USIMHUKUMU MTU KWA HISTORIA YAKE MBAYA YA ZAMANI.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Ngoja nianzie hapa, Ukisoma Hesabu 24:17 Biblia inasema"Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia."


➡️"Namwona lakini sio sasa", "namtazama lakini sio kwa ajili ya siku za Karibu ila atatokea", hii Ina maana mojawapo kwamba Kuna watu wamewekwa kwa ajili ya kuja kutokea baadae katika kusudi la MUNGU.


➡️Inawezekana kabisa Mtu fulani alivyo Sasa Inaweza kuwa tofauti na atakavyokuwa baadae.


◼️Andiko linamzungumzia Bwana YESU KRISTO katika Unabii kwamba MUNGU alishapanga atatokea na atafanya mambo makuu.

Hata wakati anazaliwa Inawezekana waliokuwa wanamuona akiwa Mtoto Kisha  baadae akiwa Kijana Mdogo walimuona ni wa kawaida tu, wangeambiwa huyo ndio Mwokozi wa ulimwengu wote wasingekubali.


➡️Bwana YESU KRISTO hakuwahi kuwa na historia mbaya, yeye historia yake ni nzuri Mwanzo mwisho ila kwetu kama Wanadamu Inawezekana kabisa Kuna watu tunawadharau au tunawaona ni wa kawaida tu lakini wamebeba hatima kubwa baadae.


➡️Kuna watu hadi katika safari ya Maisha yao walikuwa waovu au watu wa chini lakini Neema ya Wokovu wa KRISTO ilipowapata historia yao ikabadilika.


➡️Ni kweli yamkini Kuna Mtu unamfahamu alikuwa na historia mbaya zamani lakini sio sasa.

Watu wengi hukosea kwa kuhukumu watu kutokana na historria zao za zamani .


◼️Ngoja nikupe Mfano huu.


Amosi 7:12-15 " Tena Amazia akamwambia Amosii, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosii akajibu akamwambia Amazia, MIMI SIKUWA NABII, WALA SIKUWA MWANA WA NABII; bali NALIKUWA mchungaji, na MTUNZA MIKUTU; naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli."


 ➡️Amazia hakuamini kama Amosi mtunza bustani ya miti na mchungaji wa Wanyama angeweza kuwa Mtumishi mkuu wa MUNGU katika Taifa kwa wakati ule.


✔️✔️Ndugu usimhukumu Mtu kwa historia yake ya zamani, MUNGU anaweza kumbadilisha na kumfanya kuwa Mtu mkuu baadae.


◼️Kuna wengine hawakuwahi kukaa wakaamini kama Neno jema kuliko yote linaweza kutoka katika Kijiji kidogo kiitwacho Nazareth.


Yohana 1:46 "Nathanaeli akamwambia, LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETH? Filipo akamwambia, Njoo uone."


✔️✔️ Ndugu unayejifunza ujumbe huu elewa kwamba eneo la Mtu alikozaliwa au kukulia haliamui hatima ya Mtu husika ila MUNGU wa Mbinguni ndio anaamua hatima njema ya Mtu kama Mtu huyo akiamua kumcha MUNGU katika Wokovu wa KRISTO YESU.


➡️Inawezekana Historia ya Nazareth haikuwa nzuri sana kama ambavyo historia ya Mji Fulani au Kijiji Fulani sio nzuri kulingana na watu, lakini MUNGU anaweza kuchagua eneo hilo atoke Mtu mashuhuri.


➡️Leo kuna Watu wanahukumiwa kwasababu ya Maisha yao ya dhambi zamani, elimu zao ndogo, wanakotoka, kabila zao,  ukoo wao n.k

➡️ Utasikia "kwanza alifeli hivyo hafai", "alishazalishwa huyo hivyo hawezi kuolewa",  "hana akili huyo", "huyo  ni wa kufa muda wowote",  "alikuwa mchawi",  "alikuwa kahaba" n.k

◼️Historia hizo ni kweli ni mbaya ila Mtu huyo akiamua Kuokoka na kuishi maisha matakatifu historia yake inabadilika na MUNGU anamrudisha kwenye kusudi la kumuumba Mtu huyo.


2 Wakorintho 5:17 "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya."


➡️Wewe unayependa kuhukumu Watu naomba nikushauri.

Ndugu, usipende kuhukumu Watu.


Ndugu usichokijua ni kwamba YESU KRISTO hakuja kwa ajili ya wenye haki au waliokamilika bali alikuja kwa ajili ya wenye kasoro ili azirekebishe.


Mathayo 9:13 "Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi."


◼️Wengi YESU akiwaokoa historia zao hubadilika.


➡️Huyo mwenye dhambi, mwenye mapungufu baada ya kumpokea YESU KRISTO na kuacha mabaya ya zamani usimhukumu kwa ajili ya yale ya zamani 


◼️Kumbuka  MUNGU anaweza kumpa kuishi hata yule Mtu yule ambaye  watu walimwandikia kwa vinywa vyao kuwa atakufa.


Zaburi 102:20 "Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa."


◼️MUNGU humpa kustahili hata yule mnayejua hastahili siku zote.


Wakolosai 1:12 "mkimshukuru BABA, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru."


Mimi Peter Mabula Mtu mmoja nilikuwa Secondary aliwahi kuniambia neno lililoniumiza sana wakati ule alisema ”Wewe hufai kwa lolote maana hujui hata kuongea"

Jambo lile liliniuma sana kwa wakati ule lakini miaka ilivyoenda nikalisahau.

Baadae Bwana YESU akaniokoa na sasa namtumikia. 


Mfano sasa vipi yule ndugu akinikuta Kanisani leo nafundisha akiniona youtube nahubiri au redioni nafundisha?

Na alisema kwa Sauti kubwa kwamba Mimi sifai kwa lolote.


◼️Ndugu usimhukumu Mtu kwa ajili ya historia yake ya kinyonge ya zamani.


◼️Rahabu alikuwa kahaba lakini baadaye hakuwa kahaba tena maana alifanyika Mwana wa MUNGU kama walivyokuwa Waisraeli wengine.


Yakobo 2:25 "Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?"


➡️Inawezekana wewe unamfahamu Musa yule jamaa tu mwenye kigugumizi,aliyetoroka nje aliyokuwepo,  haeleweki  lakini huyo huyo mwenye kigugumizi ndiye yule Biblia inasema hakuwahi kutokea Nabii kama Musa katika Israeli.


Kumbukumbu la Torati 34:10-12 " Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye BWANA alimjua uso kwa uso; katika ishara zote na maajabu yote, ambayo BWANA alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote."


◼️Rafiki usimhukumu Mtu kwa historia yake ya zamani, YESU KRISTO anaweza kubadilisha watu.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments