![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Wana heri wafao katika KRISTO YESU yaani Wana heri watu ambao wameokolewa na Bwana YESU KRISTO Kisha muda wao wa kuondoka Duniani ukafika na wao wakaondoka wakiwa wanaishi Maisha Matakatifu katika Wokovu wa KRISTO.
➡️Tunajua kila mwanadamu anayeishi duniani kwa majira yake ataondoka duniani.
Biblia haifichi kuhusu kufa ila inasema ana heri anayekufa katika Bwana YESU KRISTO.
Ufunuo 14:13 "Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, HERI WAFU WAFAO KATIKA BWANA tanTgu SASA. Naam, asema ROHO, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao."
➡️Huyu anayekufa katika KRISTO ni Mtu gani?
◼️Mtu anayekufa katika Bwana YESU Ni mtu aliyempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake wakati wa uhai wake na hakumkana YESU wakati wa uhai wake huku akiishi Maisha Matakatifu ya Wokovu hadi mwisho wake Duniani.
Warumi 6:23 "Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; BALI KARAMA YA MUNGU NI UZIMA WA MILELE KATIKA KRISTO YESU BWANA WETU."
➡️Kwanini ni heri kwa Mtu huyo anayekufa katika YESU?
◼️Ni Kwa sababu baada ya kufa kwake hakutakuwa tena na hukumu ya kumpeleka jehanamu.
Warumi 8:1 "Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU"
◼️Jambo muhimu kujua ni kwamba hatuna makazi ya kudumu duniani bali kuna makazi ya milele baadaye kama tukimaliza Duniani tukiwa na KRISTO, Kuna Uzima wa Milele kama tukimaliza na KRISTO katika utakatifu wake.
Duniani hapa hatuna makazi ya kudumu.
Waebrania 13:14 "Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao."
◼️Kwa hiyo Mteule wa KRISTO haina haja ya kuogopa kifo wakati una KRISTO na unaishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wake.
Na biblia iko wazi sana kwamba kama Mtu aliyeokoka akifa basi ajue amekufa katika KRISTO na kama akiishi bado yeye ni mali ya KRISTO vilevile.
Warumi 14:7-9 " Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa BWANA, au kama tukifa, twafa kwa BWANA. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya BWANA. Maana KRISTO alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia."
◼️Kama umeokoka kweli na YESU KRISTO ni Mwokozi wako Biblia inasema ni heri siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.
Mhubiri 7:1 "HERI sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na SIKU YA KUFA KULIKO SIKU YA KUZALIWA."
➡️Mfano hai wa wanaokufa katika KRISTO na kujulishwa atakako kwenda ni yule mfungwa msalabani ambaye alimpokea YESU pale pale na YESU akamsamehe na kumwambia ataenda paradiso yaani pema peponi.
Luka 23:43 "YESU akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi."
◼️Paradiso ndio Makazi ya Wateule wa KRISTO waliokufa katika yeye.
➡️Kumbuka baada ya kifo hiki cha kawaida kuna kifo kingine kiitwacho jehanamu ya milele, YESU KRISTO anatuambia sisi tuliompokea kama Mwokozi kwamba hatutaenda hiyo mauti ya pili iitwayo jehanamu bali tutakuwa hai milele katika Uzima wa Milele.
Yohana 11:25-26 " YESU akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?"
◼️Ndio maana kina thamani mbele za MUNGU kifo cha mtu aliyeokoka.
Zaburi 116:15 "Ina thamani machoni pa BWANA Mauti ya wacha MUNGU wake."
◼️Ndugu uliye na YESU nakusihi sana endelea mbele na Wokovu wa YESU KRISTO, ishi Maisha Matakatifu maana Wenyeji wetu sisi tuliookoka ni Mbinguni, tukiondoka hapa duniani tunakwenda Mbinguni.
Wafilipi 3:20 "Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana YESU KRISTO;"
◼️ Ndugu, Ishi kama msafiri ambaye anajua ndege au basi muda wowote inafika ili asafiri, safari Yako ni safari ni safari ya Uzima wa Milele, hakuna haja ya kujisahau katika Maisha haya.
Yakobo 4:13-14 " Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka."
◼️ Ndugu uliye na Wokovu wa KRISTO Usiogope kuondoka maana hata Watumishi wa MUNGU mashuhuri waliondoka.
Mfano hai ni huu.
Mwanzo 35:29 "Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika"
◼️Hivyo Muhimu ni kujiandaa kwa Kuishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments