KINACHOTOKEA MUNGU AKIKASIRIKA, USIMKASIRISHE

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda Kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.

Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.


◼️Kuna mambo yanaweza kutokea MUNGU akikasirika baada ya Mtu kumkasirisha.


◼️Kumbuka MUNGU sio mwepesi wa hasira 


Zaburi 145:8 "BWANA ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,"


◼️Ingawa MUNGU sio mwepesi wa hasira ila  hawezi kumhesabu Mtu mwenye dhambi kwamba hana dhambi hadi atubu katika KRISTO YESU.


Nahumu 1:3 "BWANA si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; BWANA ana njia yake katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake."


◼️Ingawa MUNGU si mwepesi wa hasira ila usifikie hatua ya kumkasirisha, wapo waliomkasirisha wakapata madhara mabaya.


Zaburi 106:29 "Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia."


➡️Hawa walimkasirisha MUNGU akawapiga kwa ugonjwa wa tauni wakafa wengi, hayo ndio matokeo ya kumkasirisha MUNGU na ukachelewa kutubu katika KRISTO YESU.


◼️Ndugu Jitahidi usifikie hatua ya kumkasirisha MUNGU.


◾Baadhi ya mambo yanayoweza kumkasirisha MUNGU Kwa haraka.


1. Kuabudu miungu.


Kumbu 32:16" Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo."


➡️Ukitaka umkasirishe MUNGU Kwa haraka sana basi abudu miungu.


◼️Ushauri wangu usiabudu miungu kamwe bali Mwabudu MUNGU katika kweli yake ambayo ni KRISTO YESU.


2. Kufanya machukizo ya kichawi na kiganga.


2 Wafalme 17:17 "Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha."


➡️Ukitaka umchukize MUNGU Kwa haraka nenda kwa waganga wa kienyeji, fanya matambiko, tegemea mizimu au ingia mikataba na Nguvu za giza.

Ukifanya hivyo utamkasirisha MUNGU haraka sana.


◼️ Ndugu Hakikisha huendi kwa waganga wa kienyeji na Wala Hakikisha hushirikiani na mizimu ya ukoo.


3. Kuabudu sanamu.


Zaburi 78:58 "Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao."


➡️Kuabudu sanamu ni kuabudu kitu chochote kinachoonekana kiwe ni picha ya bikra Mariamu, mawe, miti au sanamu yeyote na mnyama au Mtu au kitu chochote.

Ukitaka umkasirishe MUNGU haraka sana basi abudu sanamu yeyote au hata iheshimu badala ya MUNGU.


◼️ Ndugu, katika Maisha Yako yote usiabudu sanamu Bali mwabudu MUNGU wa Mbinguni aliyejifunua katika Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.


4. Mtu wa MUNGU kuingia mapatano na mawakala wa shetani.


Ezekieli 16:26 "Tena umezini na Wamisri, jirani zako, wakuu wa mwili; ukaongeza mambo yako ya kikahaba, ili kunikasirisha."


◼️Kwa Wewe Mtu wa MUNGU yaani umeokolewa na Bwana YESU KRISTO Ukitaka umkasirishe MUNGU haraka sana basi ingia mapatano na mawakala wa shetani.


◼️Ndugu, katika Maisha Yako yote Usikubali kamwe kuingia mapatano na mawakala wa shetani wa namna yeyote.


◾Ili kupona kwenye hasira ya Mungu fanya yafuatayo haraka 


1. Tubu haraka ikitokea umemkasirisha MUNGU.


➡️Mfano hai ni Musa ambaye alitubu haraka kwa ajili ya makosa ya Waisraeli walipoabudu ndama wa dhahabu, na MUNGU akataka kuwaangamiza.


Kumbu 9:18-19 " Nikaanguka nchi mbele za BWANA siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao."


◼️Ndugu, ukimkosea MUNGU tubu haraka sana na usirudie dhambi.


2. Uwe mwepesi wa kutubu na kuacha mabaya yanayomkasirisha MUNGU.


➡️Mfano hai ni watu wa Ninawi ambao waliposikia tu Neno la MUNGU waliingia Maombi ya toba ya Kufunga siku 3 na wakaacha Dhambi, MUNGU akawasamehe, hawakupata adhabu yake.


Yona 3:6-10 ' Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie MUNGU kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende."


3. Ishi Maisha ya toba mbele za MUNGU katika KRISTO YESU.


Matendo  3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"


Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.

MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)

Ubarikiwe.

Comments