MTUMISHI WA MUNGU OMBA MUNGU AJIFUNUE KWAKO BINAFSI.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

➡️Ukisoma Hesabu 12:6 Biblia inasema " Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati yenu,Mimi, BWANA,nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto." Hiyo maana yake MUNGU anaweza akajifunua kwa Mtumishi wake yeyote hapa ametoa Mfano wa kujifunua kwa Nabii na ukiendelea  kusoma Hesabu 12:8 Biblia inasema Kwamba MUNGU Kwa Musa atajifunua tofauti na anavyojifunua kwa manabii, Biblia inasema "Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?"

◼️Kama Kuna kitu Muhimu sana kwa Mtumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU basi ni MUNGU kujifunua kwa Mtumishi huyo binafsi, maana Kila Mtumishi katika Mwili wa KRISTO ana jukumu lake.

Zaburi 98:2 "BWANA ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake."

➡️Mfano MUNGU ameufunua Wokovu wake kwa watu wote lakini Watumishi wote sio Wainjilisti Wala sio Wachungaji Wala sio Mitume na Wala wote sio Manabii, omba MUNGU ajifunue kwako binafsi ili ujijue Wewe ni nani.
Namshukuru MUNGU wa Mbinguni Mimi  Bwana YESU aliponiita alijifunua kwangu hata nikajua Mimi ni nani na majukumu yangu katika kazi yake ni yapi.

◼️Kama MUNGU asipojifunua kwako utatembea kwenye Maono ya wengine.

◼️Kama Bwana YESU KRISTO asipojifunua kwako ni rahisi kukosea au kwenda nje na wito wako kwa kuiga wengine au kwa kutumia akili zako kinyume na kusudi la MUNGU Kwa wito wako.

◾Mimi  nimewahi kuwauliza maswali Wachungaji kadhaa juu ya ndoto walizoota Kila mara kabla hawajawa Wachungaji na nilijifunza kitu juu ya "wito binafsi wa Mtu"

➡️Mchungaji mmoja alisema hivi " kabla sijafungua Kanisa nikiwa tu nimeokoka nilikuwa naota Kila mara navua samaki na kuweka kwenye Tenga, ndoto nyingine naota navua samaki mtoni, ndoto zingine navua samaki ziwani na zingine navua samaki Baharini, ndoto za hivi zilikuwa zinajirudia mara nyingi." Mimi Peter Mabula Nikagundua Bwana YESU alipomuita alijifunua kwa Mtumishi huyo ili awe Mchungaji, hata Petro alifunuliwa na Bwana YESU aliponiitwa kwamba atakuwa mvuvi wa Watu.

Luka 5:10 "na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. YESU akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu."

◼️Hapa Bwana YESU alikuwa anajifunua kwa Petro juu ya huduma aliyomwitia yaani kuvua watu au kwa Jina lingine kuwatoa watu Duniani na kuwapeleka kwa MUNGU.

➡️Mchungaji Mwingine kabla ya kuanza Uchungaji akiwa tu Kijana aliyeokoka anayemcha MUNGU alikuwa anaota mara kwa mara akivua samaki katika ardhi ya eneo Fulani mkoa fulani, baadae alipata akili ya kwenda kuanzisha Kanisa katika eneo hilo jambo la ajabu alipoenda tu eneo hilo alipata watu wengi sana katika huduma yake, huduma yake ni kubwa hadi Leo ingawa eneo hilo na mkoa husika  aliloanzisha Kanisa ni eneo ambalo asilimia 95 ya wakazi wa eneo hilo ni dini nyingine nje na Ukristo.

◼️Mtumishi wa MUNGU omba sana MUNGU ajifunue kwako binafsi ili ujue wito wako.

➡️Mtumishi Mwingine aliota Ndoto mara kadhaa akiwa ameshika Biblia akitembea na watu wengi sana wakimfuata, baadae huyu akawa Mwalimu mzuri sana wa Neno la MUNGU Kwa mamilioni ya watu.

➡️Mtumishi Mwingine aliota akiwa ameshika fimbo na maelfu ya watu wakimfuata baadae alikuwa na ujumbe wa ajabu wa Maombi ya kuwatoa watu kwenye vifungo vya shetani na watu wengi sana wakafunguliwa.

◼️Bwana YESU kujifunua kwa Mtumishi wake Ina maana kubwa sana.

◼️MUNGU anaweza akajifunua kwako kukuonyesha Nini utafanya au Nini ufanye katika wito aliokuitia kwenye kazi yake.

Tito 1:3 akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu;

◼️MUNGU anaweza akajifunua kwa kukupa maelekezo binafsi ya Wewe kwenye mwili wa KRISTO 

Mfano hai ni huu ambapo Amos alipewa huduma ya kuwaonya  watu na Wafalme hata wakawa hawataki atabili.

Amosi 7:14-17 " Ndipo Amosii akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli. Basi, sasa lisikie neno la BWANA; Wewe unasema, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka; kwa hiyo, BWANA asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake."

◼️Ndio maana Leno Lengo  la MUNGU ni kwamba watu waokoke waupate Uzima Wa Milele lakini Kila Mtumishi na Staili yake ya kuwafanya watu wampokee KRISTO YESU na kuokoka.

➡️Katika wito wengine ni waandishi wa vitabu, wengine huendesha semina, wengine mikutano ya Injili, wengine kushuhudia, wengine uumbaji n.k na Kwa njia hizo watu wengi wanakuja kwa YESU KRISTO.

Waefeso 4:1-7 " Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika BWANA, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
 BWANA mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni BABA wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake KRISTO."

➡️Wengine Bwana YESU amejifunua kwao wawe Mitume, wengine Manabii, wengine Wainjilisti, wengine Wachungaji na wengine Walimu.

◼️Kwa MUNGU Ziko idara nyingi sana, ni Muhimu sana kubaki Kila Mtumishi kwenye Idara yake aliyopewa na MUNGU wakati MUNGU anajifunua kwa Mtumishi huyo.

➡️Wengine mkazo wa Ufunuo waliopewa ni kuhubiri Imani, wengine kuhubiri Maombi, wengine kuhubiri utoaji, wengine kuhubiri ROHO MTAKATIFU n.k

◼️Lakini funuo zote hizo Lengo ni kuwafanya watu wawe ndani ya Wokovu wa KRISTO na waishi Maisha Matakatifu ya Wokovu.

◼️MUNGU huwa anatoa Ufunuo kwa watu wake.

Malaki 1:1 "Ufunuo wa neno la BWANA kwa Israeli kwa mkono wa Malaki"

◼️Ufunuo huwa umebeba majira, Nini Cha kufanya, ushauri, majibu ya maswali magumu ya wakati huo n.k

➡️Inawezekana bado hujapata Ufunuo binafsi wa MUNGU kwako katika KRISTO YESU, endelea kuomba, kumcha MUNGU na Kwa sababu yeye anataka umtumikie basi  muda sio mrefu atajifunua kwako.
Wako watu MUNGU bado hajajifunua kwao lakini wakikaa vizuri na YESU MUNGU atajifunua kwao na watafanya kazi kubwa mno, Mfano hai ni Samweli.

1 Samweli 3:7 "Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake."

➡️Ukisoma maandiko katika hii Samweli wa 1 sura ya 3 unaona Samweli anaitwa na MUNGU yeye anaenda kwa Elly, ni kwa sababu yeye wakati huo alikuwa hana Ufunuo binafsi wa MUNGU.

◼️Samweli baada ya kupata Ufunuo wa MUNGU alikuwa Mtu Mwingine kabisa, Taifa Zima likimtegemea.

◾Faida za MUNGU kujifunua kwako Mtumishi.

1. Utaelewa Nini ufanye na wakati gani.

➡️Mfano hai ni Sulemani alilopata Ufunuo wa MUNGU juu yake alijijua yeye ni nani na  nini Cha kufanya.

1 Wafalme 3:12 basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.

◼️Omba MUNGU ajifunue kwako binafsi ili ujitambue Wewe ni nani na unatakiwa ufanye nini katika kazi ya MUNGU.

2. YESU aliyekupa wito na Ufunuo atakufundisha.

➡️Mfano hai ni Paulo ambaye alipewa Ufunuo na Bwana YESU hivyo kazi aliyoifanya ya Injili alifundishwa na Bwana YESU KRISTO Kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 1:12 "Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo."

◼️Omba ROHO MTAKATIFU akufundishe na Baki katika Mafundisho yake daima ili ufanye kazi nzuri ya MUNGU katika KRISTO YESU.

3. Utaelewa mipaka yako  yote ili kulinda Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU kwako.

➡️Mfano hai ni Yohana Mbatizaji ambaye alikuwa Mtumishi mashuhuri sana lakini aliujua mpaka wake kuhusu YESU KRISTO hivyo alimpa heshima yake.

Mathayo 3:14 "Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?"

◼️Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU utakufanya uijue mipaka yako, kama huna Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU unaweza kukosea na hata kujikuta ukishindana na Watumishi wengine waaminifu wa Bwana YESU KRISTO.

◼️Mtumishi mwenye Ufunuo wa MUNGU huwa na mipaka, na hata katika baadhi ya mambo MUNGU aliyokukataza utazingatia kwa sababu una Ufunuo wake, Kuna watu hata walikatazwa binafsi kula baadhi ya vyakula ingawa wengine wanakula, hivyo utajua Nini ule na Nini usile, Nini ufanye na nini usifanye.

◼️Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU utakuwekea mipaka na Staili ya Maisha unayotakiwa kuishi.

◼️Utajua Nini uongee na Nini usiongee.

4. Utakuwa na furaha ya huduma ukitembea kwenye Ufunuo wa MUNGU ukioitiwa.

◼️Ufunuo wa MUNGU utakupa kujielewa, kujiamini na kufanya mambo kwa uhakika huku Ukiwa na furaha ya ndani na uhakika.
Furaha ya ndani ya moyo kwenye utumishi ni furaha ya ROHO MTAKATIFU.

Ayubu 33:16 "Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,"

5. Hutakuwa na mashaka Wala hofu Wala wasiwasi pindi upinzani wa huduma  au dhoruba vikitokea vinavyoenda kinyume na Ufunuo wa Bwana YESU kwako.

➡️Kumbuka MUNGU hutoa ufunuo.

Isaya 53:1 "Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?"

◼️Hivyo kama MUNGU hutoa ufunuo binafsi kwa Mtumishi wake katika KRISTO YESU hiyo itapelekea Mtumishi huyo asiwe na wasiwasi kipindi ukitokea upinzani labda wa watenda dhambi, Viongozi wadhalimu wa kidunia au wapinga kweli ya MUNGU n.k

➡️Mfano umeambiwa kuwaonya jamii fulani ili waache matambiko wamfuate YESU KRISTO, Kuna waganga wanafaidika na matambiko hayo kwa kuibia watu hivyo watakuchukia tu na wanaweza hata kuwatumia Viongozi wa kidunia walio wadhalimu ili kukuletea upinzani na machafuko au hata kukufunga gerezani ila hutaogopa maana unamjua MUNGU aliye hai.

6. Utaendelea kupewa maelekezo na ROHO MTAKATIFU maana uko ndani ya  Ufunuo au wito ulioitiwa.

➡️Mfano hai ni Danieli ambaye alikuwa anaishi katika kusudi la MUNGU aliendelea kufunuliwa mambo mbalimbali zaidi yanayoendana na wito wake.

Danieli 2:19 "Ndipo Danielii alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danielii akamhimidi Mungu wa mbinguni."

◼️Hata wewe kwa sababu MUNGU amejifunua kwako binafsi atakupa na ziada nyingi sana na Ufahamu mkubwa katika Yale aliyokufunulia au yanayoendana na huduma Yako.

Danieli 1:17 "Basi, kwa habari za hao vijana wanne, MUNGU aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danielii naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto."

◼️Ndugu Hakikisha una Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ili ufanye kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU Kwa usahihi na uhakika.
Hata Wewe omba MUNGU ajifunue kwako ili ujue wito wako.

1 Samweli 3:21 "Naye Bwa6na akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa BWANA akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la BWANA. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote."

7. MUNGU atafanya kazi na Wewe Kwa ukubwa akiwafunulia hata unaowaendea kwa Injili.

◼️Kwa sababu unaishi katika kusudi la MUNGU na unajua wito wako usishangae watu wengine kufunuliwa kuhusu Wewe, wanakujua, wanashirikiana na Wewe, wanakuombea kwa sababu rohoni wanakujua na wanaijua thamani Yako.

Ayubu 36:10 "Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo, Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu."

8. Utazaa matunda Sahihi kwa sababu YESU KRISTO alipojifunua kwako ulizingatia na unatembea kwenye kusudi la MUNGU.

Yohana 15:16 "Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni."

◼️Ndugu omba kwa MUNGU ili ajifunue kwako binafsi.

➡️Kuna watu Leo wanaishi katika Maono ya Baba zao wa kiroho na sio katika Ufunuo wa MUNGU au wito wao walioitiwa na MUNGU, hiyo sio sahihi.

➡️Kuna hawana Ufunuo wa MUNGU ndio maana wanafanya kazi ya Injili kwa akili zao tu, hapo kwenda kinyume na MUNGU ni rahisi mno.

◼️Ufunuo wa MUNGU umebebwa na ROHO MTAKATIFU hivyo mhitaji sana ROHO MTAKATIFU na omba akupe Ufunuo wako binafsi katika kazi ya MUNGU.

Luka 12:12 "kwa kuwa ROHO MTAKATIFU atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema."

◼️Huwa Kuna hasara ukifanya kazi ya MUNGU bila Ufunuo wake.

◾Hasara za kufanya kazi ya MUNGU bila Ufunuo wake.

1. Ni rahisi kuiga hata kile ambacho MUNGU hajakuitia, utaiga huduma isiyo Yako, utajipachika majina tofauti na kusudi la MUNGU, hutazaa matunda safi ya utumishi wako.

◼️Wanaoiga wapo ila jitahidi usiwe Wewe.

Mfano ni huu

Matendo  19:13-16 " Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana YESU juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa YESU, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, YESU namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa."

2. Kwa sababu huna Ufunuo binafsi wa MUNGU utajikuta tu unatembea kwenye Ufunuo wa watu wengine hata kama ni Ufunuo wa uongo.

➡️Mfano Leo Kuna watu wanaiga kutumia vitu wanavyodai ni vya upako na ni uongo, watu wamejikuta badala ya kuwa busy na YESU KRISTO wao wako busy na mafuta ya upako, maji ya upako n.k
Asiye na Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ndio huiga maana hajui wito wake.

◼️Ndugu Mtumishi Usikubali kuishi maisha ya maagizo, omba MUNGU ajifunue kwako binafsi 

3. Ukiwa huna Ufunuo wa MUNGU hutafikia malengo katika huduma.

➡️Watumishi wengi wa aina hii hukimbia Makanisa ingawa walianza kwa mbwembwe ila hawakuwa na Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.

4. Ukiwa huna Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU unaweza kujikuta una msimamo mbaya unaolipinga kusudi la MUNGU uliloitiwa.

➡️Mfano Leo Kuna watu ni Wakristo hata hudai mungu anayeabudiwa na wapinga KRISTO eti ni huyo huyo MUNGU wa Mbinguni, Wakristo wa aina hii hawamjui MUNGU wa Mbinguni aliyeumba Mbingu na Dunia.
MUNGU anayeyeabudiwa katika KRISTO YESU ndio MUNGU Pekee wa kweli na wote walio nje na KRISTO YESU wanaabudu miungu, hivyo Mtumishi asiye na Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ni rahisi sana kuwahadaa watu.

Ndugu, yeyote na dini yeyote wanaomkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wao hao Moja kwa Moja wamemkataa MUNGU Aliyeumba Mbingu na Dunia na wako nje na Yeye.

Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."

5. Kama huna Ufunuo wa MUNGU ni rahisi kutembea nje na kusudi la MUNGU kuhusu Wewe.

➡️Utaiga mambo ya kidunia n.k

6. Kama huna Ufunuo wa MUNGU utaongozwa na Tamaa zinazotokana na kuiga hata kama hujui huyo unayemuiga kweli ana Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU au hana 

◼️Kama huna Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ni vigumu kuwa Mtumishi sahihi Bwana YESU KRISTO.

2 Timotheo 3:5-7 " wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao. Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi; wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli."
 Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.


Comments