ibrahimu baada ya kukumbuka Agano la Ibrahimu.
Kutoka 2:24" MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo."
◼️MUNGU anaitwa MUNGU wa Agano hivyo ukiweka Agano na yeye hatasahau ujue na Iko siku atakumbuka Agano hilo na kukutendea mahitaji Yako.
Walawi 26:42 "ndipo nitakapokumbuka agano langu pamoja na Yakobo, tena agano langu na Isaka, tena agano langu na Ibrahimu nitalikumbuka; nami nitaikumbuka nchi hiyo."
◼️Yakobo nadhiri yake ilikumbukwa na MUNGU na akamtendea Miujiza mingi.
Mwanzo 28:20 "Yakobo akaweka nadhiri akisema, MUNGU akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;"
◼️Hannah aliweka nadhiri na MUNGU alijibu.
1 Samweli 1:11 "Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe."
➡️Kuna wakati MUNGU hukumbuka Agano, lijue hilo.
Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."
◼️ Sadaka za Kornelio zilikumbukwa na MUNGU akatendewa Muujiza.
Matendo 10:31 "akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za MUNGU."
7. Kujibiwa baada ya wakati wa jambo hilo kiroho kufika.
◼️Kiroho Kila jambo Lina wakati wake.
Kuna mambo ukisikia msukumo mkubwa kuyaombea wakati Mwingine ni kwa sababu wakati wake kupokea juu ya hayo unakuwa umefika.
➡️Ila yapo mengine hata ukiyaombea ni Sasa ila kama yanasubiri wakati wake basi yatajibiwa wakati wake kiroho ukifika.
Mhubiri 3:1 "Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."
◼️Ndugu, Hakikisha unaomba katika Jina la YESU KRISTO na majibu Yako mwachie MUNGU naye atajibu maana Kuna wakati wake uliokubalika atajibu katika wakati huo.
Isaya 49:8" BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa;"
◼️Ndugu Hakikisha unaomba kwa Imani katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi na MUNGU katika wakati wake atakuinua.
1 Petro 5:6 Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;
◼️Hakikisha unaomba kwa Neno la MUNGU la Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU unapopewa katika majira ya Maombi.
◼️Hakikisha unaomba kwa Neno la MUNGU katika KRISTO YESU.
MUNGU husikia Maombi na atakujibu.
1 Petro 3:12 "Kwa kuwa macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya."
◼️Siku zote Jina la YESU KRISTO lipo tayari kukushindia muda wowote.
◼️Ndugu, Hakikisha umeokoka na unaishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
◼️Omba katika Jina la YESU KRISTO utamuona MUNGU wa Miujiza
Naamini umejifunza jambo zuri na utafanyia kazi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments