KUWA SHAHIDI WA KRISTO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.


◼️Kuna watu ni mashahidi ya kile MUNGU amefanya kwenye Maisha yao hivyo watu hao huelezea kwa ujasiri kile MUNGU amefanya.


✔️✔️Shahidi ni Mtu aliyeona akathibitisha au ni Mtu aliyeshuhudia na ushuhuda wake ni kweli.


◼️Kuna watu ni mashahidi ya kile YESU KRISTO amefanya hivyo watu hao hubaki mashahidi waaminifu kwa MUNGU.


◼️Kuna watu hadi MUNGU Mwenyewe ilifika hatua akatangaza kwamba ni mashahidi wake.


 Isaya 43:10-12 " Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni MUNGU."


➡️Sasa Kuna watu ni mashahidi wa Bwana YESU KRISTO ambao siku zote wako tayari kutangaza Wokovu wake na matendo yake kwa ujasiri.


◼️Haijalishi wanapitia mazingira gani ila wamebeba ushuhuda wa KRISTO daima na wako tayari kutangaza kazi za KRISTO siku zote.


➡️Hebu ngoja nikupe Shuhuda 3 kuhusu Mimi kabla sijakuambia sifa za Shahidi wa KRISTO zilivyo.



◾Siku Askofu Mkuu Moses Kulala anafariki ilikuwa ni tarehe 29/08/2013, siku hiyo naikumbuka kwa sababu kuu 2, tarehe 29 mwezi ni tarehe yangu ya kukumbuka kuzaliwa, pili siku hiyo usiku nilijikuta katika Maono yaliyonipeleka Mbinguni, lango la Mbinguni lilipofunguliwa nikawa busy kushangaa tu Uzuri wake yaani nilikuwa nikiangalia sehemu Moja nasahau kuangalia pembeni au kuangalia sehemu nyingine kwa sababu ya Uzuri wa kule, yaani nikiangalia mbele nitaangalia huko tu hata kama ni siku nzima bila kuangalia pembeni, katika hali ile ghafla Malaika akaniita ndipo macho yangu yaliyopoangalia upande wa kulia nikaona kiti Cha kung'aa na Bwana YESU KRISTO akiwa amekaa kwenye kiti hicho, kiti hicho lilikuwa Karibu sana na Mimi ila kwa kule kushangaa kwangu nilikuwa sijakiona.

Bwana YESU akanionyesha Moses Kulola Mbinguni Kisha akaniambia kwamba Mimi ni mmoja wa Watumishi wake Tanzania, katikati  ya wale Watumishi nilipoangalia Duniani wakati akinieleza niliwaona wengi sana ila niliyemfahamu kwa urahisi ni Mwl Mwakasege, niliona watu wengi mno ambao Moses Kulola aliwahubiria baadae nikaona mamilioni ya watu ambao Watumishi wa Bwana YESU KRISTO wote waliobaki Tanzania wanatakiwa kuwahubiria.

Tangu siku hiyo nikijitambua na kujua wajibu wangu katika kazi ya MUNGU.


✔️Kwa njia ya kuona hivyo ni Mfano hai wa kuwa Shahidi wa Wokovu wa KRISTO maana niliona Kwa ukubwa na niliona hata Watumishi wengine wakati wamemaliza safari.


◾Siku Moja Tena  miaka michache tu  iliyopita katika ndoto Bwana YESU KRISTO alinitokea na akaniambia nikawambie watu fulani waje kwake, nikaanza kuwaambia nikiwaelekeza kwa YESU KRISTO na Kila nikimwangalia Bwana YESU namuona akiwa pale pale kwenye mlima na watu ninaowaambia habari zake wengine wakimfuata pale na wengine wakikataa.


◼️Hiyo ni sehemu ya kuwa Shahidi maana YESU KRISTO ni halisi na Wokovu wake ni ndio ya Milele.


◾Siku nyingine Tena  pia siku 3 kabla ya kumaliza mwaka 2010 nilipata ajali mbaya sana ya gari kiasi kwamba madaktari wakatangaza kwa ndugu zangu kwamba sitapona kwa sababu damu imechanganyikana na ubongo, wakasema natakiwa nipelekwe India haraka lakini hadi process zifanyike walisema nisingekuwa hai, na hayo waliyasema siku ya pili nikiwa nimelazwa hospitalini na yalikuwa yamepita zaidi ya masaa 14 sijazinduka tangu baada ya ajali.

Katika hali ya ajabu kwa saa 15 ambayo nilikuwa nimezimia Mimi nilijiona katika ulimwengu wa roho, mara nikajiona Mbinguni Kisha nikasikia Sauti ikisema "Daktari wa Duniani amesema hutapona ila Daktari wa Mbinguni YESU KRISTO amekuponya" Kisha nikaanza kuonyeshwa Maono ya baadae kuhusu Mimi na Ndoa yangu na huduma yangu, Kumbuka wakati huo nilikuwa Kijana Mdogo na muda wa kuoa ulikuwa bado ila MUNGU akanipa Neema ya kuona mambo ya Baadae kuhusu Mimi.

Wakati Maono yanaisha nikazinduka na kukuta ndio Daktari anawaambia kwamba sitapona, niliposikia Sauti hiyo sikuwa na hofu yeyote maana YESU amesema ameniponya.

Baada ya hapo nilianza kupata mabadiliko ya haraka katika mwili wangu kiasi kwamba iliwachanganya hadi madaktari kiasi kwamba siku ya 7 nikaruhusiwa kutoka hospitali nikiwa mzima Kabisa, na ndani ya mwezi mmoja sikuwa hata na kovu mwilini, Kumbuka wakati ajali nilipata makovu makubwa kichwani, mikononi na tumboni lakini baada ya mwezi mmoja hata alama tu za makovu zilikuwa zimefutika.


✔️Hapo nilikuwa Shahidi wa YESU KRISTO mponyaji hivyo Nina ujasiri wa daima wa kumwambia Mtu yeyote anayeumwa ugonjwa wowote kwamba "Bwana YESU KRISTO anaweza kukuponya" au "Bwana YESU KRISTO atakuponya au amekuponya"

Na nimeona watu wengi sana wamepona kwa Maombi tu katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi.


✔️Ninaamini na Wewe uliyeokolewa na Bwana YESU KRISTO ni Shahidi wake katika mambo mbalimbali aliyoyafunua kwako au uliyoona akitenda Kwa wengine au ulisimuliwa na Watumishi waaminifu wa MUNGU.


Luka 1:2 kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,


➡️Sasa Shahidi wa YESU KRISTO yukoje?


1. Huyu ni Mtu aliyefunuliwa maandiko akaelewa kusudi la MUNGU.


1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."


◼️Mtu huyu amelielewa Neno la MUNGU kiasi kwamba hamna namna unaweza kumtoa kwa YESU KRISTO, kupitia Neno la MUNGU amefanyika Shahidi wa Bwana YESU KRISTO.


 2. Shahidi wa KRISTO ni Mtu amemuona KRISTO kwenye Maisha yake.


◼️Shahidi  wa KRISTO ameona kazi za  KRISTO KRISTO.


➡️Hata mitume walikuwa ni mashahidi kwa sababu waliona kazi za Bwana YESU.


Matendo  10:39 "Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini."


 3.  Shahidi wa YESU KRISTO ni Mtu  amejaa ROHO MTAKATIFU  hivyo anajua afanye nini kama shahidi wa YESU KRISTO.

Ushahidi wa namna hii kuwahitaji watu kuhubiri kuhusu YESU KRISTO Mwokozi kwa vivywa vyao

                

Matendo  1:8" Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi."


  4. Shahidi wa KRISTO YESU habadilishwi na mazingira, yupo tayari kuendelea na KRISTO hata kwenye hatari kuu.


◾Mfano hai ni Antipas 

 Ufunuo  2:13 ''Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani."


◼️Hivyo Shahidi wa YESU KRISTO ni Mtu  yule ambaye yuko tayari kwa lolote ilimradi asimkose YESU KRISTO.


◼️Mtu huyu hata Ndugu zake au wazazi wakimtenga hawezi kumwacha YESU KRISTO, natamani Mtu huyo awe ni Mimi na Wewe Ndugu.

Petro siku Moja alisema "twende kwa nani Tena wakati Wewe YESU KRISTO una Maneno ya Uzima" yaani maana yake hakuna pembeni pa kwenda Wewe Bwana YESU KRISTO unatosha.


Yohana 6:68 "Basi Simoni Petro akamjibu, BWANA! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele."


Ndugu Hakikisha katika Maisha Yako yote unakuwa Shahidi wa Bwana YESU KRISTO.

Jifunze hata kwenye Biblia matendo ya Bwana YESU KRISTO ili uzidi sana kuwa Shahidi wake mwaminifu.

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments