![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
◾Hizi ni Ibada ambazo Wanadamu huzifanya, aina Moja tu ndio Ibada ya kweli ambayo ni Ibada ya MUNGU katika KRISTO YESU Kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.
Waebrania 12:28 "Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na mwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee MUNGU ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho;"
➡️Nje na Ibada hii Kuna Ibada zingine ambazo zote ni Ibada machukizo kwa MUNGU, Lengo la ujumbe huu uzijue ibada zote ili zile mbaya uziepuke.
➡️Kumbuka Wokovu wa MUNGU ulikuja kwa njia ya Waisraeli hivyo Mtu asiyemwabudu MUNGU wa Israeli huyo anaabudu ama shetani au anaabudu asichokijua, na MUNGU wa Israeli ndio MUNGU wa Mbinguni anayeabudiwa katika KRISTO YESU Kwa njia ya ROHO MTAKATIFU, nje na MUNGU huyu watu wanaabudu miungu.
Yohana 4:22 "Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi."
◾Aina ya Ibada ambazo Wanadamu huzifanya.
1. Kuna watu hufanya Ibada kwa MUNGU kwa usahihi katika KRISTO YESU kwa nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Matendo 13:2 "Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia."
◼️Watu hawa ni watu waliookoka yaani wamempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao Kisha wanaishi Maisha Matakatifu yanayoongozwa na Neno la MUNGU Kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.
◼️ Ibada hii huambata na Nguvu za ROHO MTAKATIFU, ROHO MTAKATIFU huzungumza katika Ibada ya namna hii.
◼️Hii ndio Ibada sahihi kwa Wanadamu wote, watu wanaomwabudu MUNGU Kwa njia hii ndio MUNGU Mwenyewe anawatafuta sana.
Yohana 4:23-24 " Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu BABA katika roho na kweli. Kwa maana BABA awatafuta watu kama hao wamwabudu. MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli."
2. Kuna watu hufanya ibada ya sanamu.
1 Wakorintho 10:14 "Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu."
➡️Ibada ya sanamu ni kuabudu vitu na sio kumwabudu MUNGU.
Isaya 40:18-20 " Basi, mtamlinganisha MUNGU na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani? Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha. Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika."
➡️Kumbuka MUNGU hachangamani na kitu chochote kinachoonekana kwa macho hivyo ukijifanya unamwabudu MUNGU huku umeshika kitu au umeelekeza macho Yako au uso wako kwenye kitu chochote wewe unafanya Ibada ya sanamu.
➡️ibada ya sanamu ni mchukizo kwa MUNGU wa Mbinguni.
◼️Hata tabia chafu hutengeneza Ibada ya sanamu kwa mhusika.
Waefeso 5:5 "Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU."
◼️Ibada hii huambatana na kuendelea na dhambi ingawa unafanya ibada.
Wakolosai 3:5 "Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;"
◼️Ndugu kama unafanya Ibada ya sanamu ya namna yeyote iache kuanzia Leo.
Amua kuanzia Leo Kuokoka ili uanze kumwabudu MUNGU wa Mbinguni katika Kweli yake.
3. Kuna watu huabudu ibada walizojitungia wenyewe.
Wakolosai 2:23 "Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili."
➡️Hii ni Ibada ya kujitungia, Mfano wake ni wale watu ambao kwa tamaa zao walimchagua Mtu mtakatifu wa zamani wanaanza kumwabudu, ni machukizo.
➡️Ibada hii hata kama ina hekima ndani yake haimkamilishi mtu, ni Ibada ambayo ni machukizo kwa MUNGU wa Mbinguni.
◼️ Ndugu kama unafanya Ibada uliyojitungia au mliyojitungia kama Kundi na ni kinyume na ROHO MTAKATIFU Ibada hiyo ni machukizo.
◼️ Ndugu, Usikubali kuabudu kwa Ibada za kujitungia.
Amua Kuokoka na Anza kumwabudu MUNGU katika KRISTO YESU Kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.
4. Kuna watu humwabudu MUNGU bure.
Mathayo 15:8-9 "Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.''
➡️Hawa humwanudu MUNGU wa Mbinguni kinyume na maagizo yake, Mfano watu hawa humwabudu MUNGU wa Mbinguni ila hawataki kuokolewa na YESU KRISTO, hao wanamwabudu MUNGU bure na hawana sehemu katika Ufalme wake.
➡️Hata kama watu hawa wanamtaja YESU mara chache chache na wanamwabudu MUNGU wa Mbinguni lakini wanaabudu bure kwa sababu moja tu wanafuata maagizo ya wanadamu na sio maagizo ya MUNGU.
➡️Ibada hiyo ni kumwabudu MUNGU Bure.
◼️Ndugu Amua Kuokoka Kisha Anza kumwabudu MUNGU katika KRISTO YESU Kwa njia ya ROHO MTAKATIFU ili ujitenge na Ibada za kumwabudu MUNGU Bure.
5. Kuna watu huabudu miungu
➡️mfano ni hawa ambao waliabudu miungu iitwayo Artemi.
Matendo 19:27 "Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu."
➡️watu hawa walifanya ibada kwa miungu.
Mfano Mwingine ni huyu ambayo aliabudu miungu iitwayo Baali.
1 Wafalme 22:53 "Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake."
➡️hata baadhi ya watu wa MUNGU hunaswa kuabudu miungu.
Kumbu 29:26 "wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye;"
◼️ Ndugu naomba utambue kwamba mungu yeyote anayeabudiwa na watu wa dini yeyote ile ambayo Iko kinyume na Wokovu wa KRISTO YESU watu hao wanaabudu miungu.
◼️ Ndugu, kama Viongozi wako wa dini wanakufundisha kumwabudu mungu huku wakikukataza kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako tambua Leo dini hiyo mnaabudu miungu.
◼️Ndugu kuanzia Leo nakuomba mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako, amua Kuokoka na Anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu, hapo ndipo utaingia ndani ya Ibada ya MUNGU wa Mbinguni.
6. Kuna watu humwabudu shetani.
2 Wathesalonike 2:4 "yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho MUNGU ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la MUNGU, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye MUNGU."
➡️Shetani ni muongo daima.
➡️Watu Hawa waabudu shetani ni watu hatari sana na hujikuta Wana roho za kishetani sana maana wanamwabudu shetani.
➡️Watu hawa huingia mikataba na mashetani hivyo hujikuta wanamwabudu shetani na baadae anaweza hata akawaua kabla hawajamgundua ili wakimbilie kwa YESU waokoke.
➡️Hawa wakati Mwingine wanaweza kumuua Mkristo wakidhani wanampendeza mungu wao na kumbe mungu wao ni shetani ila wao hawajui.
Yohana 16:2 "Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada."
◼️Ndugu jitenge na shetani kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.
◼️Ndugu okoka ili uanze kumwabudu MUNGU kwa usahihi .
◼️Anza kumwabudu MUNGU katika KRISTO YESU kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.
2 Timotheo 1:3 "Namshukuru Mung6u, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments