![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU kuhusu Maombi ya asubuhi.
◼️Asubuhi huonyesha Neema ya MUNGU kwako maana amekulinda usiku wote kipindi ulipokuwa umelala.
Zaburi 3:5 "Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, Kwa kuwa BWANA ananitegemeza."
◼️Ukiona umeamka asubuhi jua tu ni Neema ya MUNGU katika KRISTO YESU maana sio wote hupata Neema hiyo ya kuamka wakiwa katika Ufahamu mzuri.
Yeremia 31:26 "Basi, nikaamka, nikaangalia; na usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu."
➡️Usiku wakati umelala Inawezekana ulikuwa katika vita ya kiroho.
➡️Usiku Ukiwa umelala Inawezekana ulikuwa unapokea maelekezo ya ROHO MTAKATIFU katika jambo fulani kwenye Maisha Yako au kwenye wito wako.
➡️Usiku Inawezekana ulikuwa unaona mambo ambayo yanaendelea kwenye ulimwengu wa roho maana Mwanadamu ni roho anayeishi katika mwili, hivyo roho inaweza kupewa Neema na MUNGU ya kwenda sehemu yeyote au kuona chochote kile MUNGU alitaka kumuonyesha mhusika ambaye ni Mtu anayeishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa KRISTO Mwokozi.
Ayubu 33:14-16 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,"
◼️Usiku una mambo mengi hivyo ni Muhimu kuanza asubuhi kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO.
◾Maombi hayo ya asubuhi yanatokana na mambo 3.
✔️Maombi hayo ya asubuhi yanatokana na Shukrani kwa MUNGU.
✔️Maombi hayo yanatokana na usiku ulipokuwa umelala.
✔️Maombi hayo yanatokana na siku mpya unayoiendea.
◾Maombi 7 ya asubuhi kwa Mteule wa KRISTO ni haya
1. Mshukuru MUNGU wa Mbinguni.
1 Nyakati 23:30 "nao wasimame kila asubuhi kumshukuru na kumsifu BWANA, na jioni vivyo hivyo;"
◼️Biblia inasema Kila asubuhi wamshukuru MUNGU.
Mimi Peter Mabula nakushauri rafiki yangu unayesoma ujumbe wangu huu kwamba na Wewe Jipe jukumu hili Kila siku la kuomba ukimshukuru MUNGU katika KRISTO YESU maana amekulinda usiku ndio maana umepata nafasi ya kuamka.
◼️Mshukuru MUNGU pia kwa siku mpya aliyokupa uiishi.
Zaburi 88:13 "Lakini mimi nimekulilia Wewe, BWANA, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia."
◼️Mshukuru MUNGU maana anaweza kuisikia Sauti Yako asubuhi.
Zaburi 5:3" BWANA, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia."
2. Kama MUNGU alisema na Wewe usiku kwa ndoto au Maono au Sauti omba akupe uwezo wa kufanya kile alichokuelekeza usiku.
Kutoka 8:20" BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi."
➡️Mfano hai ni huu katika andiko hapo juu ambapo tunaona Musa alipewa na MUNGU maelekezo usiku ili asubuhi ayafanyie kazi.
Musa alipewa maelekezo usiku ya kumfuata Farao asubuhi ili Akamwambie Farao yale MUNGU amesema naye usiku.
➡️Hii ikufundishe kwamba MUNGU anaweza akasema na Wewe usiku ili ukiamka tu ufanyie kazi maelekezo hayo.
➡️Mambo mangapi Bwana YESU KRISTO amewahi kusema na Wewe Ndotoni au kwenye Maono usiku ili ukiamka tu uyafanyie kazi?
◼️Naamini ni mengi, kuanzia Leo kupitia Ufunuo wa Neno la Leo fanyia kazi Kila anachokuambia MUNGU usiku Ukiwa umelala.
➡️Jifunze kwa Yusufu ambaye alipewa maelekezo na Malaika wa MUNGU usiku na alipoamka aliyafuata maelekezo hayo ya ki MUNGU aliyokuwa amepewa Usiku.
Mathayo 1:24 "Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa BWANA alivyomwagiza; akamchukua mkewe;"
➡️Na ukisoma Isaya 3:3-5 na mstari wa 11 unaona maelekezo yaliyotokea usiku, hata Wewe unaweza kupewa maelekezo usiku na Bwana YESU KRISTO, omba kuyaelewa na kuyafanya.
3. Kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO haribu mipango mibaya iliyopangwa na watu wabaya au mawakala wa shetani wakati ulipokuwa umelala.
➡️Mfano ni huu ambapo usiku Sauli alipanga mipango ya kumuua Daudi.
1 Samweli 19:2 "Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;"
➡️Sauli alipanga mipango mibaya dhidi ya Daudi usiku, alipanga kumuua.
Hata Wewe unaweza ukapangiwa mipango mibaya usiku na wapangaji wa mabaya hayo wanaweza kuwa Wanadamu au Nguvu za giza.
◼️Ukiamka wakati Mwingine kemea na kukataa mabaya yote yaliyopangwa dhidi Yako wakati umelala.
Kuna vitendo unatakiwa uvifanye mara tu unapoamka.
Hata Bwana YESU KRISTO alipoamka tu aliukemea upepo.
Marko 4:39 "Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu."
➡️Wewe ukiamka huwa unafanyaje ? Wakati Ukiwa umelala uliona mabaya?
◼️Ndugu katika Jina la YESU KRISTO nakusihi uwe unakemea na kuyafuta kwa Jina la YESU KRISTO Kila mabaya uliyoyaona kipindi umelala.
4. Omba Maombi ya kutambua ulichokiona wakati umelala.
Mwanzo 28:16" Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua."
➡️Watu wengi hudharau waliyoyaona wakati wamelala, Ndugu Wewe usiwe hao wanaodharau waliyoyaona.
◼️Kama Kuna kitu umekiona wakati umelala ila hujakielewa omba Maombi ya kutambua na ROHO MTAKATIFU atakupa kutambua.
Inawezekana uliona ni lini utatendewa Muujiza wako ila hukujua, Inawezekana umeonyeshwa adui Yako n.k
5. Ombea njia utakazoziendea siku hiyo.
Zaburi 143:8 "Unifanye kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unijulishe njia nitakayoiendea, Kwa maana nakuinulia nafsi yangu."
➡️Inawezekana umeamka asubuhi lakini siku hiyo Mchana au asubuhi unasafiri unaenda kazini au safari ya mbali, unaenda kwenye usaili, unaenda kuhubiri n.k
◼️Ombea njia zako utakazoziendea siku hiyo, zikabidhi kwa MUNGU Kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO.
6. Omba MUNGU akupe Nguvu za kufanikiwa siku hiyo.
Isaya 51:9" Amka, amka, jivike nguvu, Ee mkono wa BWANA; Amka kama katika siku zile za kale, Katika vizazi vile vya zamani."
◼️Ukiamka Jivike Nguvu za kufanikiwa kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO.
➡️Biblia ipo wazi kwamba usitegemee akili zako tu Bali mtumaini MUNGU hivyo usiseme tu kwamba "Leo lazima nifanikiwa katika kitu fulani" Bali omba MUNGU Kisha ndio ujitamkie kufanikiwa.
Kumbuka kutegemea watu tu au kujitegemea pasipo MUNGU ni hasara.
Yeremia 17:5'' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA."
7. Omba MUNGU akupe fadhili zake za asubuhi ili uwe na siku njema.
Zaburi 90:14 "Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote."
➡️Fadhili za MUNGU ni nini?
◼️Fadhili za MUNGU ni msaada wa MUNGU.
◼️MUNGU anaweza akakufadhili hata kama hukustahili, omba kwa MUNGU katika jina la YESU KRISTO na fadhili za MUNGU zitakufuata kuanzia asubuhi Yako.
Naamini umejifunza jambo zuri na utafanyia kazi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments