Bwana YESU KR
![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
ISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Somo la leo tunaangalia mambo matano ambayo Kila Mtu Duniani anatakiwa kuyatamani sana.
Ayubu 6:8 "Laiti ningepewa haja yangu, Naye MUNGU angenipa neno hilo ninalolitamani sana!"
➡️Inawezekana Kuna mambo unayatamani sana, kama ni mambo mema hamna tatizo ila haya 5 chini yatamani zaidi.
Mambo 5 unayotakiwa kuyatamani Zaidi.
1. Tamani Neno la MUNGU.
1 Petro 2:2 "Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;"
◼️Ni agizo la Biblia ni vyema Kila Mtu tangu anapompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake, Mtu huyo atamani kujifunza Neno la MUNGU.
◼️Neno la MUNGU ndio Lina majibu Yako yote ya vitu unavyovitamani, hivyo tamani kwanza Neno la MUNGU na Anza kujifunza na kuliishi Kila kitu kwako kitawezekana.
➡️Neno la MUNGU ndilo Lina mausia Bora ya kukusaidia, watu mashuhuri zamani walitamani Neno la MUNGU na kufanyia kazi likawa msaada kwao.
Zaburi 119:40 "Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako."
➡️Ukitamani Neno na ukazingatia utafaidika na mengi.
◼️Ukitamani Neno la MUNGU katika ROHO MTAKATIFU ujue umetamani mafanikio Yako ya Kila namna.
◼️Ukitamani Neno la MUNGU katika KRISTO YESU ujue umetamani ushindi wako wa Kila namna.
◼️Ukitamani Neno la MUNGU ujue ukifanyia kazi utatembea kwenye ushindi wako.
2. Tamani Maisha ya mbinguni.
Waebrania 11:16 "Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo MUNGU haoni haya kuitwa MUNGU wao; maana amewatengenezea mji."
◼️Ukitamani Maisha ya mbinguni itakufanya umpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako na uishi Maisha matakatifu daima ili uje uishi Mbinguni baada ya mwisho wa kuishi kwako duniani.
◼️Hakuna asiyependa kuishi kwenye uzima wa milele hivyo tamani kuishi Mbinguni na hiyo itakusaidia kufanya mema na kujitunza katika KRISTO YESU ili ufike Mbinguni.
◼️Mtu anayetamani kuishi Mbinguni hana mchezo na MUNGU na hana mchezo na Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.
3. Tamani kuwa na karama za rohoni.
1 Wakorintho 14:12 "Vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa."
◼️Karama za rohoni ni utendaji kazi wa ROHO MTAKATIFU kupitia Mteule wa KRISTO.
➡️Zipo karama nyingi ukiitamani sio kosa, ishi tu Maisha matakatifu na msikilize ROHO MTAKATIFU anakwambia nini.
1 Wakorintho 12:7-11 " Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye."
◼️Karama za rohoni ni utendaji kazi wa ROHO MTAKATIFU ndani ya Wateule wa YESU KRISTO.
1 Wakorintho 14:1 "Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu."
◼️Karama za MUNGU zitakufanya uwe Mtu mkuu na zitaleta mafanikio mengi kiroho na kimwili.
◼️Inawezekana Kuna Watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU wengi unaowafahamu zaidi iwe walioishi zamani au Sasa, unaowafahamu kwa sababu tu ya karama za ROHO MTAKATIFU ndani Yao, hivyo tamani karama za rohoni kama unataka kwenye Maisha Yako uwe fulani.
4. Tamani Wokovu wa MUNGU.
Zaburi 119:174 "Ee BWANA, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu."
◼️Wokovu wa MUNGU ni msaada wa MUNGU ,tamani kusaidiwa na MUNGU.
◼️Wokovu pia ni kuokoka hivyo tamani kuokoka utafanya vyema sana utafanikiwa sana kiroho na kimwili Kisha Uzima wa Milele.
5. Tamani kwenda kuishi na KRISTO wakati wako wa kuishi duniani ukiisha.
Wafilipi 1:23 "Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na KRISTO maana ni vizuri zaidi sana;"
➡️Paulo anatupa kielelezo Cha kitu kizuri Cha kutamani, yeye alitamani kwenda kuishi na KRISTO YESU Mbinguni na ilikuja kuwa hivyo.
◼️Ukitamani kwenda kuishi KRISTO aliko utampokea KRISTO YESU kama Mwokozi wako na utaishi Maisha matakatifu kama KRISTO alivyo mtakatifu, hivyo tamaa Yako itakuwa njema sana.
1 Petro 1:15-16 " bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."
◼️Ndugu, ukiyatamani mambo haya matano na ukayaishi utakuwa mshindi Duniani na baada ya Maisha ya ushindi Duniani utaenda Uzima wa Milele.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments