MAENEO 7 AMBAYO MUNGU ANAWEZA KUSEMA NA WEWE KUTOKEA HUKO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.


◼️MUNGU wetu wa Mbinguni huwa anazungumza na Wanadamu ukiwemo Wewe na Mimi.


Ezekieli 12:25 "Maana mimi ni BWANA; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU."


◼️Ulishawahi kujiuliza MUNGU anaweza kusema na Wewe kutokea wapi?

Watu wengi wamekariri Maeneo labda Moja au mawili tu ambayo wanajua MUNGU katika KRISTO YESU anaweza kusema nao, kama MUNGU akitumia eneo lingine tofauti na wanalolijua hawatajua kama ni MUNGU anasema nao.

Mimi Peter Mabula Niko hapa Leo kukuletea Maeneo Saba ambayo MUNGU anaweza kuzungumza na Wewe kutokea huko.


◾Maeneo 7 ambayo MUNGU anaweza kusema na Wewe kutokea huko.


1. MUNGU anaweza kusema na wewe kutoka Mbinguni Moja kwa Moja .


◼️Mfano hai ni huu.

 Mathayo 3:17 "na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye."


◼️Katika andiko hili Sauti ya MUNGU ilisikika kutokea Mbinguni na watu wakaisikia, hivyo MUNGU anaweza kuzungumza nasi kutokea Mbinguni Moja kwa Moja.


✔️✔️Wako watu wengi MUNGU alizungumza nao kutokea Mbinguni, na kwako anaweza akazungumza na Wewe Moja kwa Moja kutokea Mbinguni.


Kutoka 20:22 "BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni."


◼️Endelea tu kumcha MUNGU katika KRISTO YESU na atasema na Wewe mambo mengi sana.


2. MUNGU anaweza akasema na Wewe kupitia Mtumishi wake.


Zekaria 7:7 "Je! Hayo siyo maneno aliyoyasema BWANA kwa vinywa vya manabii wa zamani, wakati Yerusalemu ulipokaliwa na watu na kufanikiwa, na miji yake iliyokuwa ikiuzunguka; na wakati ule ambao nchi ya Negebu na Shefela ilipokuwa ikikaliwa na watu?"


➡️Hapa watu wengi sana wamepishana na kusudi la MUNGU Kwa sababu hawakuwaamini Watumishi wa Bwana YESU KRISTO waliosema nao, na kumbe ni MUNGU alitumia Vinywa vya Watumishi hao kusema nao.


◼️ Ndugu jiwekee utaratibu wa kuwasikiliza Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO wanapokupa ujumbe wa Neno la MUNGU, MUNGU anaweza kusema na Wewe kutokea kwenye Vinywa vyao.


2 Wakorintho 5:20 "Basi tu wajumbe kwa ajili ya KRISTO, kana kwamba MUNGU anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya KRISTO mpatanishwe na MUNGU."


➡️Inawezekana Mchungaji wako kwa sababu unamzidi elimu au uchumi hivyo unamdharau, Ndugu ni hasara kuu kwako kama MUNGU ataamua kusema na Wewe kupitia Mchungaji huyo na Wewe ukapuuzia kwa sababu unamwangalia Mchungaji kimwili na sio kiroho.


3. MUNGU anaweza kusema na wewe akiwa hapa hapa Duniani.       

◼️Mfano hai ni Ibrahimu ambaye alipata Neema hiyo ya MUNGU kusema nae hapa hapa Duniani kwenye mazingira ya nyumbani kwake Ibrahimu.


Mwanzo 17:22 "MUNGU akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu."


◼️Biblia inaposema kwamba MUNGU alipomaliza kusema nae akapanda kwenda Mbinguni, hiyo maana yake wakati anazungumza alikuwa hapa hapa Duniani.


◼️Hata Wewe unaweza ukapata Neema hiyo, Ishi tu Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO na MUNGU ipo siku atasema na Wewe.


◼️Hata Yakobo alipata Neema hiyo, ya MUNGU kusema nae kutokea hapa hapa Duniani.


Mwanzo 35:13" MUNGU akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye."


◼️Hata Musa alipata Neema hiyo.


Kutoka 19:20-21 " BWANA akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa BWANA kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia."


4. MUNGU anaweza kusema na wewe kutokea Kanisani, Ibadani, Madhabahuni.


◼️Mfano hai ni huu.


Mambo ya Walawi 1:1" BWANA akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia,"


◼️Kumbe MUNGU anaweza kuzungumza na Wewe kutokea Ibadani, Kanisani, madhabahu au kule unakomfanyia Ibada.


◼️Ndugu kamwe usiache kwenye Ibadani kule ambako MUNGU Baba anaabudiwa katika ROHO MTAKATIFU ndani ya KRISTO YESU Mwokozi, kama unahitaji MUNGU azungumze na Wewe.


5. MUNGU anaweza kusema na wewe  kutokea kwenye ndoto au Maono anayokupa.


Ayubu 33:14-16 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,"


◼️Hata baadhi ya Watumishi wake MUNGU husema nao kupitia Ndoto na Maono, hata Wewe kama umeokoka ni Mtumishi wa MUNGU na MUNGU anaweza kusema na Wewe kutokea kwenye  Ndoto au Maono.


Hesabu 12:6 "Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati yenu,Mimi, BWANA,nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto."


6. MUNGU anaweza kusema na wewe kutokea ndani ya Malaika.


◼️Mfano hai ni huu ambapo anapoanza kuzungumza ni Malaika ila baadae Biblia inaonyesha ni MUNGU anazungumza kutoka ndani ya Malaika.

         

Mwanzo 31:11-13 " Na malaika wa MUNGU akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani. Mimi ni MUNGU wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa."


◼️Hata kwako MUNGU wa Mbinguni anaweza kuzungumza na Wewe kutokea ndani ya Malaika wake, Hakikisha tu unajifunza Biblia ili uwe na Ufahamu wa kujua "Hapa anazungumza Malaika kama Malaika na hapa anazungumza MUNGU kutokea ndani ya Malaika"



7. MUNGU anaweza kusema na wewe kutokea sehemu maalumu aliyoipanga yeye wakati huo.


◼️Mfano  hai MUNGU alimwambia Ezekieli aende uwandani na huko atazungumza nae.


Ezekieli 3:22 "Na mkono wa BWANA ulikuwako juu yangu huko; akaniambia, Ondoka, enenda uwandani; nami nitasema nawe huko."


◼️Kumbe MUNGU anaweza kuchagua sehemu ambayo atasema na Wewe, hivyo uwe mtii sana kwa ROHO MTAKATIFU ili akupe kufika sehemu ambayo MUNGU atapanga kusema na Wewe.

Mfano Unaweza ukashangaa rohoni Mwako unasikia Kufunga na kuomba na ukapata msukumo wa kwenda porini ili ufunge siku tatu Kisha urudi, kumbe huko unakoenda kufanyia Maombi ndio sehemu MUNGU amepanga kusema na Wewe, unashangaa Ukiwa huko unapata mafunuo mengi ya MUNGU na kumbe MUNGU aliandaa eneo hilo ili aseme na Wewe.


Siku Moja Mimi nilipata msukumo wa Kufunga siku 3 nikamuomba Mchungaji mmoja kwamba niwe pale Kanisani siku 3 katika ya wiki kwa sababu siku hizo hakuna Ibada Kanisani akanikubalia.

Nikaamua Maombi yangu niyafanyie madhabahu, usiku baada ya Maombi siku ya kwanza tu nikajipumzisha MUNGU alisema na Mimi kwa ndoto na maono jumla kama 7 na kitu Cha ajabu nilipoamka sikusahau hata ndoto Moja, na ujumbe ule aliosema nami niliufanyia kazi.


◼️MUNGU anaweza kuchagua eneo akasema na Wewe Kwa muda huo Ukiwa katika eneo hilo.

Hata MUNGU kuzungumza na Musa kwenye kijiti haikuwa bahati tu Bali ulikuwa mpango kamili wa MUNGU kuzungumza na Musa eneo hilo siku hiyo.


Kutoka 3:3-4 " Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa."


  ◼️ Ndugu fuata sana maelekezo sana ya ROHO MTAKATIFU maana kuna sehemu anaweza kukupa msukumo wa kwenda mahali fulani kumbe MUNGU anataka kusema na wewe huko.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments