MUME NA MFALME ALIYEFANYA MABAYA KWA USHAWISHI WA MKEWE.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

➡️Katika  ujumbe wa leo tunamwangalia Mume na mfalme aliyefanya mabaya kuliko wafalme wote waliomtangulia kwa sababu ya ushawishi wa mkewe.

1 Wafalme 21:25 "(Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea."

  ➡️Katika Taifa la Israeli zamani kulikuwa na Falme mbili, Ufalme wa kaskazini ulioitwa Ufalme wa Israeli na Ufalme wa kusini ulioitwa Ufalme wa Yuda.
Sasa kabla ya Ahabu kuwa Mfalme walikuwa wametawala wafalme 9 ingawa wafalme 3 kati yao  Walitawala Israeli nzima ambao ni Sauli, Daudi na Sulemani, na kabla ya Ahabu kuanza kutawala walikuwa wametawala wafalme 6 yeye akawa wa 7 kutawala Ufalme wa Kaskazini.

◼️Kitu Cha Ajabu Biblia inasema ni hiki "hapakuwa na Mfalme kama Ahabu aliefanya mabaya kuliko wafalme wote waliomtangulia kwa kuchochewa na Mkewe "

➡️Ukiangalia Wafalme waliomtangulia wengi wao walifanya mabaya sana kama akina Yeroboamu, akina Baasha, akina Zimri na wengine na Biblia inasema baadhi yao waliwakosesha Taifa Zima Mfano ni huu

1 Wafalme 15:33-34 " Katika mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya alianza kutawala juu ya Israeli wote huko Tirza, akatawala miaka ishirini na minne. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwa5na akaiendea njia ya Yeroboamu, na kosa lake ambalo kwa hilo aliwakosesha Israeli."

◼️Licha ya Wafalme hao waliomtangulia Ahabu walifanya mabaya lakini Hakuna hata mmoja kati yao aliyefanya mabaya kuliko Ahabu.

◼️Biblia inasema Ahabu alifanya mabaya kwa MUNGU kuliko viongozi wote wakuu wa nchi yake walimtangulia na sababu ya yeye kufanya mabaya hayo ni Moja tu ni kwa sababu ya Mkewe aitwaye Yezebeli.

1 Wafalme 16:30 "Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia."

 ➡️Hapa tunajifunza kwamba ndio Ina Nguvu ya kubadilisha Hatima.
Kuna hatima njema na Kuna hatima mbaya, kwa Ahabu ndio ilileta hatima mbaya sana.

◼️Ninaposema haya Wapo Wanawake ambao walikuwa na YESU KRISTO na wanamcha MUNGU ila hatima njema ikaondoka kwa sababu ya waume  zao ambao ni wapinga KRISTO.

◼️Wapo Wanaume ambao walikuwa na YESU KRISTO wakimcha MUNGU ila hatima zao njema zikaondoka kwa sababu ya Ndoa, walioa wapinga KRISTO.

➡️Chanzo cha yote kwa Ahabu hadi akafanya maovu kuliko wafalme wote waliomtangulia ni kuoa Mwanamke wakala  wa shetani aitwae Yezebeli.

1 Wafalme 16:31 "Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia."

➡️Mwanamke huyu Mchawi na wakala wa shetani ambaye Baba yake  alikuwa kuhani wa miungu alikuwa  ametumwa na shetani kwa Ahabu ili amfabye Ahabu kuwa chukizo kuliko wafalme wengi wote waliomtangulia.
Yaani kama ni Duniani ya Leo ingesemwa kwamba Rais wa awamu ya Saba amefanya mabaya kuliko Marais wote waliomtangulia kwa sababu ya ushawishi wa kishetani kutoka kwa Mkewe.

◼️Ndugu zangu Ndoa ni kitu Muhimu sana na Cha kukiendea kwa umakini sana Ukitaka ubaki na Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.

➡️Yezebeli alipofika tu Ikulu kazi yake ya kwanza ya kishetani ilikuwa kugeuza moyo wa Ahabu jambo la pili  alileta ibada ya shetani Ikulu ya nchi.

1 Wafalme 16:32 "Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria."

➡️Ahabu nae baada ya kugeuzwa moyo na mkewe akaanza kuwa msimamizi wa kujenga majengo ya kumwabudia shetani katika nchi yote ya Israeli.

1 Wafalme 16:33 "Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia."

Ahabu kwa kuanza kusimamisha madhabahu za shetani katika nchi ndio maana akawa ni aliyefanya mabaya kuliko wafalme wote waliomtangulia, maana madhabahu za giza ndio chanzo kikuu Cha maovu na makosa mabaya kwa jamii kubwa.

➡️Hata wewe Leo angalia kule ambapo madhabahu za MUNGU katika KRISTO YESU ni chache huko kumejaa madhabahu za giza nyingi na maovu huko ni mengi zaidi hasa umwagaji damu.

➡️Ahabu hakuishia tuu kuamrisha watu wamwabudu shetani bali alianza hadi uuaji akiwanyang’anya Watu wema ardhi zao na alifanya haya kwa sababu ya mke wake mchawi na wakala wa shetani.

1 Wafalme 21:7, 13-16 " Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli..................  Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana MUNGU na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa.
 Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki."

➡️Katika kipindi Cha kutawala Cha Ahabu Watumishi wa kweli na MUNGU katika Taifa walibaki wachache sana, maana wengi waliuawa chini ya Uongozi wa Ahabu aliechochewa na Mke wake, hata hao Watumishi wa MUNGU wachache hakutaka wamwambie mambo walioambiwa na MUNGU ili wamwonye.

1 Wafalme 22:18 "Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?"

◼️Kitendo cha kukataa maonyo Ya MUNGU kulipelekea ujumbe mkali wakutangaza mwisho wake na mwisho wa mkewe.

1 Wafalme 21:19-20 " Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa BWANA."

➡️Tangazo la Mbinguni mabaya kwa Ahabu na Yezebeli likatimia.

1 Wafalme 22:37-38 " Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria. Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la BWANA alilolinena."

➡️Lakini kabla ya hapo Ahabu alisababisha mateso hadi kwa taifa zima.

1 Wafalme 18:18 "Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za BWANA; nawe umewafuata mabaali."


◾Tunajifunza nini 

1. Mwanandoa usikubali mwenza wako kukushiwishi Kwenda kinyume na MUNGU wa Mbinguni.

Kumbu 13:6-8 " Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako; katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia; usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;"

2. Kama hujaingia katika Ndoa usikubali kuingia katika Ndoa mpinga KRISTO au  mtu ambae familia yao ni mawakala wa shetani.

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

◼️Fanya mambo Yako yote katika KRISTO YESU KRISTO, nje na hapo Kuna shetani.
Hata Ndoa Hakikisha ni Ndoa Takatifu katika KRISTO YESU tu.

3. Kiongozi usikubali ushauri wowote unaopelekea jamii unayoiongoza kinyume na KRISTO YESU.

Mithali 28:6 "Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri."

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe. 

Comments