![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU Mwenyezi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi.
◼️Iko wazi kabisa kwamba MUNGU anaweza kumpa Mteule wake Nguvu za kuwashinda maadui zake.
➡️Mfano hai ni Daudi ambaye alipewa na kuwashinda maadui zake Kila alikokwenda.
2 Samweli 8:6 "Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda."
◼️MUNGU anaweza kumfanya Mteule wake kuwa Mtu asiyeshindwa dhidi ya watu wanaotumika kipepo.
Yeremia 15:20 "Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA."
◼️Kwa sababu umempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako Wewe una sifa zote MUNGU kukulinda na kukupa Nguvu za kuwashinda mawakala wa shetani wote wanaofanya vita na Wewe haijalishi ni majini, mizimu, Wachawi, waganga wa kienyeji au mawakala wa shetani wengine, katika KRISTO YESU Kwa njia ya Maombi unao uwezo wa kuwashinda wote na wakati wowote.
Mimi Peter Mabula ni Shuhuda nyingi juu ya hili, hivyo nasema kitu ambacho hata Mimi mwenyewe nimeshuhudia kwa macho yangu mara nyingi Mimi mwenyewe au Wateule wa KRISTO wengine wakishinda Nguvu za giza kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
Warumi 8:37 "Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda."
◼️Bwana YESU KRISTO amewapa Wateule wake Mamlaka kubwa sana, kupitia Maombi tunashinda.
Luka 10:19 "Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."
◾Sasa Utamshindaje adui mwenye nguvu?
1. Ushindi wako uanze na Imani kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
◼️Mfano hai ni Kalebu aliyekuwa na Imani kubwa kwa MUNGU.
Hesabu 13:30 "Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka."
◼️Hata wewe Hakikisha una Imani kubwa kwa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Kumbuka MUNGU hutupa kushinda katika KRISTO YESU Pekee.
1 Wakorintho 15:57 "Lakini MUNGU na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu YESU KRISTO."
2. Kwenye maombi kwa Imani tamka ushindi unaouhitaji.
◼️Uwe kama Elisha aliyetamka kwa Imani akiumba mshale wa MUNGU wa kuwapiga Washami na ikawa hivyo.
2 Wafalme 13:17 "Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza."
3. Hakikisha MUNGU yupo na wewe yaani umeokoka unaishi Maisha matakatifu, unafuata maeleekezo ya ROHO MTAKATIFU na unatembea kwenye Neno la MUNGU ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
◼️Kumbuka MUNGU atakuwa pamoja na Wewe kama ukiamua kuwa naye katika KRISTO YESU.
2 Nyakati 15:2 "naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; BWANA YU PAMOJA NANYI, MKIWA PAMOJA NAYE; NANYI MKIMTAFUTA ATAONEKANA KWENU; LAKINI MKIMWACHA ATAWAACHA NINYI."
4. Tumia Mamlaka ya jina la YESU KRISTO kushinda, tamka ushindi kwa kinywa chako kwenye Maombi.
Luka 21:15 "kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga."
5. Omba kwa kutumia Neno la MUNGU maana Neno la MUNGU lina nguvu ambayo hakuna adui anaweza kushindana nayo.
Matendo 19:20 " Hivyo ndivyo neno la BWANA lilivyozidi na kushinda kwa nguvu."
◼️Ukimtegemea MUNGU wa Mbinguni hakika utashinda dhidi ya kila maadui wa kimwili na kiroho.
◼️Kwa YESU KRISTO ushindi wa kiroho ni lazima .
◼️ Ndugu Endelea kuomba na kuishi Maisha matakatifu ya Wokovu utamuona MUNGU wa Mbinguni.
◼️ Ndugu Endelea kwenda Kanisani, kwenda kwenye mikutano ya Injili, kwenda kwenye Semina za Neno la MUNGU na kwenye Maombi utamwona MUNGU wa Miujiza.
Wafilipi 4:13 "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments