![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU Mwenyezi. |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Kuna wakuu Wengi Wewe mfuate Mkuu wa Uzima.
Katika Matendo sura ya 3 Mtume Petro anawashangaa Wayahudi kuhusu kufa na kufufuka kwa YESU lakini kitu kikubwa zaidi Akawaambia YESU KRISTO ndio Mkuu wa Uzima.
Matendo 3:14-15 " Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule MKUU WA UZIMA, ambaye MUNGU amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake."
◼️YESU KRISTO ni Mkuu wa Uzima na tukiwa na YESU MUNGU huwa anatupa ROHO MTAKATIFU ndani yetu ambaye naye ni Mkuu kuliko mkuu wa dunia ambaye ni shetani.
1 Yohana 4:4 "Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia."
◼️YESU KRISTO ndiye Mkuu wa Uzima, Acha kufuata wakuu Wewe mfuate Mkuu wa Uzima.
◼️Kwa Mkuu wa Uzima hata aliye mkuu wa ulimwengu hana Nguvu mbele yake.
Yohana 14:30 "Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu."
◼️Ndugu YESU KRISTO ndiye Mkuu wa Uzima.
◼️Kama Kuna Mtu unamjua ni Mkuu sana, YESU KRISTO ni zaidi ya wakuu wote, amua kumfuata YESU KRISTO.
➡️Hata kama Kuna Kuhani anajiita kuhani Mkuu, huyo sio, YESU KRISTO ndiye Kuhani Mkuu kupita makuhani Maarufu wote, hivyo nakuomba sana Mfuate Bwana YESU KRISTO.
Waebrania 3:1 "Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, YESU,"
◼️Kama Kuna Mchungaji wako ni Mkuu sana, nipo hapa kukuambia kwamba YESU KRISTO ndiye Mchungaji Mkuu wa Wachungaji wakuu wote, hivyo mfuate YESU KRISTO Mwokozi.
1 Petro 5:4 "Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka."
➡️Kuna Wachungaji ni Maarufu sana na washirika wao inafika kipindi kwenye vivywa vyao hawamtaji Tena YESU KRISTO bali wanawataja Wachungaji wao Maarufu, Ndugu YESU KRISTO ndiye Mchungaji Mkuu wa Wachungaji wakuu wote hivyo mfuate yeye na mtaje yeye zaidi.
Waebrania 13:20-21 " Basi, MUNGU wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu YESU, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa YESU KRISTO; utukufu una yeye milele na milele. Amina."
➡️ Inawezekana Kuna Rais au Mfalme unamkubali sana kwa sababu ni Maarufu sana, Niko hapa kukuambia kwamba YESU KRISTO ni Mkuu wa Wafalme wote, hivyo mfuate yeye.
Ufunuo 1:5 "tena zitokazo kwa YESU KRISTO, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,"
◼️Kama Kanisa lenu ni Maarufu sana, YESU KRISTO ni Mkuu kuliko Kanisa lolote, hivyo mfuate yeye.
◼️Kama dhehebu lenu ni Maarufu sana na Lina Nguvu sana, tambua kwamba YESU KRISTO ni Mkuu kuliko hekalu na dhehebu lolote na dini yeyote hivyo mfuate yeye.
Mathayo 12:6 "Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu."
◼️ Mfuate Bwana YESU KRISTO Kwa sababu Ufalme wake hauna mwisho, wafalme wengine wote Falme zao zina mwisho wake ila YESU KRISTO Ufalme wake hauna mwisho hivyo mfuate yeye.
Luka 1:32-33 " Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, NA UFALME WAKE UTAKUWA HAUNA MWISHO."
➡️Ndugu, Viongozi wengi wa dini hufundisha watu kufuata dini na sio YESU KRISTO, wengine hufundisha watu kufuata dhehebu au tamaduni fulani na sio kumfuata YESU KRISTO, Ndugu nakuomba sana Wewe kuanzia Leo mfuate Bwana YESU KRISTO Mwokozi maana yeye ndiye Mkuu wa Uzima.
➡️Kuna watu wako busy kumfuata Nabii na sio kumfuata YESU KRISTO Mwokozi, Ndugu tambua kwamba YESU KRISTO ndiye Pekee Nabii Mkuu hivyo mfuate YESU KRISTO na sio kuwafuata Manabii wapotoshaji wa kweli ya Injili, YESU KRISTO ndiye Pekee Nabii Mkuu hivyo mfuate.
Luka 7:16-17 " Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, MUNGU amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando."
◼️YESU akasema ndiye MUNGU Mkuu hivyo ukimfuata YESU KRISTO umemfuata mkuu wa Uzima aliye juu ya vyote.
Tito 2:13-14 " tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema."
◼️ Ndugu unauhitaji Wokovu wa Bwana YESU KRISTO kuliko chochote unachokihitaji hivyo hivyo mpokee YESU KRISTO Mkuu wa Uzima ili upate uzima wa Milele.
Waebrania 2:10 "Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments